Mabasi mawili, lori la mafuta yateketea, barabara yafungwa

Muktasari:

  • Jeshi la Zimamoto, Polisi waendelea na jitihada kuuzima moto wa lori la mafuta uliotokana na ajali ya mabasi mawili ya Sauli na New Force yaliyokuwa yanatoka Mbeya na Tunduma wenda Dar es Salaam. Polisi imesema mtu mmoja amefariki dunia na wengine kujeruhiwa.

Pwani. Mabasi mawili yaliyokuwa yakitoka Mbeya na Tunduma kwenda Dar es Salaam yameteketea kwa moto baada ya kugongana na lori la mafuta katika eneo la Ruvu mkoani Pwani usiku wa kumamkia leo Alhamisi Machi 28, 2024.

Mabasi yaliyohusika kwenye ajali hiyo ni Sauli na New Force. Sauli linafanya safari zake Dar –Mbeya na New Force Dar- Tunduma.

Akzungumzia ajali ilivyotokea, Kamanda wa Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amesema magari ya Saul na New Force yalikuwa yanafukuzana, “sasa katika kuovateki basi la Sauli likaona lori linatoka upande wa Dar, kurudi nyuma dereva akashindwa, hivyo akagonga chumba cha mwisho kwenye lori la mafuta na New Force kwa kuwa nalo lilikua kasi, likaligonga Sauli kwa nyuma hivyo ndivyo ikatokea ajali."

"Baada ya kutokea kwa ajali hii, moto mkubwa ulilipuka na kusababisha mabasi haya kuwaka moto pamoja na lori lenyewe, moto ulikuwa mkubwa kiasi kwamba magari mengine yalishindwa kutembea, hasa yale yanayotoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na yale ya Morogoro kwenda Dar," amesema.

Kamanda huyo amesema mpaka sasa mtu mmoja amefariki dunia na wengine kujeruhiwa.

Amesmea kwa sasa “tunapambana kuhakikisha magari hayo yaliyoungua tunayaondoa barabarani ili watumiaji wengine waweze kutumia Barabara, maana baada ya moto hakuna gari lililopita na foleni kutoka pande zote ni kubwa, hivyo tutapumua kama magari yataanza kutembea."

Saa 5 asubuhi wakati vikosi vya ulinzi na usalama vikiendelea kuzima moto, lori la mafuta liliripuka tena na moshi mkubwa ukatanda, hivyo kuwafanya askari pamoja na viongozi wengine kukibia umbali kadhaa.

Kutokana na hali hiyo, barabara haijaanza kutumika na magari yanayotoka Dar es Salaam na au Morogoro yanatumia barabara ya zamani ya Mlandizi yakilazimika kupita kwa zamu kwa kuwa njia si nzuri na  foleni kubwa.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi