Madiwani Ileje wataka Tanesco kuwadhibiti vishoka

Muktasari:
Madiwani katika halmashauri ya Wilaya Ileje mkoani Songwe wameliomba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuanza kutoa vibali kwa makandarasi wanaokwenda kufanya kazi ya kusuka nyaya za kuingizia huduma hiyo kwa wananchi ili kuepuka wananchi kutapeliwa.
Songwe: Madiwani katika halmashauri ya Wilaya Ileje mkoani Songwe wameliomba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuanza kutoa vibali kwa makandarasi wanaokwenda kufanya kazi ya kusuka nyaya za kuingizia huduma hiyo kwa wananchi ili kuepuka wananchi kutapeliwa.
Ombi hilo limewasiloshwa leo Jumatano Novemba 3, 2021 wakati wa kikao cha baraza la madiwani linalofanyika mjini Itumba wilayani hapa.
Wamesema kuwa kumekuwa na baadhi ya wakandarasi wanakifika kwa wananchi hata katika maeneo ambayo mpango wa kufikisha umeme haujafika na kisha kuwashawishi wananchi wawape kati ya Sh20,000 na 40,000 ili wawawekee nyaya za umeme ili kuwekewa umeme wa mpango wa REA.
Diwani kata ya Itale, Fahari Mwampashi amesema ili kudhibiti wananchi kutapeliwa na vishoka hao, Tanesco waanzishe utaratibu wa kuwatambulisha rasmi wakandarasi.
"Iwapo Tanesco mtawathibitisha hawa tutajenga imani nao lakini pia likitokea ratizo tunaweza kufahamu wapi kwa kuwapata" amesema Mwampashi
Meneja wa Tanesco Wilaya ya Ileje, Mhandisi James Bigambo amesema makandarasi hao wanapofika vijijini waulizwe leseni walizopewa na Ewura pamoja na barua kutoka Tanesco ya kumtambulisha na iwapo hana nyaraka hizo asiruhusiwe kufanyakazi katika eneo hilo.
"Sisi Tanesco hatuwezi kumpa barua mkandarasi akawasukie nyaya za umeme wateja wake katika eneo ambalo mradi haujafika, kwani tunahakikisha mradi umekamilika ndipo tunawatangazia wananchi" amesema Bigambo