Machinga Iringa wapewa siku tano kuhamia maeneo mapya

Mwenyekiti wa umoja wa Wamachinga Mkoa wa Iringa, Yahaya Mpelembwa.

Muktasari:

  • Manisapaa ya Iringa imetoa siku tano kwa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga, kufanya kuhamia maeneo rasmi yaliyotengwa kwaajili ya biashara hizo huku wao wakisema jambo hilo ni changamoto kwao.

Iringa. Manisapaa ya Iringa imetoa siku tano kwa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga, kufanya kuhamia maeneo rasmi yaliyotengwa kwaajili ya biashara hizo huku wao wakisema jambo hilo ni changamoto kwao.

Haya yamebainishwa na Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoani Iringa Yahaya Mpelembwa baada wafanyabiasha hao kubomolewa vibanda vyao hapo jana, huku akibainisha kuwa maeneo yaliyotengwa ni pamoja na Lavera Magorofani, Magaria Mabovu na eneo jipya la biashara Mlandege.

Mpelembwa amesema taarifa hiyo ya Wamachinga kuhamia maeneo mapya, imetolewa na uongozi wa Manispaa ukiongozwa na Mstaiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada.

Ameongezea kwa kusema kwamba uhamisho wote unaofanyika ni kutokana na makubalino ya awali katika vikao vya Wamachinga Mkoani hapo, ambavyo vilikuwa vikiwataka wafanyabiashara hao kuhamia maeneo rasmi.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mpelembwa amesema uhamisho huo wa Wamachinga ni suala la lazima maana lilitokana na vikao baina yao na Halimashauri na hivyo amewataka wafanyabiashara wenzake kufata taratibu zinazotakiwa ili kuepusha migororo.

"Mpaka kufikia jumatatu, wanapaswa wawe wamefika sehemu iliyotengwa na Manispaa kwaajili ya kufanyia shughuli zao, japo kuna changamoto maana kwa muda mrefu walizoea kutumia eneo la Magari Mabovu…kuwavunjia vibanda na taarifa inayowataka kuhamia maeneo rasmi imekuwa ni changamoto,” amesema Mpelembwa.

Kwa upande mwingine Mwenyekiti huyo amesema kuna baadhi ya ya mizigo imeharibiwa na kupotea na kwamba inakuwa ngumu kuendeleza biashara.

"Ilo suala la kuhama sio la mchezo mchezo mimi nipo hapa takribani miaka minne hivyo wateja wangu wamenizoea itakuwa tofauti na nitayumba nikihama," amesema Ester Mileje mmoja wa Wamachinga wa eneo la Magari Mabovu

Mwananchi Digital ilifanya jitihada kadhaa za kumtafuta Mstahiki Meya kwa njia ya simu bila mafanikio, hata pale lilipofika ofisini kwake iliambiwa yuko nje ya ofisi.