Mafuriko Jangwani kuwa historia, ujenzi wa daraja washika kasi
Muktasari:
- Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema mipango ya Serikali kuboresha miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam ina lengo la kuhakikisha barabara zote zinapitika mwaka mzima ili kurahisisha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa Taifa.
Ulega amesema hayo leo Jumapili, Aprili 26, 2026 wakati akitoa maelezo hayo mbele ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliyekuwa na ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara jijini Dar es Salaam.
Ulega ametoa mfano wa ujenzi wa Daraja la Jangwani alilosema kukamilika kwake kutaondoa adha ya kukatika kwa njia ya kutoka Magomeni kuelekea katikati ya jiji na kurejea kwa kusema jambo hilo sasa litakuwa historia.
“Nakwambia tu mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Jangwani litakalokuwa na urefu sawa na viwanja vinne vya mpira itamaanisha mambo ya njia kufungwa kwa sababu ya mafuriko yatakuwa historia,” amesema Ulega.
Waziri Ulega amemueleza Waziri Mkuu Daraja la Jangwani lina urefu wa mita 390, upana wa mita 42.8 na kimo cha mita 15 na litakuwa suluhisho la kudumu kwa tatizo la mafuriko katika eneo hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likikumbwa na changamoto hiyo wakati wa mvua.
Kwenye ziara hiyo ya ukaguzi, Ulega amesema maboresho makubwa yanayoendelea jijini Dar es Salaam yanatokana na azma ya Rais Samia Suluhu Hassan kuona kwamba miundombinu inakuwa fursa kwa Watanzania badala ya kusababisha kero na ukosefu wa utu kwa wakazi wa jiji hilo.
Pamoja na mambo mengine, Dk Mwigulu amekagua miradi ya ujenzi wa madaraja ya Mkwajuni na Kigogo, ambapo alionesha kuridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa na kwamba hatua zinazochukuliwa zinaonesha mabadiliko makubwa ya maendeleo ya jiji hilo.
Waziri huyo ametoa pia taarifa kuhusu ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi aliosema umeleta mapinduzi makubwa kwa wananchi, akibainisha kuwa kwa sasa huduma hiyo inapatikana kuanzia Mbagala hadi Kariakoo ikiwa na mabasi yenye viwango vya kisasa, hali inayorahisisha usafiri na kupunguza adha iliyokuwepo hapo awali.
Ulega ameongeza Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara, ambapo katika siku chache zijazo baadhi ya maeneo yataanza kuhudumiwa na mabasi ya mwendokasi, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri jijini humo.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kwenye ziara ya kukagua ujenzi wa madaraja ya Mkwajuni na Kigogo, jijini Dar es Salaam
Amesema juhudi hizo zinafanyika chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini.
Aidha, ameeleza Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mingine ya kudhibiti mafuriko, ikiwamo mradi wa mifereji katika eneo la Boko Basihaya wenye thamani ya shilingi bilioni 57, ambao kwa sasa uko katika hatua ya manunuzi ya kumpata mkandarasi.
Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa madaraja ya Mzinga, Mpiji Chini na Ununio, ambayo kwa pamoja inagharimu shilingi bilioni 46.5, ikilenga kupunguza na kuondoa kabisa athari za mafuriko katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Kuhusu miradi ya madaraja ya Kigogo na Mkwajuni iliyokaguliwa, Ulega amesema inagharimu jumla ya Sh28 bilioni 28 na inalenga kuboresha mtandao wa usafiri, kuondosha changamoto ya mafuriko pamoja na kuimarisha usalama kwa watumiaji wa barabara.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.
Naye Dk Mwigulu amesema Rais Samia ni kiongozi mbunifu, wa vitendo na mwenye dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania kwa kutoa majawabu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao ikiwamo uboreshwaji wa miundombinu.
Amesema ujenzi wa madaraja hayo ni ubunifu wa Rais Samia wa kumaliza mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuwaelekeza wataalam kuandika andiko la kutafuta namna ya kutatua tatizo la mafuriko kwa dhararu ndipo zinapatikana fedha ambazo zimewezesha ujenzi wa jumla ya madaraja 81 nchi nzima ikiwamo barabara ya kwenda Lindi na Mtwara ambayo kipindi cha mvua hugeuka kisiwa.