Maelezo mke wa bilionea Msuya anavyodaiwa kumuua wifi yake yasomwa mahakamani

Mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita

Muktasari:

  • Mke wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, Miriam Mrita ameeleza sababu na namna alivyohusika na mauaji ya wifi yake, Aneth Msuya.


Dar es Salaam. Maelezo ya onyo yanayodaiwa kuchukuliwa polisi yameeleza namna mke wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, Miriam Mrita sababu na namna alivyohusika na mauaji ya wifi yake, Aneth Msuya.

Miriam ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji hayo ya wifi yake huyo Aneth aliyeuawa Mei 25, 2016 kwa kuchinjwa shingoni nyumbani kwake, Kibada Kigamboni , jijini Dar es Salaam, amedaiwa kukiri kuhusika na mauaji hayo, katika maelezo yake ya onyo.

Katika maelezo hayo, Miriam anadaiwa kueleza kuwa aliamua kumuua wifi yake kwa sababu alikuwa anamfuata fuata katika suala la usimamizi wa mirathi ya mumewe, marehemu bilionea Msuya na kwamba katika kutekeleza mauaji hayo alimkodi mtu aliyemlipa Sh20 milioni.

Mbali na Miriam mshtakiwa mwingine katika keso hiyo namba 103 ya mwaka 2018 inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ni mfanyabiashara Revocatus Myella.

Maelezo hayo ya Miriam yalisomwa mahakamani hapo na shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, WP Sajenti Mwajuma, aliyemhoji mshtakiwa huyo na kuandika maelezo yake alipotiwa mbaroni, baada ya kupokewa mahakamani hapo kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Kwa mujibu wa maelezo hayo mshtakiwa huyo aliteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu mumewe, Bilionea Msuya ambaye  aliacha wosia kuwa asilimia 40 ya fedha alizoacha benki wapewe wazazi na dada zake na asilimia 60 iliyobaki apewe mkewe na watoto wake.

Pia marehemu bilionea Msuya alieleza katika wosia huo kuwa mali nyingine zikiwemo magari, mgodi na hoteli zinapaswa kugawanywa kwa utaratibu wa mirathi.

Mshtakiwa huyo alieleza kuwa alifungua shauri la mirathi katika Mahakama Kuu Arusha kwa kumtumia wakili aliyechaguliwa na familia.

Hata hivyo baadaye  aliliondoa shauri hilo mahakamani  bila ya kumweleza wakili aliyechaguliwa na familia sababu za kufanya hivyo na kutafuta wakili mwingine bila ya kukaa kikao na wanafamilia.

Miriam aligawa fedha hizo za benki  bila ya kuwa na mgogoro wowote asilimia 40 ilienda kwa wazazi na ndugu wa marehemu na asilimia 60 ilienda kwake na kwa watoto.

Kwa mujibu wa maelezo hayo baadhi ya mali za marehemu mshtakiwa huyo aliziorodhesha kwa jina lake jambo lililosababisha kutokuwa na maelewano mazuri na ndugu wa marehemu mume wake.

Mshtakiwa huyo alipata taarifa kuwa kuna ndugu wa mume wake jijini Dar es Salaam walipigwa risasi walikuwa wamelazwa lakini hakuwahi kuonana nao kwa sababu hawakuwa na mahusiano mazuri.

Maelezo hayo yamedai kuwa baada ya tukio hilo la kupigwa risasi dada wa marehemu Bilionea Msuya ndipo likafuatia tukio la mauaji ya Aneth.

Katika maelezo hayo inadaiwa mshtakiwa huyo alikiri kuwa ndiye aliyehusika na mauaji hayo baada ya ya kuona kuwa alikuwa anamfuata fuata sana.

Katika kutekeleza mpango wa mauaji hayo mshtakiwa huyo alieleza kuwa alimpa kazi hiyo mtu anayeitwa Ray kwa makubaliano ya malipo ya Sh20 milioni.

Mshtakiwa huyo alieleza kuwa alimpigia simu Ray na kumuuliza kama anafahamu anapoishi marehemu  Aneth lakini alimjibu kuwa hafahamu ila anajua anaishi Kibada.

Miriam alieleza kuwai Mei 15,2016 Ray alimpitia yeye mshtakiwa na wakaelekea Kigamboni eneo la Kibada wakiwa na gari lao aina ya  Range Rover ili kutafuta nyumba aliyokuwa anaishi marehemu Aneth na walipofika eneo hilo walikutana na binti wa kazi wa Aneth.

Walimuuliza binti huyo kama anapajua nyumbani kwa Aneth naye  akawajibu ni pale na yeye anaishi kwenye nyumba hiyo.

Maelezo hayo yamedai kuwa walimuuliza binti huyo kama ana simu akawajibu hana hivyo walimuahidi kumnunulia na wakakubaliana kuwa  Mei 18.2016 na wamkute nje ya nyumba hiyo na siku hiyo.

Siku hiyo, Mei 18  walikwenda na kumkuta binti huyo nje ya nyumba hiyo kama walivyokuwa wamekubaliana, hivyo wakampatia simu kwa ajili ya mawasiliano binafsi.

Wakati huo Ray alikuwa amebeba briefcase nyeusi ndani kulikuwa  na sh10 milioni lengo lao kumuonyesha binti huyo akubali ombi lao ili siku ya tukio asiwepo nyumbani badala yake alitakiwa kuondoka.

Mei 23,2016 asubuhi Miriam alimpitia Ray na jamaa zake ambapo walikutana Magomeni kwa ajili ya kazi hiyo na ilipofika Mei 25, 2016 Miriam alipelekwa mkoani Arusha.

Mei 26,2016 Miriam akiwa Arusha  alipata taarifa kwamba Aneth ameuawa kwa kuchinjwa na yeye, lakini  hakwenda kwenye mazishi kwa sababu mama mkwe wake alikuwa amemwambia kuwa ikitokea  yeye amekufa au familia ya mume wake asiende kwenye mazishi.

Mei 27,2016 Ray alisafiri na kuelekea jijini Arusha hadi kwenye hoteli ya mshtakiwa huyo ili akamaliziwe  fedha zake zilizobaki kiasi cha  Sh 10 milioni ambazo alipewa.

Baada ya kumaliza kusoma maelezo ya mshtakiwa huyo, shahidi huyo wa kwanza alieleza kuwa baada ya mshtakiwa huyo kukamatwa na kufikishwa katika Kituo cha Polisi cha Chang'ombe Agosti 7,2016 alifanyiwa gwaride la utambuzi pamoja na watuhumiwa wengine kina mama na alitambuliwa na binti huyo.