Mabula ataka Serikali isiwaondoe wananchi kwa ajili ya wawekezaji

Muktasari:

  • Mbunge wa Ilemela (CCM), Dk Angelina Mabula ameitaka Wizara ya Madini kuacha kuwaondoa wananchi kwenye maeneo yao ardhi kwa ajili ya kuwapa wawekezaji wenye leseni ya uchimbaji madini badala yake washirikishwe kuwa sehemu ya umiliki.

Dodoma. Mbunge wa Ilemela (CCM), Dk Angelina Mabula ameitaka Wizara ya Madini kutowaondoa wananchi kwenye ardhi wanayomiliki kwa sababu ya kumpa mwekezaji, badala yake ameshauri wawe sehemu ya umiliki wa uwekezaji huo.

Mabula amesema hayo leo Ijumaa ya Aprili 5, 2024 wakati akichangia mjadala kwenye bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

“Sekta ya madini uwekezaji wake ni mkubwa, naishauri Wizara ya Madini tunapozungumzia suala la kutwaa maeneo kwa ajili ya kuwapa wenye leseni, tuangalie pia suala la kumwezesha mwenye  ardhi yake, si lazima aondolewe pale, anaweza pia akawa sehemu ya umiliki wa leseni ile ambayo mwekezaji amekuja kuwekeza hata kama atapata asilimia mbili ana uhakika wa kuendelea na maisha mazuri kwa kutumia ardhi yake.

“Tusijikite katika kuwaondoa na kuwapa kipaumbele wawekezaji, tuone namna bora ya kumshirikisha huyu mwenye ardhi yake akawa sehemu ya umiliki wa ile migodi na yeye akafurahia hata kama atapata asilimia ndogo,” amesema Dk Mabula.

Dk Mabula ambaye aliwahi kuwa waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika suala zima la miundombinu na uchimbaji, hivyo ameiomba Wizara ya Madini isiangalie kuwaondoa wenye maeneo, iangalie namna bora ya kuwawezesha na wao wafurahie maisha.


Mkakati wa Serikali

Jumatano ya wiki hii wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwasilisha bungeni mapendekezo ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2024/2025, alisema Serikali imeendelea kutekeleza dhamira yake ya kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwapatia leseni, kuwatengea maeneo maalumu na  kuwapatia mafunzo yanayohusiana na masuala ya sheria, usalama, afya na utunzaji mazingira.

“Hadi Februari, 2024 Serikali imetenga jumla ya maeneo 58 yenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,125.92 kwa ajili ya wachimbaji madini wadogo katika mikoa mbalimbali nchini.