Maboresho ya sheria yalivyosaidia kesi za ujangili

Maboresho ya sheria yalivyosaidia kesi za ujangili

Muktasari:

  • Kati ya kesi 37 za ujangili zilizofunguliwa kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka jana katika Mahakama za Arusha, Dodoma na Manyara, Serikali imeshinda kesi 26 na imeshindwa kesi tatu.

Kati ya kesi 37 za ujangili zilizofunguliwa kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka jana katika Mahakama za Arusha, Dodoma na Manyara, Serikali imeshinda kesi 26 na imeshindwa kesi tatu.

Miongoni mwa kesi hizo, saba ziliondolewa mahakamani na Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP) huku moja ikiendelea.

Kamishna Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (Tanapa), Paschal Shelutete anabainisha hayo baada ya kuulizwa kuhusu kesi zilizoripotiwa kuhusu ujangili.

Akizungumzia changamoto za kesi za ujangili zinazotoka hifadhi za Mikumi mkoani Morogoro na Tarangire, Manyara, Shelutete anasema ni pamoja na ukusanyaji wa vielelezo kwa kufuata utaratibu, mashauri kuchelewa, mashahidi huru wanaotokana na wananchi kutopatikana kutoa ushahidi, majalada kupotea na shauri kufutwa.

“Changamoto nyingine ni askari wa hifadhi kukosa uelewa wa sheria wakati wa ukamataji majangili, hivyo kusababisha upungufu katika kesi husika na kuchelewa kwa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuwalipa mashahidi huru,” anasema Shelutete.

Mwaka 2017, mkazi wa Dodoma, Boniface Malyango maarufu ‘Shetani hana huruma’ alinusurika kifungo cha miaka 32 jela baada ya kukosekana kwa ushahidi kuhusu makosa matatu yanayohusiana na ujangili.

Awali, Malyango na wenzake wawili walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za ukusanyaji, usafirishaji na uuzaji vipande 118 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh1.9 bilioni.

Kwa mujibu wa Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mwajuma Lukindo, Malyango hakutiwa hatiani baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa hana hatia yoyote, hivyo kunusurika kifungo cha miaka 32 jela.

Hata hivyo, mwaka 2019, mfanyabiashara maarufu wa China aliyepewa jina la “Malkia wa pembe za ndovu” alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa makosa ya usafirishaji kimagendo zaidi ya pembe 350 za ndovu kwenda barani Asia.


Wanasheria wanasemaje?

Kuhusu kesi za ujangili, Mwanasheria Paul Kadushi anasema zipo kwenye matabaka mbalimbali, wakiwamo watu wanaowinda kwa ajili ya kupata nyamapori na wanaowinda kwa biashara ambao ndio wanajihusisha na usafirishaji haramu.

“Hata hawa wanaowinda kwa ajili ya nyamapori, kuna wengine wanaowinda kwa kiasi kikubwa na kufanya biashara; na si ile ambayo mtu anakwenda kuwinda kwa ajili ya kula na familia yake, hawa pia huwa tunawaweka katika kipengele cha usafirishaji haramu wa wanyamapori,” anasema Kadushi.

“Hata wanaowinda kwa ajili ya kula na familia, huo pia ni uwindaji haramu, hivyo ni lazima apate kibali.”

Akizungumzia mafanikio ya kuendeshaji kesi za ujangili, Kadushi anasema, “ni makubwa kwa sababu kati ya mwaka 2009 hadi 2014, tulipoteza asilimia 60.3 ya tembo wote nchini kwa ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo, lakini Serikali ilichukua hatua kwa kufanya maboresho hasa kwa kuanzisha kitengo maalumu kwenye ofisi ya DPP.”

Kwa mujibu takwimu za Serikali zilizotolewa Juni 2015, tembo nchini walipungua kutoka 109,051 mwaka 2009 na kufikia 43,330 ilipofika mwaka 2014.

Hata hivyo, idadi hiyo iliongezeka kufika 60,000 mwaka 2019 hadi ikalazimika kuundwaq vitengo maalumu ambavyo Kadushi anasema ni mahususi kwa ajili ya kuendesha kesi hizo na pia kikosi kazi cha kutokomeza ujangili. Vilevile waliongeza adhabu katika sheria ya wanyama pori na kuboresha usimamizi wa kesi kuanzia ngazi ya upepelezi.

“Lakini, DPP alitoa mwongozo au maelekezo namba moja mwaka 2017, kwa ajili ya upelelezaji na uendeshaji wa kesi za wanyamapori na misitu. Maelekezo ambayo kisheria yalikuwa yanalenga kuboresha usimamizi na uratibu mzuri wa upelelezi ili kufanikisha ushindi wa kesi pindi zinapofunguliwa mahakamani,” anasema.

“Kwa hiyo, yote hayo yalifanikisha kupatikana kwa mafanikio makubwa. Na katika kesi kubwa kubwa, zote tulishinda; na ujangili kwa kiasi kikubwa ulipungua kwa sababu wale majangili walikuwa wapo magerezani ama wanaendelea na kesi zao au wengine wameshafungwa.”

Kadushi anasema, unapokuwa ‘unawakaba’ majangili wakubwa, wadogo wanakuwa hawana tena ushawishi wa kufanya ujangili kwa maana hata wakiua tembo wanakuwa hawana mtu wa kumuuzia.

“Hata wale wasafirishaji wakubwa wengi tulifanikiwa kuwakamata na kuwaweka magerezani.”


Changamoto za kesi

Kadushi anasema “pengine changamoto pekee ni pale unapohitaji ushahidi kutoka nchi nyingine, sasa haya maombi ya ushahidi nchi za nje, hasa kama meno ya tembo yamekamatiwa nchi fulani, ili maombi hayo yakubaliwe itategemea na utashi fulani wa nchi hiyo, hata kama kuna mikataba ya kimataifa inayokwazwa na hilo eneo.”

Anasema pamoja na kuwapo kwa hiyo mikataba, hiari ya nchi huwezi kuilazimisha, kwa hiyo mara nyingine ushahidi unaweza kufika kwa kuchelewa.

Akizungumza katika moja ya mikutano kwa njia ya Zoom, Mwanasheria Simon Wankyo anasema uchunguzi kuhusu masuala ya uhujumu uchumi kama biashara ya dawa za kulevya au usafirishaji wa binadamu, utakatishaji fedha chafu, uhalifu wa wanyamapori unapaswa kufanywa na wachunguzi maalumu waliopata mafunzo.

Wankyo anasema wachunguzi na waendesha mashtaka wanapaswa kujua vizuri mahitaji ya sheria zinazohusika za kesi hizo. “Mwendesha mashtaka mzuri anapaswa kuwasiliana na vyombo vyote vya usimamizi ili kuwezesha uchunguzi wa kesi husika.”


Adhabu

Kwa mujibu wa Kadushi, awali sheria ilikuwa inaeleza kuwa mtu atakayekutwa na hatia adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka 15, licha ya kesi za ujangili kuwa katika kipengele cha uhujumu uchumi.

Anasema kifungo hicho kinamaanisha kuwa, mtu anaweza akapewa hukumu hata mwezi mmoja kwa sababu haujazidi miaka 15.

“Kwa hiyo katika sheria namba 3 ya mwaka 2016, makosa haya ya wanyamapori niliyosema tangu zamani ni makosa ya uhujumu uchumi, adhabu imeongezwa, kwa maana kifungo cha chini ni jela miaka 20 na cha juu ni miaka 30,” anasema mwanasheria huyo.

Akifafanua adhabu, mwanasheria huyo anasema Mahakama pia inaweza kutoa adhabu ya mtu kulipa faini mara kumi ya thamani ya nyara ya Serikali ambayo amekamatwa nayo.

“Mathalani kama mtu amekamatwa na jino la tembo ambalo utaalamu unaonyesha aliyeuawa ni tembo mmoja; kwa sababu tembo ana meno mawili, ina maana tembo mmoja kwa mujibu wa kanuni zile za nyara za Serikali, tembo mmoja ni Dola 15,000 za Marekani, kwa maana hiyo, Mahakama inaweza kutoa adhabu mtu huyo kulipa mara kumi ya thamani hiyo ambayo ni sawa na Dola 150,000 za Marekani kwa tembo mmoja pamoja na kifungo cha miaka 20 au 30.”

Kuhusu mtu aliyenunua nyama au ngozi lakini akakamatwa nayo kwa kuhusishwa na ujangili, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Maurus Msuha anasema kuna msemo usemao “aliyekutwa na ngozi ndio kaua mnyama.”

Hata hivyo, anasema kama mnunuaji ana uthibitisho kwa wakati huo anapokamatwa, hiyo ni sawa, lakini kama hana atakwenda kueleza mahakamani kwamba alinunua kwa fulani.

Makala haya yameandikwa kupitia ruzuku ya Internews Earth Journalism Network.