Mafuriko yaua Kyela

Mbunge wa Kyela ambaye ni Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akizungumza na baadhi ya Wananchi  waliothirika na maji ya mafuriko katika kijiji cha Itope Wilayani Kyela. Picha na Brandy Nelson

Muktasari:

 Ni kutokana na mvua kubwa zilizonyesha tangu Aprili 14, mwaka huu. Zaidi ya watu 250 hawana mahali pa kukaa.

Kyela. Watu watatu wamefariki dunia na wengine watatu hawajulikani walipo baada ya kukumbwa na mafuriko yaliyotokea katika maeneo mbalimbali wilayani Kyela mkoani Mbeya.

Mafuriko hayo pia yamesababisha shule 27 kufungwa zikiwamo 20 za msingi na saba za sekondari kutokana na kuzingirwa na maji.

Mafuriko hayo pia yamezoa daraja la kamba linaloelea (kiteputepu) katika Mto Kiwira, linalounganisha kata za Ndandalo na Ibungu na kusababisha wananchi kukosa mahitaji mbalimbali, hivyo kulazimika kuomba boti.

Athari nyingine zilizotokana na mafuriko hayo ni kukatika kwa mawasiliano katika barabara inayounganisha Kikusya - Kyela – Ipinda hadi Matema na kufungwa kwa barabara ya kwenda Bandari ya Itungi katika Ziwa Nyasa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Mbunge wa Kyela ambaye pia Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliyetembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo, wananchi walisema zimeleta madhara makubwa.

Mtendaji wa Kijiji cha Itope, Lutufyo Mwangamile alisema tangu mvua hizo zilipoanza Aprili 14, mwaka huu nyumba nyingi zimeanguka na nyingine kujaa maji.

“Katika kijiji changu, kaya 850 zimeathiriwa na mafuriko haya na wananchi 250 wamekosa mahali pa kulala na wameomba hifadhi katika vijiji jirani,” alisema Mwangamile.

“Kuna watu wasioona wanane ambao hawana uwezo, wanahitaji kusaidiwa maana nyumba zao zimezingirwa na maji, hawana chakula na hakuna ndugu wa kuwasaidia,” alisema.

Akizungumza baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika, Dk Mwakyembe alisema athari ni kubwa kwani mvua zilizonyesha ni za kihistoria ambazo zimeathiri kata kumi na moja kati ya 20 za wilaya hiyo.

Kuhusu shule zilizofungwa, Dk Mwakyembe alisema Serikali inaendelea na mchakato wa kuzisaidia ili wanafunzi waendelee na masomo.

“Mvua ya safari hii ni ya kihistoria, haijawahi kutokea na hata madaraja ambayo yalikuwa yakiaminika kwa ajili ya mawasiliano yamesombwa na maji,” alisema.

Dk Mwakyembe aliahidi kutoa msaada wa chakula na vyandarua na kuwataka watendaji wa halmashauri ya wilaya kufanya tathmini mapema ili kuhakikisha chakula kinawafikia waathirika mapema.