Madiwani, RC Mongella wanyukana

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela

Muktasari:

  • Madiwani wa Jiji la Arusha wamemshukia Mkuu wa Mkoa huo, John Mongela wakidai amewadhalilisha kwa kuwaita wapika majungu, wafitini na wanakwamisha maendeleo.

Arusha. Madiwani wa Jiji la Arusha wamemshukia Mkuu wa Mkoa huo, John Mongela wakidai amewadhalilisha kwa kuwaita wapika majungu, wafitini na wanakwamisha maendeleo.

Wiki iliyopita, Mongela akiwa kwenye kikao na madiwani wa jiji la Arusha na watendaji wa jiji hilo kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliwatuhumu madiwani kuwa na majungu, kufitiniana na hivyo kukwamisha maendeleo ya jiji, ikiwemo ujenzi wa kituo kipya cha mabasi.

Jana akizungumza kwa niaba ya madiwani wenzake, Diwani wa Ngarenaro, Isaya Doita alisema wamesikitishwa na tuhuma za Mongella alizotoa hadharani juu yao, ambazo zimewadhalilisha na kulikuwa na fursa ya kuzungumza kupitia vikao vya chama kwani wao ni madiwani wa CCM.

“Tumeomba kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, tujadiliane atueleze matatizo yetu ili kama ni kweli tujirekebishe, lakini ninachojua mimi hakuna diwani ambaye ni kikwazo cha maendeleo,” alisema.

Doita alisema tayari wamemuomba Meya wa Jiji la Arusha, Maximillian Ilangye kufuatilia jambo hilo na kuomba kukutana na Mkuu huyo wa Mkoa na kujadiliana juu ya tuhuma alizotoa ili kurejesha ushirikiano baina yao.

“Tayari Meya amekubali na atazungumza na Mkuu wa Mkoa ili tupate hii fursa ya kuzungumza na kupata muafaka ili kuondoa sintofahamu baina yetu,” alisema.

Doita ambaye amekuwa diwani kwa zaidi ya miaka 15 sasa, miaka 10 akiwa diwani wa Chadema katika kata hiyo, alisema tuhuma za Mongela ni nzito na wameona sio busara kukaa kimya, kwani aliwataka watendaji wa jiji kuwa makini na madiwani.

“Sasa watendaji wa jiji wanatuogopa kufanya kazi, lakini pia hata Kaimu Mkurugenzi wa jiji anatuogopa kwa sababu tumetajwa na kiongozi wetu kuwa sisi ni watu hatari wapika majungu na wafitini,” alisema. Doita akizungumza kuhusiana na tuhuma za kukwamisha ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi eneo la Bondeni City, alisema katika vikao vya jiji hakukuwahi kubadilishwa msimamo juu ya ujenzi wa kituo hicho cha mabasi.

“Ni kweli hapo nyuma kulikuwa na kutokuelewana baina ya watendaji wa jiji na Mbunge Mrisho Gambo, kuhusu eneo la ujenzi wa kituo cha mabasi kutokana na Gambo kutaka kujengwa eneo la Olasiti na jiji kujengwa Bondeni City, lakini mgogoro ulikwisha,” alisema.

Alisema kauli kuwa wanashikiliwa akili na mtu mmoja, anaamini sio sawa kwani baadhi yao wamekuwa kwenye siasa kwa muda mrefu na inaonekana kuna mvutano wa viongozi na Gambo, jambo ambalo madiwani waliowengi hawahusiki.

Akizungumzia tuhuma za mikakati ya kumng’oa Meya, Doita alisema baadhi yao walikuwa wanataka kuitishwa kikao maalumu kujadili maendeleo ya jiji, hasa kutokana na kushtakiwa Mkurugenzi wa jiji, Dk John Pima na watendaji wengine kutokana na ubadhirifu.

Hata hivyo, baadhi ya madiwani wa jiji la Arusha, ambao wanatajwa kuwa karibu na Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo, wanatajwa kuwa na mkakati kumng’oa Meya kwa hoja hawezi kutengwa na tuhuma ambazo zimemfikisha mkurugenzi mahakamani.