Madaktari wa mifupa wapigwa msasa Dar

Madaktari Bingwa wa Mifupa kutoka nchi zaidi ya 12 wakifuatilia mafunzo kuhusu magonjwa yatokanayo na ajali wakati wa Kongamano la sita la madaktari bingwa wa mifupa duniani lililofunguliwa leo, katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi) jijini Dar es Salaam. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Ni katika mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo na mbinu mbalimbali za kutibu mifupa

 


Dar es Salaam. Zaidi ya madaktari bingwa 100 wa mifupa kutoka nchi 12 za Afrika wanashiriki mafunzo ya matibabu ya mivunjiko mbalimbali ya mifupa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI).

Mafunzo hayo ya siku tano yanalenga kuwajengea uwezo madaktari hao katika mbinu mbalimbali za kutibu mifupa na namna ya kufidia kipande cha mfupa kilichopotea kutokana na ajali.

Akizungumzia katika mafunzo hayo yaliyoanza Juni 19 na kutarajiwa kumalizika Juni 23, 2018 Mkurugenzi wa Tiba wa Moi, Dk Samuel Swai amesema taasisi hiyo inapokea zaidi ya wagonjwa 10 kila siku waliovunjika mifupa.

Amesema idadi ya wagonjwa waliovunjika mifupa ilipungua baada ya Serikali kupiga marufuku unywaji wa viroba ambapo walipokea wagonjwa 15 - 20 kwa siku.

"Tunashirikiana na Chuo Kikuu cha San Francisco cha Marekani katika kutoa mafunzo haya. Hii ni mara ya sita tutashirikiana kutoa mafunzo haya na yamekuwa na mchango mkubwa kwa madaktari wetu," amesema Dk Swai.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka MOI, Dk Billy Haonga amesema katika mafunzo hayo wanajifunza namna ya kuhudumia wagonjwa ambao mifupa imetoka nje na misuli kuhama.

Amesema mafunzo hayo yanawashirikisha madaktari bingwa 70 kutoka sehemu mbalimbali nchini na wengine kutoka Kenya, Uganda, Malawi na Nigeria.

"Tunashirikiana na madaktari bingwa kutoka Ulaya na Marekani. Tumeshirikisha madaktari wengine kutoka hospitali za mikoani zilizotuma wawakilishi," amesema.