Madereva ‘wafurika’ vituo vya mafuta

Dar/Mikoani. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeendesha operesheni ya kuwasaka madereva wanaonunua mafuta na kuacha risiti za EFD, jambo lililosababisha baadhi ya madereva kufurika kwenye vituo vya mafuta wakisubiri risiti hizo ili kuepuka faini.
Awali, kulikuwa na taarifa katika mitandao ya jamii iliyowataka wenye magari kuhakikisha wanachukua risiti hizo baada ya kujaza mafuta na wasipofanya hivyo wangetakiwa kulipa faini ya kati ya Sh30,000 na Sh1,500,000.
Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Mkurugenzi wa Elimu kwa mlipa kodi Richard Kayombo alisema faini hiyo inalenga kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kudai risiti kwa kila fedha wanayotoa.
Kayombo alisema jitihada kubwa zimefanyika kuhakikisha risiti zinatolewa kwenye vituo vya mafuta lakini changamoto inayoonekana ni wanunuaji wa mafuta kukataa kuchukua risiti hizo.
Alisema operesheni hiyo endelevu itafanyika nchi nzima na itahusisha maofisa wa TRA katika kuhakikisha wanakabiliana na changamoto hiyo.
Mfanyabiashara ambaye atabainika kutotoa risiti, Kayombo alitaja adhabu yake kuwa ni faini ya kati ya Sh3 milioni hadi Sh4.5 milioni kwa kila mauzo ambayo amefanya na kukwepa kutoa risirti.
Akizungumzia hatua hiyo, James Shayo mkazi wa Mbagala alisema itawasumbua wengi lakini inakwenda kuwajengea watanzania utamaduni wa kudai risiti.
Mkoani Kilimanjaro pia kulikuwa na heka heka ya madereva kufuatilia risiti hizo baada ya TRA mkoani humo kusisitiza wito huo.
Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Gabriel Mwangosi alisema utunzaji wa kumbukumbu ni muhimu katika kuwezesha ukadiriaji wa kodi sahihi.
Mkoani Morogoro, mmiliki wa vituo vya mafuta Omary Al-Saedy alisema amekuwa akikagua wafanyakazi wake wakati wakitoa huduma na kushuhudia wateja wakikataa kupokea stakabadhi hizo
Jijini Arusha nako hofu ilitawala kwa madereva kukamatwa na maofisa wa TRA kwa kutodai risiti
Mkazi wa Arusha Jeremiah Laizer alisema amepata taarifa kupitia mitandao ya kijamii kuna msako kwa madereva wasiodai risiti. Elizabeth Edward, Mussa Juma, Flora Temba na Maryasumta Eusebi, Hamida Shariff.