Mafuriko balaa, Mwenge wa Uhuru wasimama kwa dharura

Askari wa Jeshi la Polisi wakiwa wanaongoza gari la mbio za Mwenge wa Uhuru katika mkondo wa maji eneo la Manjecha Kijiji cha Michenga Ifakara,  baada ya maji kujaa barabarani kufuata mkondo wa maji mto Lumemo kuzidiwa baada ya mwenge huo kumaliza mbio zake Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba jana April 23.2924 mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda

Muktasari:

Wakati Mwenge wa Uhuru 2024 ukizindua zaidi ya miradi sita yenye thamani ya sh2.361bilioni, wananchi wa halmashauri ya Mlimba, wamewaomba viongozi wao kueleza shida na changamoto ya barabara ili viongozi  wachukue hatua za kupata utatuzi wa haraka.

Mlimba. Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchini na kuendelea kuharibu miundombinu ya barabara, msafara wa magari ya mbio za Mwenge wa Uhuru umelazima kusimama kwa muda eneo la Manjecha Kijiji cha Michenga wilayani Ifakara mkoani Morogoro, baada ya Mto Lumemo kujaa na maji kusambaa barabarani.

Msafara huo ulisimama wakati ukitokea Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba leo Jumatano Aprili 24, 2024 asubuhi na kukaa kwa takribani dakika 20 ukisubiri maji hayo yapungue kisha uendelee na safari.

Mwenge huo ulikuwa unatokea Kijiji cha Igima, maofisa wa Jeshi la Polisi na wengine wa Serikali na wa chama walilazimika kushuka kwenye magari hayo na kutafuta namna ya kuvuka eneo hilo.

Eneo hilo ambalo pia lina mkondo wa maji, lilifurika maji kiasi cha kuwafanya wakimbiza Mwenge huo wakalazimika kuushusha mwenge huo na kuvuka nao kwa miguu kupitia eneo lililokuwa na maji machache mpaka upande wa pili wa Manjicha baada ya kumaliza mbio zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba na kukabidhiwa kwa Halmashauri ya Ulanga.

Makabidhiano hayo yalifanyika katika Kijiji cha Minepa, wilayani Ulanga.

Kutokana na uharibifu wa barabara, magari mengi yaliyokuwa kwenye msafara huo yalikwama eneo korofi la Igima Sheli na yakakwamuliwa kwa kuvutwa na trekta.

Mwandishi aliyekuwa katika msafara huo ameshuhudia basi la Kilamsa lililokuwa limewabeba vijana wa hamasa likinasa katika  tope eneo la Idete baada ya kuacha njia na kunasuliwa na vijana hao.

Wakizungumza na Mwananchi Digital wakiwa Kijiji cha Igima wilayani Mlimba ambako Mwenge huo ulilala jana, walisema mara nyingi Mwenge ukipita katika maeneo hayo kila mwaka barabara nyingi zile za kiwango cha vumbi na changarawe huwa zinakarabatiwa, lakini mwaka huu imeshindikana kwa sababu ya mvua nyingi.

Mkazi wa Mchombe, Tukuzeni Lusingo amesema ana imani viongozi wameona adha wanayokumbana nao wananchi mvua zinyeshapo.

“Labda sasa watatufikiria na sisi huku tujengewe barabara za lami, ubovu huu wa barabara unachangiwa pia na kiwango chake cha vumbi,” amesema Lusingo.

“Kwa mfano, hapa tuliambiwa Mwenge ungelala Mngeta, lakini haujaweza kufika kule kwa sababu ya barabara, hakuendeki,” amesema.

Mkazi mwingine wa Igima, Lukagulagi Kidehele amesema alitamani kusikia viongozi wakipaza sauti zao kumuomba kiongozi wa mbio hizo za Mwenge awafikishie serikalini juu ya ubovu wa barabara hizo.

“Lakini ndiyo hawakufika Mngeta sasa, sisi wananchi wa Mlimba tunateseka sana, tunataka kilio hiki kimfikie Rais (Samia Suluhu Hassan),” amesema.

Kidehele amesema halmashauri hiyo imekuwa ikizalisha mazao ya biashara ikiwemo mpunga, kokoa, ndizi, ufuta na mengine ambayo ni uchumi mkubwa kwa wananchi.

Akitoa taarifa wakati wa makabidhiano ya Mwenge huo Wilayani Ulanga katika Kijiji cha Minepa, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dustan Kyobya, amesema wananchi wanampongeza kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava kwa kuvumilia na kukabiliana na changamoto ya mafuriko.

“Wilaya ya Kilombero na Ulanga tupo katika bonde la ardhi oevu la Kilombero, lakini tumshukuru kiongozi wa mbio za mwenge kwa kuwa na ujasiri licha ya kukwama njiani,”amesema Kyobya.

Hata hivyo amesema Serikali imetenga Sh97 bilioni kwa ajili ya kutengeneza kilometa 37 za barabara kutoka Lumemo Ifakara hadi Igima kwa kiwango cha lami.

Naye Mnzava amesema ubora na viwango vya miradi iliyokaguliwa ni vya kuridhisha.