Madaktari Bingwa kupiga kambi siku tano Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda

Muktasari:

Kambi hiyo ya matibabu ya kibingwa itaanza Juni 12, 2023 hadi Juni 16, 2023 katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Simiyu.

Bariadi. Timu ya Madaktari Bingwa 24 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa inatarajiwa kupiga kambi ya siku tano ya matibabu bila malipo kwa wakazi wa Mkoa wa Simiyu.

Kambi hiyo ya matibabu ya kibingwa itaanza Juni 12, 2023 hadi Juni 16, 2023 katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Simiyu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bariadi Juni 6, 2023, Mkoa wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda amewaomba wakazi wa mkoa huo kujitokeza kupata huduma bila malipo ya vipimo, ushauri na tiba kutoka kwa mabingwa hao.

‘’Wataalam hao watapima na kutoa matibabu kwa magonjwa ya ndani na nje, magonjwa ya wanawake pamoja na watoto. Nawasihi wananchi wa Simiyu wajitokeze kupata huduma ambazo ni nadra kupatikana kwenye hospital zetu za Mkoa wa Simiyu,’’ amesema Nawanda.

Katika hatua nyingine, Mkoa wa Simiyu imezindua mfumo wa kuratibu huduma za Mama na Mtoto (M-mama) inayolenga kupunguza vifo vya mama na mtoto huku Dk Nawanda akiwaagiza wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kuwalipa kwa wakati madereva waliosajiliwa kutoa huduma katika ngazi ya jamii.

Jumla ya madereva 82 tayari wamesajiliwa kutoa huduma ya kusafirisha wagonjwa kutoka vijiji 470 vya mkoa huo kwenda na kutoka vituo vya huduma za afya .

Kwa mujibu wa Mratibu wa mfumo wa M-Mama Mkoa wa Simiyu, Sara William, tayari vituo 222 vya huduma vimesajiliwa katika mpango huo.

‘’Magari 14 ya kubeba wagonjwa na madereva wa magari binafsi pia wamesajiliwa na kupewa mafunzo maalum kutekeleza jukumu la kusafirsha wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura,’’ amesema Sara

Mgaga mfawidhi Hospital ya Rufaa Mkoa wa Simiyu, Dk Athanas Gambakubi ameishukuru Serikali kwa kuboresha miundombinu ya huduma za afya hospitalini hapo huku akiiomba kuongeza idadi ya wataalam bingwa kukidhi mahitaji.

Dk Gambakubi amehimiza wananchi wa mkoa huo wenye matatizo ya kiafya yanayohitaji huduma za kibingwa kutumia fursa ya kambi ya siku tano ya matibabu kupata huduma bila malipo.