Magonjwa yasiyoambukizwa kwa watoto, vijana janga jipya

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Profesa Paschal Ruggajo

Muktasari:

Magonjwa yasiyoambukiza, ajali na afya ya akili yameelezwa kuwa changamoto iliyosahaulika kwa kundi la watoto na vijana na hivyo kuiweka nchi kwenye hatari kubwa ya ongezeko la wagonjwa na ukosefu wa nguvu kazi.

Mwanza. Magonjwa yasiyoambukiza, ajali na afya ya akili yameelezwa kuwa changamoto iliyosahaulika kwa kundi la watoto na vijana na hivyo kuiweka nchi kwenye hatari kubwa ya ongezeko la wagonjwa na ukosefu wa nguvu kazi.

Hayo yameelezwa na Profesa Francis Furia wa Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili alipokuwa akiwasilisha mada katika mkutano wa nne wa sayansi uliofanyika mwisho wa wiki jijini Mwanza.

Katika wasilisho hilo lenye kichwa cha habari cha ‘Magonjwa yasiambukiza kwa watoto na vijana; asiachwe yoyote nyuma’ Profesa Furia amesisistiza kuangaliwa kwa kundi hilo ili kuepusha gharama za matibabu kwa serikali na familia kwa ujumla.

“Asilimia 50 ya wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza nchini, wamepata magonjwa haya wakiwa chini ya umri wa miaka 14.

“Watoto na vijana wangekua sehemu ya kinga na matibabu tangu awali kungeondoa idadi kubwa ya magonjwa yasiyoambukizwa kuongezeka kwa kasi,” amesema Furia.

Amesema watoto chini ya miaka mitano huanza kuugua wakiwa kwa umri mdogo, lakini sio rahisi kugundulika mapema.

Akitaja takwimu za kundi hilo, amesema Tanzania ina watoto 800 chini ya miaka mitano wanagundulika na magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa upande wake Profesa Rose Lazier wa chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afya na Sayansi, amesema kongamano la kisayansi limekutanisha wadau mbalimbali wa mambo ya faya na kumekua na mijadala mingi yenye kuleta mwanga wa kupambana na magonjwa yasyoambukiza.

“Maboresho ni mengi katika kuhakikisha magonnjwa yasitoambukiza yanatoweka lakini changamoto kubwa ni namna ya wadau wote kufanya kazi pamoja na kuhakikisha kila mmoja anatoa mchango wakewa kitaalamu na kurahisisha huduama na uelewa wa magonjwa yasiyoambukiza,” amesema Laizer.

Awali akifunga kongamano hilo Profesa Paschal Rugajjo, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Tiba Wizara ya Afya amesema, Serikali imepokea mapendekezo nane ya kongamano hili na itayafanyia kazi ipasavyo.

Amesema magonjwa yasiyoambukiza yanagharimu Serikali na kuchukua maisha ya watu na kila kwenye vifo 10 vifo vinne hutokana na magonjwa yasiyoambukiza, ajali na maginjwa ya afya ya akili.

Naye Saldin Kimangale ambaye ni mwanasaikolojia amesema, kwa kuwa afya ya magonjwa ya akili imekua sehemu ya magonjwa yasyoambukiza ni muhimu Serikali ikafanya jitihada za makusudi kuweka wanasaikolojia kwenye shule zote.