Maelfu benki zilizofilisiwa hawajalipwa fedha zao

Thursday February 04 2021
benki pic
By Sharon Sauwa

Dodoma Serikali imesema hadi kufikia mwishoni mwa Desemba mwaka jana, jumla ya Sh4.94 bilioni zimelipwa kwa asilimia 37.9 ya wateja wenye amana katika benki sita za wananchi (Community Banks) ambazo zilifutiwa leseni za biashara.

Malipo hayo ni sawa na asilimia 77.27 ya Sh6.39 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanaidi Ali Khamis alisema wateja waliolipwa ni 21,675 kati ya 57, 076 ikiwa ni asilimia 37.98 ya waliokuwa na amana zilizostahili fidia.

Mwanaidi aliyasema hayo bungeni jana wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Jang’ombe (CCM) Ali Hassan King.

“Je, Serikali imefikia hatua gani katika kufuatilia fedha za wananchi zilizopo katika benki ambazo zimezuiliwa kuendesha shughuli zao hapa nchini?”alihoji King.

Akijibu swali hilo, Mwanaidi alisema katika mwaka 2017 na 2018 Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilizifutia leseni za kufanya biashara za kibenki, benki saba kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Advertisement

Alizitaja benki zilizofutiwa leseni ya kufanya biashara nchini kuwa ni FBME Bank Ltd; Mbinga Community Bank Plc, Njombe Community Bank Ltd, Kagera Farmers’ Cooperative Bank Ltd, Meru Community Bank Ltd,Efatha Bank Ltd, na Covenant Bank for Women (T) Limited.

Alisema baada ya kuzifutia leseni benki hizo, BoT iliiteua Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kuwa mfilisi.

Alisema katika kutimiza wajibu wake wa msingi kisheria, DIB ilianza zoezi la kulipa fidia ya bima ya amana ya hadi Sh 1.5milioni kwa waliostahili malipo hayo katika benki hizo.

Alisema hatua hiyo bado inaendelea kwa wateja ambao hawajajitokeza kuchukua fidia.

Alisema sambamba na hatua hiyo, DIB inaendelea na ufilisi wa Benki hizo tajwa.

Mwanaidi alisema hadi kufikia mwishoni mwa Desemba mwaka 2020, jumla ya Sh 4.94bilioni zimeshalipwa kwa wateja wenye amana wa Benki sita za wananchi ukiiondoa Benki ya FBME.

Kuhusu Benki ya FBME, Mwanaidi alisema hadi mwishoni mwa Desemba 2020, jumla ya Sh 2.42bilioni zimelipwa kwa wateja wenye amana ambazo ni sawa na asilimia 52.13 ya Sh 4.65bilioni ambayo ni kiasi kilichotengwa kukamilisha hatua hiyo.

Alisema jumla ya wateja waliolipwa ni 3,443 kati ya 6,628 ambao ni sawa na asilimia 51.95 ya waliokuwa na amana zilizostahili fidia.

Alisema wateja waliokuwa na amana inayozidi Sh1.5 milioni watalipwa kiasi kilichobakia chini ya hatua ya ufilisi ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za Benki husika.

Alisema zoezi la kukusanya madeni na mali za benki hizo linaendelea ili kupata fedha za kuwalipa wateja wenye amana zenye thamani zaidi ya Sh1.5 milioni.

Katika swali lake la nyongeza, King alitaka kufahamu ni lini wateja hao watalipwa fedha zao zote kwa sababu benki hiyo haijafilisika.

Pia alitaka kufahamu ni lini BoT itaacha kuingiza benki za ovyo ovyo kama hiyo zikaleta madhara kwenye nchi.

Akijibu maswali hayo, Waziri wa Katiba na Sheria Mwigulu Nchemba alisema utaratibu wa malipo kwa wateja wa benki ya FBME umechukua muda mrefu kwa sababu ilikuwa inafanyakazi katika nchi mbili tofauti.

Alisema hilo lilisababisha utaratibu wa kukusanya mali na kuzibadilisha kuwa fedha uchukue muda mrefu.

Alisisitiza utaratibu huo ukikamilika wateja wote wa benki hiyo watalipwa fedha zao.

Alisema BoT haingizi nchini benki za hovyo bali huhakikisha inazifanyia uchunguzi wa kina wa kuhusu utendaji wake.

Advertisement