Magonjwa yasiyoambukiza yaikamua NHIF

Mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga

Muktasari:

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema fedha nyingi za mfuko huo zinatumika katika kushughulikia magonjwa sugu, huku dawa za saratani na huduma ya kusafishwa figo ‘dialysis’ nazo zikitumia fedha nyingi zaidi.

Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema umetumia Sh99.09 bilioni kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kulipia huduma zilizotolewa kwa wagonjwa wanaougua magonjwa yasiyoambukiza.

Imeelezwa kuwa fedha hizo sawa na asilimia 18 ya fedha zote ambazo zililipiwa katika kushughulikia magonjwa sugu huku dawa za saratani na huduma ya kusafishwa figo ‘dialysis’ zikitumia fedha nyingi zaidi.

Hayo yamesemwa leo Alhamis Agosti 11, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Bernard Konga alipokuwa akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu mfuko huo katika kikao kazi cha wahariri na waandishi wa vyombo vya habari nchini.

Amesema magonjwa yasiyoambukiza ni mzigo mkubwa kwa mfuko huo na kuziomba sekta zote kusaidia ili kupambana na magonjwa hayo.

“Dawa za saratani zinakula zaidi mfuko wa NHIF ukiangalia haya ni magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha, magonjwa mengine ni pamoja na huduma ya kusafishwa damu kwa wagonjwa wa figo (dialysis) tunatumia Sh35.4 bilioni kwa mwaka,” amesema.

Konga amesema ili kupambana na suala hilo Serikali inajitahidi kupambana na magonjwa hayo kwa kukinga ikiwemo kutoa elimu huku akisisitiza kuwa kunahitajika afua ili kusaidia mfuko huo.

Pamoja na hayo, Konga amesema mpaka sasa mfuko huo una zaidi ya wanachama 4.83 milioni sawa na asilimia 8 ya Watanzania wote huku asilimia 6 wakihudumiwa na bima ya CHF na bima zingine zikichukua asilimia 1.