Mabalozi India, Korea kushindana kusafirisha maparachichi ya nchini

Muktasari:

  • Wakati kontena la kwanza la futi 40 lililosheheni maparachichi kutoka Njombe likifungua milango nchini India, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Mavura amesema anaweka mambo sawa ili Tanzania iuze matunda hayo nchini humo.

Wakati kontena la kwanza la futi 40 lililosheheni maparachichi kutoka Njombe likifungua milango nchini India, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Mavura amesema anaweka mambo sawa ili Tanzania iuze matunda hayo nchini humo.

Awali, Tanzania ilipeleka sampuli ya kilo 200 za maparachichi kwenda nchini India kwa ajili ya kuyatambulisha, lakini Mei 4 biashara ikaanza hivyo kuwatia moyo zaidi wakulima nchini.

Biashara hiyo ilifanikishwa na kampuni ya IG Fruits ya India, iliyosafirisha kontena lililokuwa na trei 5,700 za matunda hayo ambazo kila moja ilikuwa na kilo nne, ikimaanisha shehena hiyo ilikuwa na uzito wa tani 22.8.

Imekuwa safari ndefu ambayo sasa imeanza kuzaa matunda, kwani Novemba 25 mwaka jana ndipo mamlaka nchini India ziliridhia maparachichi kutoka Tanzania kupelekwa nchini humo baada ya kujiridhisha na ubora wake na baada ya miezi sita ya maandalizi muhimu biashara imeanza kufanyika.

“Leo tarehe 4 Mei 2022 ni siku adhimu ambapo kwa mara ya kwanza ubalozi wa Tanzania nchini India tumepokea kontena la maparachichi kutoka Tanzania kupitia kampuni ya IG Fruits ya nchini India. Mapokezi haya yamefanyika katika Bandari ya Jawaharlal Nehru Mumbai. Huko nyuma tuliwahi kupokea shehena ya kilo 200 ambayo ilikuja na ndege yetu ya ATCL. Tunaishukuru kampuni ya Kamal Agro Processing kwa kutufungulia na kutambulisha zao hili katika soko la India,” aliandika Anisa Mbega, balozi wa Tanzania nchini India kwenye ukurasa wake wa Twitter.


Juhudi zinaendelea Korea

Kwenye taarifa ya Balozi Anisa katika ukurasa wake wa Twitter, Balozi Mavura alionyesha mshawasha wa kuwafungulia fursa Watanzania katika Taifa hilo anakowawakilisha.

“Hongera sana Mheshimiwa Balozi Anisa Mbega kwa kuliwezesha hili. Nami niko kwenye mchakato wa kuingiza parachichi hapa Korea,” aliandika Balozi Mavura akimjibu Balozi Mbega.

Alipotafutwa ili kupata ufafanuzi wa hatua anazozichukua kuwatafutia wakulima wa maparachichi nchini soko la mavuno yao, Balozi Mavura alieleza mambo kadhaa ambayo yakikamilika kila kitu kitakaa sawa.

“Kuna mahitaji makubwa, ila tunakwamishwa na taratibu za kuingiza matunda na mimea, ni ngumu sana hapa Korea. Hii ni changamoto inayozikumba bidhaa za nchi za Afrika,” alisema.

Wakati mchakato wa kukamilisha utaratibu wa kuingiza maparachichi ukiendelea, taarifa zinaonyesha Tanzania inauza kahawa na tumbaku nchini Korea Kusini.


Mipango ya kitaifa

Kuingia kwa mzigo huo nchini India ni mwendelezo wa kutafuta masoko mapya ya maparachichi ya Tanzania duniani ambayo mwaka 2021 ilisafirisha jumla ya tani 11,237 zenye thamani ya dola 33 milioni za Marekani, takwimu za Chama cha Wakulima wa Bustani Tanzania (Taha) zinaonyesha.

Mapato hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 12.6 yakilinganishwa na ya mwaka 2020. Mpaka mwakani, Taha inasema Tanzania inatarajiwa kuuza nje tani 15,000 za maparachichi na kuingiza dola 45 millioni.

Mkurugenzi wa Taha, Dk Jacquline Mkindi anasema Tanzania huzalisha tani 40,000 za maparachichi kila msimu na idadi inazidi kuongezeka kwa asilimia 20 kila mwaka, kwani wananchi katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Songwe, Iringa, Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Kigoma, Kagera na Morogoro wameichangamkia fursa hiyo vizuri.

Taha ndio waliowezesha kupeleka shehena nchini India, huku Tanzania ikiendelea kupeleka matunda hayo katika mataifa ya Ufaransa, Uholanzi na Uingereza.

“IG Fruits iliunganishwa na Taha kuyafikia mazao hayo nchini. Zipo kampuni nyingine nyingi zilizoonyesha nia ya kununua maparachichi kutoka Tanzania baada ya kujiridhisha na ubora. Tunaendelea kuzishawishi nyingine. Watanzania tutoke kwenye maneno twende kwenye utekelezaji,” anasema Balozi Anisa.

Baada ya IG Fruits kuonyesha nia ya kununua zao hilo, Dk Jacquline anasema waliiunganisha na wakala wa usafirishaji, Avoafrica ya nchini.

“Kampuni hiyo (Avoafrica) ndiyo ilikuwa inakusanya mazao kutoka kwa wakulima. Tulifanya hivyo ili wakutane na madalali ambao wangetuharibia soko, tuliona ni vema tuwaunganishe na kampuni kubwa inayotambulika,” anasema.

Avoafrica ni kampuni ya kizalendo yenye makao makuu mjini Makambako mkoani Njombe.

Kutokana na kuimarika kwa soko la matunda hayo, wakulima wamepata matumaini makubwa zaidi ya kuimarisha mashamba.

“Nilikuwa na ekari 12 za maparachichi, kwa jinsi masoko yanavyoongezeka, natarajia kuongeza nane,” anasema Saidan Kenan, mkulima wilayani Kilolo.