Magereza waanza kuboresha mitalaa urekebishaji

Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Mzee Ramadhani Nyamka akizindua kazi za uandaaji mitaala ya urekebishaji tabia kwa wafungwa mkoani Morogoro. Picha na Lilian Lucas.

Muktasari:

  • Linalenga kuongeza ufanisi na kusaidia  wafungwa wajirekebisha na kujitegemea wamalizapo vifungo.

Morogoro. Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP), Mzee Ramadhani Nyamka amesema Jeshi la Magereza nchini limeanza kutekeleza maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo uboreshaji wa mitaala yake ya urekebu wa wafungwa.

Kauli hiyo ameitoa leo Desemba 18, 2023 mjini Morogoro wakati wa uzinduzi wa kazi za uandaaji mitaala ya urekebishaji tabia kwa wafungwa kuanzia ngazi za astashahada na shahada.

Kamishna Nyamka amesema moja ya maelekezo yaliyotokewa na Rais Samia ni kulitaka jeshi hilo kuhakikisha programu za urekebu kwa wahalifu zinafanyika kwa kiwango stahiki na kinachokubalika.

Amesema kwa kuzingatia jambo hilo mafunzo sahihi kwa maofisa na askari katika tasnia ya urekebu yanatakiwa kupewa uzito wa kipekee na unaostahili.

"Kazi ya urekebishaji wahalifu ni kazi ya kitaalamu sana hivyo inahitaji miongozo na mitaala inayoakisi hali ya sasa na inayoendana na wakati wa sasa," amesema Nyamka.

Amesema katika ripoti ya mapendekezo ya Tume ya maboresho ya Haki Jinai moja ya eneo ambalo limetiliwa msisitizo ni kuboresha mitaala ya Jeshi la Magereza na hasa kwenye programu za urekebishaji wahalifu ili matokeo ya urekebishaji yaonekane kikamilifu.

"Mfungwa anapomaliza kifungo chake na kurudi uraiani ionekane kweli amerekebishwa na kuwe na mabadiliko mapya, " amesema Nyamka.

Hata hivyo amesema ili waweze kufikia mafanikio hayo ni budi wataalamu wa mitaala watimize jukumu lao kwa wakati na ufanisi wa hali ya juu.

Amesema pamoja na maboresho makubwa ya mitaala yanayofanyika ni jukumu la jamii kuwasaidia wafungwa wanaomaliza vifungo vyao na tayari wana ujuzi ili waweze kujitegemea kiuchumi na sio kuwanyanyapaa.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa ukuzaji mitaala, Utafiti na upembuzi yakinifu kwa Soko kutoka Baraza la Taifa na elimu ya ufundi na Mafunzo ya ufundi stadi, Dk Magreth Shawa amelipongeza jeshi la magereza kwa kufuata taratibu na miongozo.

Amesema  ni jembo jema kuhuisha mitaala ili iendane na kuzalisha watu wanaoweza kuajirika kwenye magereza na kufanya kazi ambazo ni za kurekebisha wafungwa ili wanaomaliza vifungo vyao waweze kujitegemea na kutokurudia makosa.

"Mitaala inakuwa na sehemu tatu, inarekebisha akili ya mtu, mikono ya mtu jinsi ya kutenda na mtizamo lazima abadilike na kama ilivyo sasa wengi wakitoka magereza watu wanawaogopa lakini tunataka wakitoka magereza ule mtaala uwe umewasaidia wasirudie tena makosa.

Naye mtaalamu wa Mafunzo wa magereza Dk Marius Rutta amesema matatajio ya Jeshi ni kushirikiana na wataalamu kutoka ustawi wa Jamii, Veta na Nakvet ili kuandaa mitaala iliyo bora inayoendana na wakati na kubadilisha fkra ya jamii na wafungwa wanaomaliza vifungo vyao.

Amesema Jeshi la Magereza litahakikisha linakuwa na wataalamu wabobezi kwenye sayansi ya urekebishaji na suala hilo litafanyika kwa kufuñgua milango na kupeleka wataalamu nje kujifunzia zaidi Ili kupata uzoefu Katika tasnia ya urekebishaji.