Magari 50 ya wanafunzi yazuiliwa kutoa huduma Morogoro

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama kampeni ya ukaguzi wa magari hayo ilianza Juni 10, 2025 kwa kutoa elimu kwa wamiliki na Julai 9, 2025 ukaguzi ukaanza kufanyika.
Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limeendelea na kampeni ya ukaguzi wa magari ya shule yanayotumika kusafirisha wanafunzi, ambapo jumla ya magari 50 yamefungiwa baada ya kubainika kuwa katika hali ya ubovu usioruhusu kuendelea na shughuli hizo za usafirishaji.
Kampeni hiyo inalenga kuboresha viwango vya usafiri na usafirishaji wa wanafunzi pamoja na kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na ubovu wa magari hayo.
Akizungumza na wanahabari leo Alhamisi Julai 10, 2025 Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Alex Mkama amesisitiza kuwa magari yaliyofungiwa hayataruhusiwa kuendelea kutoa huduma ya kusafirisha wanafunzi hadi yatakapofanyiwa matengenezo na kukaguliwa upya, ili kuthibitisha usalama wake.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linaendelea na ukaguzi wa magari ambayo yanatumika kubeba wanafunzi ukaguzi huo ulianza Juni 10 na bado unaendelea hadi kufikia Julai 9, 2025 jumla ya shule 90 zimefikiwa na magari 147 yamekaguliwa ambapo 97 miongoni mwa hayo yalikuwa katika hali nzuri na kuruhusiwa kuendelea na kazi ya kusafirisha wanafunzi, 50 yalikutwa yakiwa mabovu na yamefungiwa kufanya shughuli hizo hadi yatakapotengenezwa na kufanyiwa ukaguzi kwa mara nyingine,” amesema Kamanda Mkama.
Kamanda Mkama, ametoa wito kwa wamiliki na watumiaji wa vyombo vyote vya moto kuzifahamu na kuheshimu sheria za usalama wa barabarani, akisisitiza kuwa atua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao.
Mwananchi imezungumza na baadhi ya wazazi wanaotumia magari hayo kuwasafirishia watoto (wanafunzi), akiwamo Sophia Mwakasege, amesema hatua hiyo ni nzuri na Polisi wanapaswa kuendelea nayo.
“Siku za nyuma, magari mengi yaliyokuwa yanatubebea watoto wetu, hayakuwa mazima, mengi yalikuwa mabovu, lakini tangu Jeshi la Polisi lilivyotangaza ukaguzi tunaona hata wamiliki wananunua mabasi mapya,” amesema Mwakasege.
Naye Ayubu Msuya ameliambia Mwananchi kuwa ukaguzi wa magari hayo umesaidia pia kuwawahisha watoto shuleni kwa sababu hayaharibiki hovyo barabarani.
“Wamiliki walikuwa wanapuuza sana suala la kufanyia matengenezo magari haya, lakini kwa mtindo huu wa kuyakagua umewaamsha wamiliki,” amesema Msuya.