Maaskofu wataka haki kwa kila mtu

Padri Deogratias Matiika  akifukizia ubani kwenye pango mtoto Yesu wakati waibada ya misa takatifu ya mkesha wa sikuku ya Krisimasi iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Paulo wa Pili Parokia ya Korongoni Moshi mjini.Picha na Dionis Nyato


Muktasari:

  • Baadhi ya maaskofu na viongozi wa makanisa, wamekemea kauli za chuki zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali, huku wakitaka Watanzania watendewe haki.


Dar/ Mikoani. Baadhi ya maaskofu na viongozi wa makanisa, wamekemea kauli za chuki zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali, huku wakitaka Watanzania watendewe haki.

Waliyesema hayo walipokuwa wakihubiri katika ibada za mkesha na za Krismasi juzi na jana.

Viongozi hao pia wamehimiza upendo na amani katika mkesha wa Krismasi ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo.

Akitoa mahubiri kwenye mkesha wa Krismasi ambao kitaifa ulifanyika Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kondoa, Askofu Dk Given Gaula aliwataka viongozi kutenda na kuchunga kauli zao ili ziwe faraja kwa Watanzania badala kuanzisha chuki na migogoro.

Askofu Dk Gaula alisema kauli za kuwaeleza watu kama vile wakaishi Burundi wakati ni Watanzania, hazijengi kwani zinawafanya wengi kuwa na utulivu lakini hawana amani mioyoni mwao.

“Hata katika Taifa kama hakuna furaha kwa sababu ya ugumu wa maisha, kwa ajili ya ukatili wa watu na uonevu, watu wanaweza kuwa na utulivu lakini hawana amani.Unaweza kuwaambia wakimbilie Burundi lakini hawawezi hapa ni kwao,” alisema Dk Gaula.

Aliendelea: Hapa ni kwao walizaliwa hapa waliishi hapa, hawawezi kukimbilia Burundi hapa ni kwao, usifanye maisha yao kuwa magumu Bwana asifiwe, na Mungu anakuona. We baba ukiwa katili pia Mungu anakuona,” alisema.

Dk Gaula alisema pia kumekuwa na uonevu kwa baadhi ya viongozi hasa watendaji wa vijiji na kata ambao wanaonea watu na kufanya migogoro ya wakulima na wafugaji isiishe licha ya utulivu walionao wananchi.

“Mnaweza kuwa na utulivu msiwe na amani, mnaweza kuwa na amani msiwe na upendo, bahati nzuri Tanzania tunaweza kuwa na vyote, lakini kuna baadhi ya watendaji wa kata na vijiji ni wakatili sana,” alisema Dk Gaula.

Alizungumzia pia migogoro ya wakulima na wafugaji akisema ni kutokana na mioyo ya watu kutokuwa na Mungu.

Kwa upande wa wanasiasa, alisema ni wakati wa kuheshimiana ili chama kilichopo madarakani, kisiwakandamize wasio madarakani. Lakini alisema wasio madarakani nao wawaheshimu walioko madarakani.

Naye Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo, alivitaka vyombo vya dola wakiwamo mahakimu na majaji kutenda haki na kuepuka kuwaonea na kuwatesa wengine kwa kufikiri Mungu haoni

Machinga watajwa

Akihubiri jana katika ibada ya Krismasi ndani ya Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu jijini Dodoma, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk Dikson Chilongani aliwataka viongozi kujishusha kwa watu wa chini na kujua matatizo na changamoto zao kabla ya kutoa maagizo.

Askofu Chilongani alizungumzia kuhusu machinga ambao alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakitoa maagizo wakiwa kwenye viti vyao, bila kujishusha kuona mahitaji ya kundi hilo.

Alisema hana uhakika kama baadhi ya viongozi wanajua shida wanazopitia machinga, ila wao wakiwa kwenye viti wa utukufu juu wanatoa maagizo ambayo mwisho wake hayaleti msaada kwa kundi hilo.

“Sina uhakika kama kweli baadhi ya viongozi wanajua hali ya maisha ya wamachinga; wao wanatoa magizo wakiwa kwenye viti vyao vya enzi, hiyo siyo sifa ya kiongozi. Wanatakiwa kushuka chini na kujifunza maisha ndipo watoe maagizo,” alisema Dk Chilongani.

Alitolea mfao wa Yesu Kristo ambaye aliacha utukufu na enzi akashuka kwa wanadamu na kujua hali zao kisha kapaa mbinguni.

Uviko- 19

Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki la Kondoa, Bernadin Mfumbusa aliwataka waumini kutambua kuwa janga la Uviko-19 bado lipo duniani hivyo watu wachukue tahadhari kwa kufuata maelekezo na ushauri wa wataalamu.

Askofu Mfumbusa alikuwa akihubiri katika ibada ya kitaifa iliyofanyika ndani ya Kanisa la Kiaskofu Parokia ya Roho Mtakatifu Kondoa, alitumia muda mfupi na kusisitiza waumini kufuata maagizo ya wataalamu ili kujikinga na Uviko-19.


Ukatili

Askofu wa jimbo wa Katoliki la Shinyanga, Liberatus Sangu alisema kutokuwa na hofu ya Mungu, kumekuwa chanzo cha matukio mengi ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Askofu Sangu alitoa kauli hiyo juzi usiku kwenye ibada ya mkesha wa Krismasi iliyofanyika katika kanisa la Mama Mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga, akiwataka Watanzania kumlilia Mungu ili kukomesha matukio hayo.

“Bila kuwa na upendo hakuna amani, hakuna umoja ni wakati sasa wa kubadilika na kutenda matendo ya kumpendeza Mungu na kuepuka kufanya mambo ambayo yanachochea kuongezeka maovu yakiwamo wizi, ubakaji na ufisadi,’’ alisema.

Alisema kuna baadhi ya viongozi wanaotaka kujilimbikizia mali kutokana na uchu walionao, pasipo kutambua athari zake.