Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mafuta yaibua mapya kila kona



Dar/mikoani. Wakati kilio cha ongezeko la bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kikiendelea kusikika kila kona nchini, mambo mapya yameibuka, yakiwemo matukio ya baadhi ya daladala kugoma na nyingine kukatisha ruti.

Kufuatia matukio hayo, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu (Latra) imetishia kuyafutia leseni mabasi yatakayohusika katika migomo, huku wananchi wakiiomba Serikali kuondoa ushuru na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bidhaa za mafuta kama njia ya kupunguza makali ya maisha.

Wananchi hao wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuiga hatua zinazochukuliwa na baadhi ya nchi za Afrika, ikiwemo Zambia, Namibia na Afrika Kusini, ambazo zimepunguza kodi na ushuru ili kupunguza mzigo kwa wananchi.

Maumivu ya ongezeko hilo la mafuta linalofikia wastani wa Sh950 kuanzia Aprili mosi, 2026, kumezifanya daladala jijini Mbeya kugoma, madereva wakishinikiza kupandishwa nauli, hatua ambayo imekumbana na onyo la Latra.

Licha ya onyo hilo, maeneo mengine nchini yameshuhudia daladala, bajaji na bodaboda zikipandisha nauli holela na kusababisha kilio kutoka kwa wananchi katika maneo.

Tayari Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo ametangaza kuitisha kikao cha wadau wa usafirishaji Aprili 8, 2026 jijini Dar es Salaam, ambacho kitajadili suala hilo na kutoka na uamuzi.

Aprili mosi, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza ongeko hilo la bei za mafuta linaloelezwa kuchochewa na mgogoro wa kimataifa unaoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ulioanza Februari 28, 2026.

Mgogoro huo umeathiri uzalishaji na usafirishaji wa mafuta ghafi duniani, hasa baada ya kufungwa kwa Mlango wa Hormuz, ambao hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani.

Vilevile, kushambuliwa kwa visima vya mafuta, maghala ya kuhifadhi mafuta na viwanda vya kuyasafisha kumeigusa moja kwa moja Tanzania ambayo inaagiza mafuta kwa kiasi kikubwa, jambo linalotajwa kuongeza gharama za usafirishaji kutokana na kukosekana kwa meli za kuyasafirisha.

Hali hiyo imesababisha ongezeko kubwa ambalo halijashuhudiwa kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, na kuilazimisha Serikali kukuna kichwa kutafuta namna ya kupunguza athari hizo, kama alivyoeleza Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.

Dk Mwigulu amebainisha mambo mambo mawili wakati akijibu Maswali ya papo kwa hapo bungeni leo Alhamisi Aprili 2, 2026, kwamba sasa Serikali itajielekeza katika kuongeza nguvu kwenye shughuli za uchimbaji madini na kubana matumizi.

Waziri Mkuu ametoa majibu hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT-Wazalendo), Ado Shaibu ambaye amehoji Serikali inachukua hatua gani kukabiliana na athari zitokanazo na kuendelea kwa vita vya Mashariki ya Kati.

Shaibu amesema matokeo ya vita hivyo yatasababisha mtikisiko katika usafiri, shughuli za madini na kwenye masuala ya bima, hivyo akaomba kutambua mkakati wa Serikali katika eneo hilo.

Waziri Mkuu amesema, Tanzania siyo kisiwa kwani inafanya biashara kama ilivyo kwa mataifa mengine, hivyo nayo ni miongoni mwa mataifa yatakayokumbwa na mtikisiko huo.

"Tanzania inafanya biashara na inategemeana na mataifa mengine, hivyo tumeshafanya tathmini ya kutosha kujua athari hizo pamoja na ongezeko la bei kwa baadhi ya bidhaa, lakini tutaendelea kujulishana wakati huu ambao wabunge tutakuwa hapa," amesema Dk Mwigulu.

Waziri Mkuu amesema nguvu kubwa itawekwa kwenye uchimbaji madini kwa kuwa wanatambua sekta hiyo ni miongoni mwa maeneo ambayo yakisimamiwa vizuri inaweza kupunguza mtikisiko huo.

Dk Mwigulu amesema hata katika kipindi cha mwaka jana madini yalichochea kwa kiasi kikubwa mapato na hasa kupitia wachimbaji wadogo.

Amesema kila wilaya inaelezwa kuwa na madini lakini eneo lililofanyiwa utafiti ni asilimia 16 tu.

Waziri Mkuu amesema mkakati mwingine ni kubana matumizi na lazima Serikali ifanye hivyo ili kuachana na maeneo ambayo hayana ulazima.

Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Mussa Zungu amesema Kamati ya Nishati na Madini iingekutana leo Alhamisi Aprili 2, kufanya tathimini ya hali ya mafuta nchini kufuatia agizo alilolitoa Aprili mosi.

Spika Zungu jana aliagiza kamati hiyo kukutana na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi ili wapeleke majibu na kwenye tangazo la leo, amewataka na wabunge wengine wanaopenda kuungana na kamati hiyo kufanya tathimini waende.


Gharama za maisha

Katika maeneo mbalimbali nchini, wananchi wamekumbana na shubiri ya ongezeko la gharama za maisha linalotokana na vyombo vya usafiri hususan bodaboda na bajaji ambazo kwa sehemu kubwa ndiyo wasafirishaji wakubwa wa wananchi, kupandisha nauli.

Dereva mkazi wa Kange, mkoani Tanga, Ayubu Limo amemwomba Rais Samia kuingilia kati changamoto hiyo na kutafuta suluhisho la haraka, akisema kupanda kwa mafuta kunaathiri sekta nyingi za uchumi.

“Hata tukipandisha nauli, bado athari itaonekana kwenye biashara nyingine kwa sababu gharama za usafirishaji zitapanda,” amesema Ayubu Limo.

“Haya magari pia yanahitaji matengenezo, matairi ni ghali na mafuta yanapopanda mzigo unakuwa mkubwa zaidi, hali inayofanya wamiliki washindwe kuendesha biashara kwa ufanisi,” ameongeza.

Kwa upande wake Ednest Lukindo ambaye pia ni dereva, amesema jambo la msingi ni kushuka kwa bei ya mafuta kwa kuondoa ushuru na VAT, kwa kuwa hata nauli zikiongezwa hakutaondoa tatizo la msingi.

Mmoja wa wakazi wa Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro aliyeomba jina lihifadhiwe, amesema: “Mimi naona Serikali ya Tanzania iangalie mfano wa Zambia, Namibia na kwingineko ambapo wametangaza hali ya dharura katika upatikanaji wa mafuta na kuchukua hatua za kupunguza makali ya gharama za nishati.

Wameondoa VAT na kusitisha ushuru wa bidhaa kwa petroli na dizeli kwa miezi mitatu kuanzia jana, hii ni hatua nzuri ya kuwasaidia wananchi, nasi tunahitaji msaada kama huo.

Mkazi wa Dodoma, Wiliam Mussolin amesema kutoka katikati ya jiji hilo kwenda gereza la Isanga amelipa Sh5,000 badala Sh3,000 ya zamani na alipohoji ongezeko hilo la nauli ameambiwa ni kutokana na kupanda kwa bei ya petroli.

“Niligombana naye lakini nikakumbuka kuwa ni kweli mafuta yamepanda ikabidi niwe mpole, ila nauli zimepanda sana,” amesema Mussolin.

Naye dereva wa bodaboda, Yusuph Nondo amesema gharama za usafirishaji zimekuwa kubwa, ndiyo maana wameongeza nauli ili na wao wapate faida.

“Mahali pa Sh2,000 tunakwenda kwa Sh3,000 hadi Sh4,000 kwa sababu kama nanunua mafuta Sh3,900 kwa lita moja unadhani mimi nitapata faida shilingi ngapi? Tumeamua tujiongeze ili tuendelee kufanya kazi,” amesema Nondo.

Mkazi wa Mjimwema, Mkoa wa Kigoma Juma Selemani amesema ongezeko hilo limekuwa pigo kwa wananchi wa kipato cha chini kwani walikuwa wanalipa nauli kawaida, lakini imepanda gafla bila maandalizi jambo linalowaumiza watu, hasa wenye kipato cha chini.

“Kwa sasa hakuna nauli ya Sh500 kwenye bajaji, nauli ni Sh1,000 kila kituo jambo ambalo litatulazimu wakati mwingine kutembea kwa miguu maana hatutaweza kumudu gharama wakati wote, hii hali inaumiza wananchi sana,” amesema Selemani.

Mama lishe kutoka eneo la Kibirizi mkoani Kigoma, Asha Ramadhani amesema kupanda kwa nauli kumepunguza faida katika biashara yake na kwamba gharama za usafiri kwenda sokoni kufata bidhaa zimeongezeka na itamlazimu naye kupandisha bei ya chakula kwa wateja wake.

Mwendesha bajaji, Sharif Said amesema kwa sasa kutoka mjini hadi Ujiji nauli ni Sh2,000 badala ya Sh1000 za awali, hivyo wao kama wafanyabiashara wasipopandisha bei za bidhaa watakuwa wanapata hasara.

Eneo la kilimo linaelezwa nalo linaweza kuathirika kama ambavyo Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Pembejeo za Kilimo Mkoa wa Njombe, Abusalum Magoma anavyoeleza.

Ameishauri Serikali kuwa na matenki ya kuhifadhia mafuta angalau kwa miaka mitatu na kuendelea kama ilivyo katika Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili tatizo linapotokea lisilete madhara makubwa kwa wananchi kama sasa.

"Tukianza kwenye sekta ya kilimo sisi ndiyo waathirika wakubwa, kwa sababu tunaamini pembejeo hizi zitapanda bei kwa kuwa lazima zipite kwenye athari za bei ya mafuta," amesema Magoma.


Mgomo wasitishwa

Jijini Mbeya mgomo wa daladala uliotokea mapema jiji leo asubuhi umeisha jioni na huduma kurejea kufuatia kikao kilichofanyika kikihusisha serikali na wadau wa usafirishaji.

Kikao hicho kimeazimia huduma kurejea kama ilivyokuwa awali hadi pale mkutano rasmi wa kitaifa utakaotoa mwelekeo mpya kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amesema baada ya sintofahamu iliyojitokeza wamekutana na kujadiliana na wadau na kupata muafaka na sasa huduma inaendelea kawaida.

Mwenyekiti wa Daladala, Ulimboka Mwambuli amesema kikao hicho kimekuwa na mafanikio baada ya pande zote kukubaliana na kukiri mapungufu na sasa huduma zimerejea.


Kubana matumizi

Baadhi ya wabunge wameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza matumizi ili kukabiliana na nyakati ngumu za uchumi ambazo Taifa linaingia.

Kwa mujibu wa wabunge hao, eneo la kuanzia ni katika matumizi ya magari ya viongozi yakiwemo ya kwao, wakishauri Serikali iangalie suala hilo ili kuokoa fedha zitakazowapelekea maendeleo wananchi sambamba na kudhibiti wizi.

Wametoa ushauri huo leo Alhamisi Aprili 2, 2026 wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, iliyowasilishwa Aprili mosi na Dk Mwigulu Nchemba, aliyeliomba Bunge kuidhinisha Sh 12.5 trilioni.

Mbunge wa Buchosa (CCM), Erick Shigogo Shigongo amesema hatarajii kuona katika hali ngumu ya uchumi iliyopo, lakini watu wanaendesha mambo kama vile hakuna changamoto zozote, hilo si jambo sahihi.

Katika maelezo yake, Shigongo amesema: “Hata katika familia ya kawaida, unapoingia katika nyakati ngumu kuna mambo ya kupunguza.

“Ombi langu mimi, sitamani kuona tunaingia kwenye hali ngumu ya uchumi kama Taifa, natamani kuona tunaendesha maisha yetu kama Serikali katika kujibana kutokana na hali tulionayo,” amesema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Nyasa (CCM), John Nchimbi amesema eneo la matumizi ya magari ya Serikali linatumia fedha nyingi, akisema ni wakati muafaka liangaliwe upya.

“Iangaliwe aina ya magari yanayotumika na kazi anazozifanya mtumishi. Utakuta mtumishi yeye ni mkurugenzi, tena hapahapa Dodoma na kazi zake hazimlazimu kutoka nje ya mkoa lakini anatumia gari la Sh480 milioni,” amesema.

“Kwa nini anatumia gari la gharama hiyo wakati haendi mbali? Serikali inatumia magari aina ya V8 zaidi ya 400, wakati kuna wengine hawakupaswa kuyatumia hayo,” amesema.

Nchimbi ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, amesema hata hao wanaotumia V8 hivi sasa, kuna tatizo la mafuta, lakini madereva wa magari wanayawasha kuanzia asubuhi hadi jioni yakiwasubiri viongozi.

“Unajiuliza hawa wanajua kama haya mafuta yananunuliwa kwa dola? Lakini ni gharama ya Serikali, mtu anangurumisha gari kuanzia asubuhi hadi mchana akimsubiri bosi wake ili lisipate joto,” amesema.

Mbunge huyo, amesema kama wabunge wanataka kudhibiti matumizi ya Serikali lazima waanzie kwa viongozi, wakiwemo wabunge, hasa kwa magari wanayoyatumia na mafuta yanayotumika katika usafiri huo.

Amesisitiza ni wakati muafaka wa kuwekwa utaratibu wa udhibiti wa matumizi kuanzia mtu mmoja mmoja hadi Serikalini ili kubana matumzi yatakayowezesha kuokoa fedha zitakazorudi kwa wananchi kuwapeleka maendeleo.

Imeandikwa Bakari Kiango (Dar), Rachel Chibwete (Dodoma), Happiness Tesha (Kigoma), Mbonea Herman (Tanga), Yese Tunuka (Moshi), Sadam Sadick (Mbeya), Seif Jumanne (Njombe) na Habel Chidawali (Dodoma)