Madiwani Bukombe wapewa kazi maalum tishio la El Nino

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba

Muktasari:

Kupitia Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe, tayari Serikali imechukua hatua kukabiliana na madhara ya El-Nino kwa kuwakabidhi viongozi na watendaji wa Sekalini Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kuzuia na Kukabiliana na madhara ya El Nino.

Bukombe. Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Said Nkumba amewatwisha madiwani wa halmashauri hiyo mzigo wa kuelimisha umma katika kata zao umuhimu wa wote wanaoishi bondeni kuhama kwa hiari kuepuka athari za mvua za El Nino zinazotabiriwa kunyesha sehemu mbalimbali nchini.

Madiwani hao wamekabidhiwa jukumu hilo na Mkuu wa Wilaya ya  Bukombe, Said Nkumba kutokana na ushawishi wao kwa umma katika kata wanazoongoza.

Akihutubia kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, Nkumba amewataka viongozi hao wa kisiasa kutumia vikao na mikutano yote ya hadhara katika kata zao kuueleza umma madhara ya mvua za El-Nino zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi huu wa Oktoba.

‘’Kwa kushirikiana na wataalam katika kata zenu, kutoa elimu kwa umma kuwahimiza wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni kuhama kuepuka madhara ya mvua kubwa zinazotabiriwa kunyesha sehemu mbalimbali nchini,’’ amesema Nkumba

Diwani wa Kata ya Busonzo, Nicholaus Mayala aliahidi kwa niaba ya wenzake ktekeleza agizo hilo kwa kuwahamasisha wananchi kuhama kutoka makazi ya mabondeni kabla ya madhara.