Mageuzi ya sekta ya kilimo nchini kupitia ujengaji uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
Muktasari:
- Kilimo ni moja ya sekta muhimu zaidi Afrika Mashariki, huku asilimia 80 ya wakazi wa ukanda huo wanaishi katika maeneo ya vijijini na maisha yao yanategemea shughuli hiyo kwa kiasi kikubwa na taarifa hiyo ni kulingana na Jumuiya ya Afrika Mashariki (2019).Ifahamike kuwa, sekta ya kilimo ndiyo inayoendesha sehemu kubwa ya uchumi wa Tanzania.
Kilimo ni moja ya sekta muhimu zaidi Afrika Mashariki, huku asilimia 80 ya wakazi wa ukanda huo wanaishi katika maeneo ya vijijini na maisha yao yanategemea shughuli hiyo kwa kiasi kikubwa na taarifa hiyo ni kulingana na Jumuiya ya Afrika Mashariki (2019).Ifahamike kuwa, sekta ya kilimo ndiyo inayoendesha sehemu kubwa ya uchumi wa Tanzania.
Kulingana na Benki Kuu ya Tanzania (2018), sekta ya kilimo inachangia kwa asilimia 30 ya Pato la Taifa na kwa ukubwa huo sekta ya kilimo ni mara tatu ya ukubwa wa sekta ya biashara kwa asilimia 11, madini kwa asilimia 4.8, na uzalishaji wa viwanda kwa asilimia 5.5.
Sekta hiyo inaajiri takriban asilimia 77.5 ya nguvu kazi ya nchi na inachangia zaidi ya asilimia 95 katika mahitaji ya kitaifa ya chakula ukirejelea Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo II-ASDP II wa mwaka 2017.
Kwa Afrika Mashariki yote, mabadiliko ya tabianchi na kutokutabirika kwa hali ya hewa huathiri kiasi kikubwa uzalishaji wa kilimo, mifumo ya chakula na usalama wa chakula.
Utafiti umegundua kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yana athari tofauti kwa maeneo tofauti ya kijiografia na mwenendo wa mazao, na idadi ya watu walio katika mazingira magumu wako katika uwezekano mkubwa wa kuathiriwa zaidi. Vilevile, kuongezeka kwa idadi ya watu mijini Afrika kunasababisha mahitaji ya chakula kuongezeka.
Hii inachagiza haja ya kuundwa kwa njia jumuishi, ambayo imekuwa ikifahamika kama ‘utumiaji na uongezaji masuluhisho na mbinu za kisasa za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabanchi kwa ujumla kwa ajili ya maendeleo endelevu na jumuishi ya kilimo cha kibiashara.’
Kwa kuwa kilimo kinategemea mvua kwa kiasi kikubwa na rahisi kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na kutokutabirika kwa hali ya hewa, athari hasi za mabadiliko ya tabianchi tayari zinaonekana katika mifumo ya kilimo kwa Afrika Mashariki kupitia vipindi vikali vya hali ya hewa, mabadiliko ya mipaka ya ikolojia ya kilimo, kupungua kwa ubora wa mazao na wingi, na ongezeko la magugu na wadudu.
Mradi wa Kilimo Himilivu kulingana na tabianchi kwa Siku za Usoni (CRAFT)
Mradi wa Kilimo Himilivu kulingana na tabianchi kwa Siku za Usoni (CRAFT) ulianzishwa mahususi kwa ajili ya kushughulikia changamoto hizi zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi zinazoathiri sekta ya kilimo kwa nchi za Kenya, Tanzania na Uganda.
Mradi huu wa miaka mitano, uliozinduliwa mwaka 2018, chini ya ufadhili wa Wizara ya Mambo ya nje ya Uholanzi, unatekelezwa na Shirika la Maendeleo la Uholanzi la SNV kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Wageningen na Utafiti, Programu ya Utafiti ya CGIAR juu ya Mabadiliko ya Tabianchi, Kilimo na Usalama wa Chakula, Agriterra, na Ushirikiano wa Rabo.
CRAFT inafanya kazi kupitia kwa sekta binafsi, na inasaidia wadau wa sekta ya umma katika kutengeneza mazingira wezeshi uliojikita katika ushahidi wa mashambani kwa utumiaji wa kiwango kikubwa wa Njia za Kilimo Stahamilivu na cha Kisasa (CSA), pamoja na matumizi bora, yenye tija ya nishati mbadala katika kilimo.
Shughuli za CRAFT zimehusishwa katika uwekezaji jumuishi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuimarisha mienendo ya kilimo biashara na ushirika katika minyororo saba ya thamani nchini Uganda, Kenya na Tanzania.
Kiongozi wa Sekta ya Kilimo kutoka shirika la SNV hapa nchini, Menno Keizer anasema kuwa, “Gharama ya kutofanya chochote inaweza kuwa juu zaidi mara 20 ikilinganishwa na ile ya kutowekeza katika hatua za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.”
Mkakati wa utekelezaji unategemea hatua za ziada katika ngazi tatu: (a) mifumo ya kilimo, (b) mifumo ya soko jumuishi, na (c) mazingira wezeshi. Na faida za utekelezaji wake ni kama ifuatavyo:-
Kuongeza kipato kwa wakulima wadogo na wajasiriamali wadogo na kati. Hii itafanikiwa kupitia kuongezeka kwa matumizi ya mbinu na teknolojia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi miongoni mwa wakulima wadogo, wajasiriamali wadogo na kati na vyama vya ushirika.
Pia unaongeza ufanisi wa kibiashara kwa wajasiriamali wadogo na kati wanaofanya kilimo biashara na ushirika kutokana na uwekezaji unaohusiana na udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi. Hili litafanikiwa kupitia kuongezeka kwa uwekezaji na ukuaji wa biashara katika minyororo ya thamani kwa muktadha wa hali ya hewa, na kuongezeka kwa ushirikishwaji wa maendeleo ya kilimo biashara ya wanawake na vijana.
Kuboresha mazingira yanayowezesha kufanyika kwa kilimo stahamilivu katika uwanda mpana. Pia hili nalo litaweza kufanikiwa kwa kuongezeka kwa ushirikiano na ubadilishanaji uzoefu kati ya wadau wa sekta ya umma na binafsi katika utekelezaji wa kilimo stahamilivu.
Mafanikio ya mradi wa CRAFT katika sekta ya kilimo nchini kwa kipindi cha miaka 3 iliyopita
i. Mradi ulisaidia wakulima wadogo 37,500 (asilimia 40 wakiwa ni wanawake) kupata maarifa na ujuzi katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na masuluhisho ya udhibiti kama matumizi ya mbegu zilizoboreshwa, udhibiti wa udongo na maji pamoja na utunzaji wa mashamba baada ya mavuno. Hii imesababisha mavuno na mapato kuimarika mara dufu.
ii. Kupitia Mfuko wa Ubunifu na Uwekezaji kwenye masuala ya tabianchi (CIIF), CRAFT imewekezaa zaidi ya Pauni 2.6 Milioni katika uwekezaji wa uondoaji hatari kwa wafanyabiashara 18 wa kilimo biashara na ushirika nchini; na hivyo kuchochea matumizi ya njia na teknolojia za kisasa za kilimo stahamilivu katika minyororo maalumu ya thamani ya chakula kama alizeti, viazi, maharagwe na mtama.
iii. Ili kuhakikisha kunakuwapo ujumuishaji wa kijinsia na vijana, makampuni yapatayo 6 ya kilimo biashara yanaongozwa au kumilikiwa na wanawake na vijana.
iv. Katika juhudi za kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa kutoka katika shughuli za kilimo biashara, mradi huo ulisaidia matumizi ya nishati mbadala na namna bora ambayo nishati hizo zinatakiwa kutumika katika kilimo biashara. Lengo hili lilifanikiwa kupitia uhamasishaji, upangaji wa maonyesho ya teknolojia na msaada wa maendeleo ya shughuli za kilimo biashara zilizothibitishwa na mradi.
v. Kupitia Tathmini ya Hatari ya Hali ya Hewa ya nchi kwenye minyororo ya thamani mahususi(CRA),hatari ya mabadiliko ya tabianchi na mikakati inayofaa ya kukabiliana nayo kwa wadau tofauti tofauti, rasilimali na michakato katika minyororo ya thamani iliyowezeshwa ya mradi, ilitambuliwa nchini. Matokeo ya uchambuzi yalitumika kuhuisha miongozo ya mazao na kuandaa masimulizi ya hali ya hewa na biashara.
vi. Kuhamasisha na kukuza uimara wa kaya kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi, kwa kuwezesha mashamba darasa yanayozingatia mbinu na teknolojia ya kilimo himilivu. Pamoja na, mafunzo ya usimamizi wa kifedha na utamaduni wa kuweka akiba kati ya wakulima wadogo na shughuli za kilimo biashara. Hii iliwawezesha wakulima kudhibiti majanga na mafadhaiko yanayosababishwa na sababu zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi.
vii. Kulifanyika zoezi la Tathmini ya Hatari ya Hali ya Hewa (CRA). Katika mradi wa CRAFT, mbinu ya tathmini ya hatari ya hali ya hewa (CRA) inachunguza ni hatari gani wadau tofauti, rasilimali, na michakato katika mnyororo wa thamani inakabiliana nazo, na kutambua mikakati inayofaa ambayo itasaidia kupunguza hatari hizi.
Wakati huo huo, elimu iliyopatikana kutoka katika tathmini ya CRA inatoa sababu ya kuwapo kwa uendelezwaji wa shughuli za kilimo biashara cha kisasa na himilivu katika mradi wa CRAFT.
Ili kuelewa kutokutabirika kwa hali ya hewa, mifano ya utabiri wa hali ya hewa ilitengenezwa kwa kila zao lililokuwa katika minyororo ya thamani nchini.
Makadirio ya mabadiliko ya hali ya hewa yalifanywa kwa matukio tofauti tofauti katika minyororo ya thamani iliyotambuliwa.
Kwa kila mnyororo wa thamani, mfano wa majira kama ya mvua, kiwango cha juu, kiwango cha chini, na joto la wastani vilichanganuliwa kugundua hatari ya hali ya hewa iliyopo na kupendekeza mikakati inayofaa ya kukabiliana kwa ajili ya wadau tofauti, rasilimali na michakato kwa minyororo ya thamani ya mazao yote ya viazi, mtama, maharagwe, na alizeti.
viii. Mfano kama ilivyo mifano mingine mingi ya makadirio ya hali ya hewa ililinganisha wastani wa joto la kipindi cha 1961 – 2005 dhidi ya mvua na mwenendo wa joto la baadaye la miaka ya 2050.
Warsha ya CRA yalithibitisha makadirio ya hali ya hewa yalionyesha kuongezeka kwa joto la Tanzania kwa nyuzijoto 2 za Celsius (ºC) katika kipindi cha miaka 30 ijayo.
Kwa mfano, katika maeneo yanayolima alizeti, mfano wa makadirio ya hali ya hewa katikati ya karne (yaani miaka ya 2050) ulionyesha kuwepo kwa ongezeko la joto kwa karibu nyuzijoto 2.8ºC na 2.5ºC katikati, kusini, na mashariki mwa nchi kwa vipindi vyote vifupi (Oktoba, Novemba, Desemba) na virefu (Machi, Aprili na Mei) vya misimu ya mvua. Mvua ya wastani ya msimu pia ilitabiriwa kuongezeka hadi asilimia 10, hususan katika msimu mrefu wa mvua.
Vivyo hivyo, idadi ya siku za mvua mfululizo kwa sehemu ya Kaskazini-Mashariki mwa Tanzania ilikadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5-10, ambayo ni siku moja. Licha ya ukweli kwamba, nchi nzima ilikadiriwa/kuonyesha uwepo wa upungufu wa vipindi virefu zaidi ya mvua.
Kwa upande mwingine, mvua katika maeneo ya kaskazini mashariki yanayolima viazi ilikadiriwa kuongezeka kwa asilimia 20-30 katika miaka ya 2030 na 2050; na kupungua kidogo (kwa asilimia 5-10) katika maeneo yanayolima viazi Kusini-Magharibi, hususan katika msimu mfupi wa mvua.
Menno Keizer anasema kuwa, “Ikiwa hakuna hatua zinazoweza kuchukuliwa, athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa mavuno ya mazao nchini Tanzania itaendelea kuwa mbaya sana.”
Analeza kuwa CRAFT imewapa jawabu la kutumainiwa la namna ya kukabiliana na hatari za mabadiliko ya tabianchi na ushiriki wa dhati wadau wa kilimo biashara, wakulima wadogo, Serikali, watunga sera na wadau wengine muhimu kama vyombo vya habari, kupitia chaguo sahihi la njia na mikakati inayokwenda sambamba dhidi ya hatari ya mabadiliko ya tabianchi ya sasa na ya baadaye na kujenga minyororo endelevu ya thamani ya chakula ambayo instahamili hatari ya mabadiliko ya tabianchi.
Matokeo ya CRA, kwa mradi ambao umesaidia wakulima wadogo na shughuli za kilimo biashara, umekuwa na umuhimu mkubwa na faida kwa upangaji mzuri wa shughuli za kilimo (kwa kutumia kalenda ya kisasa ya upandaji wa mazao), ikiwasaidia kupanga vizuri, kupunguza gharama na kuongeza mavuno na faida.
Kwa mfano, taarifa hii inawasaidia aidha waamue au waache kupanda, wakati gani watamwagilia au la, wakati gani wa kutumia mbolea na upi la na ikiwa wataanza kuvuna au la.
“Kuongezeka kwa mwenendo mzuri wa kilimo biashara na ushirika. Kupitia Mfuko wa Ubunifu na Uwekezaji kwenye masuala ya tabianchi (CIIF), CRAFT-imewafikia wafanyabiashara 18 wa kilimo na ushirika na kuwekeza zaidi ya TZS 6.7 bilioni na kupelekea makampuni ya kilimo na vyama vya ushirika viliwekeza zaidi ya TZS bilioni 8.92 katika minyororo maalum ya thamani ya chakula,” anaongeza Menno Keizer.
Uwekezaji wa pamoja kupitia mfuko wa CIIF, haujaboresha tu utendaji wa kilimo biashara pekee ambapo 33 aidha zinaongozwa au kumilikiwa na wanawake / vijana) lakini pia imeongeza uimara wa kukabiliana na majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa kuongezea, kupitia CIIF, makampuni hayo yameanzisha uhusiano wa kibiashara na wazalishaji kupitia kilimo cha mkataba shirikishi ambayo sio tu iliimarisha mnyororo wa ugavi wa kampuni lakini pia iliongeza mapato ya wakulima kwa kuuza mazao yao kwa bei nzuri. Baadhi ya kampuni za Kilimo zilizonufaika na mradi wa CRAFT;
Mradi huo mkubwa umekuwa na manufaa makubwa kwa jamii na kila aliyeshiriki. Kampuni tatu za kilimo biashara za Temnar, Nondo na EAFFC ndiyo miongoni mwa wanaufaika hao, ambazo kupitia hizo, mradi wa CRAFT ulifanikiwa kuwafikia wakulima wadogo katika maeneo mbalimbali.
Temnar yenyewe ni kampuni ya kilimo inayohusika na usindikaji, usambazaji, na uuzaji wa mafuta ya kula pamoja na alizeti, Nondo Investment Company ikiwa ni kampuni inayojishughulisha na mnyororo wa thamani wa zao la alizeti, na East African Fruit and Farm Company ambayo inajishughulisha na usindikaji, usambazaji, na uuzaji wa zao la viazi.
EAFCC
Mratibu wa mradi kutoka EAFFC, Hance Melchior anasema moja ya mafanikio ya CRAFT ni ujuzi walioupata wa kutumia njia za kidijitali kuendesha shughuli zao. “Tuna mfumo maalumu wa kusajiri wakulima na mazao yao, pia tunasajiri masoko yaani kuwapa wateja fursa ya kuagiza kutoka kwa wazalishaji ambao ndiyo wakulima,” aneleza Melchior.
Pia anaeleza kuwa wana mfumo wa kuhifadhi taarifa za wakulima kuanzia nini wamelima? Wamevuna nini? Wamevuna kwa kiasi gani? Wameuza wapi?
Mkulima kutoka Rungwe, Moshi, Evarist anasema kuwa, “tulikuwa tayari kukubali mabadliko na kutumia njia za kisasa na himilivu za kilimo kama vile kalenda ya mazao na taarifa za hali ya hewa zimetusaidia kwa kiasi kikubwa. Mimi kwa sasa ninavuna mpaka gunia 120 za viazi mwaka huu ikilinganishwa na gunia 70 mwaka jana kwa sababu ya kufata kalenda ya mazao inayoendana na utabiri wa hali hewa.”
Nondo
Mkurugenzi Mtendaji wa Nondo Investment Company, Herymathew Raymond anasema kuwa licha ya faida mbalimbali zilizopatikana kutokana na kushiriki katika mradi wa CRAFT, alikabiliana na changamoto kubwa ya mabadiliko ya kisera baada ya Serikali kutaka mazao yote kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani tofauti na hapo awali, jambo ambalo liliathiri kiasi kikubwa kampuni hiyo. “Sera ile ilikuja kutumaliza kwani hatukuweza kununua alizeti tena kutoka kwa wakulima, ilitulazimu tuzifuate mnadani.”
Raymond hata hivyo, anakiri kuwa kampuni yake imefanya kazi kubwa ya kutengeneza soko kwa wakulima wa alizeti kwani kampuni hiyo ina kiwanda kikubwa cha kukamua alizeti chenye uwezo wa kukamua alizeti tani 3o (ambayo ni sawa na magunia 500 ya alizeti kwa siku).
Temnar
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Temnar yenye makao makuu yake Mtwara, John Julius anasema kuwa ili kufikia idadi kubwa ya walengwa na kutimiza malengo ya CRAFT, kama kampuni iliingia katika ubia na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ambapo kupitia mtaalamu wake aliyeopo katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Naliendele (NARI) aliweza kutembelea vikundi vya wakulima vilivyo chini ya Temnar takriban 145 na kutoa mafunzo ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kulima kisasa na kwa tija. “Pia, mtaalamu huyu alikuwa anatoa mafunzo jinsi ya kutumia na kufasiri taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya kuanza msimu ya kilimo.”
Naye kwa upande wake, mkulima wa alizeti na mkazi wa kijiji cha Ngalole, kilichopo Masasi, Mtwara, Hamida Lucas anasema kuwa, “tulikuwa tunalima kwa mazoea kwa kuamini kupanda ni mwezi Desemba, lakini baada ya mafunzo ya mradi wa CRAFT mambo yamebadilika. Tumejifunza kuwa mvua inaponyesha kubwa tukate majani na kutandaza chini kwani hata inapokata majani yanahifadhi unyevu kwa ajili ya uoteshaji alizeti. Na tumeshauriwa aina ya mazao yanayotakiwa kulimwa katika kipindi ambacho hakuna mvua na mafunzo hayo yamesaidia kuongeza mavuno yetu.”
Matarajio ya baadaye
Kwa miaka ijayo, CRAFT inakusudia kubuni mifumo zaidi ya kuongeza matumizi ya njia na teknolojia za kisasa za kilimo himilivu kwa wakulima wadogo, wajasiriamali na vyama vya ushirika, na kuzalisha mazao zaidi na ramani maalum zinazoonyesha maeneo yanayofaa kwa minyororo lengwa ya thamani katika kipindi cha mabadiliko ya tabianchi katika miaka 30 ijayo.
Shukrani
Shukurani zetu zinakwenda kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haswa Wizara ya kilimo, Tamisemi kupitia halmashauri za mkoa na wilaya ambapo mradi wa CRAFT unafanya kazi na mashirika mengine ya umma na serikali.
Wasiliana nasi:
Kwa habari zaidi, tafadhali wasiliana na SVN / CRAFT Tanzania kupitia [email protected].