Madiwani Rombo wahoji makato ya bima bila matibabu

Baadhi ya Madiwani wa Baraza la halmashauri ya Rombo wakiwa kwenye kikao cha robo mwaka. Picha na Fina Lyimo.

Muktasari:

  • Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro wamelalamikia utaratibu wa kujigharamia kulipa bima ya afya huku wakikatwa fedha ya bima ya afya kwa kipindi cha miezi mitatu sasa.

Rombo. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wamelalamikia utaratibu wa kujigharamia malipo ya huduma za afya huku wakikatwa fedha ya bima ya afya kwa kipindi cha miezi mitatu sasa.

Wakizungumza leo Jumanne novemba 7, 2023 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani, ambacho kimepokea na kupitisha taarifa za kipindi cha robo ya kwanza, wamesema kuwa licha ya kukatwa fehda kwaajili ya bima ya afya, kila wafikapo hospitali kwaajili ya huduma, huelezwa bima zao hazijalipwa.

Diwani Athuman Kimaro, amesema: “Tangu mwezi wa saba mwaka huu tukienda hospitali tunatumia fedha zetu za mfukoni, wakati kila mwezi tunakatwa fedha za matibabu kwenye posho tunazolipwa kila mwezi, ni masikitiko tunaambiwa hazina hawajaweka michango yetu kwenye bima."

Kwa upande wake Diwani Mallel Venance, amesema hakuwahi kuomba bima lakini amekuwa akikatwa makato bila kupata matibabu.

"Sababu ya mimi kutojaza za bima hii ni kutokana na malalamiko ya madiwani kudhalilishwa wanapofika hospitali na kuambiwa bima hazijalipwa huu ni udhalilishaji, maana unakuta kadi ya bima ipo na unaenda hospitali kwa kujiamini na bado unalipa hela kwa ajili  ya matibabu licha ya kukatwa fedha kila mwezi,” amesema Venance.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Gilbert Tarimo amemtaka mkurugenzi wa halmashauri kumaliza sintofahamu hiyo ili madiwani weweze kupatiwa matibabu bila kubugudhiwa kama ilivyo kwa wachangiaji wengine.

Akizungumza katika Baraza hilo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Godwin Chacha, amewataka madiwani hao kuwa na subira wakati suala hilo likishugulikiwa katika ngazi ya mkoa kwa kushirikiana na Tamisemi.