Magufuli aalika wanunuzi wa nje kununua mazao

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule wa Kenya hapa nchini Dan Kazungu Ikulu jijini Dar es Salaam  Julai 30, 2018

Muktasari:

Amesema hakuna haja ya kwenda kununua chakula cha wakimbizi Ulaya wakati kinapatikana Tanzania.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametoa wito kwa mabalozi ambao nchi zao zina uhaba wa chakula kuja kununua nchini ili wakulima wapate masoko.

Amesema hakuna haja ya kwenda kununua chakula cha wakimbizi Ulaya wakati kinapatikana Tanzania.

Rais alisema Serikali inatafuta soko la chakula ili kutowavunja moyo wakulima ambao katika msimu huu wamezalisha ziada huku nchi ikiwa na chakula cha kutosha.

Alisema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi hati za utambulisho za viwanja kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yenye makazi yake nchini kwa ajili ya kujenga ofisi na makazi jijini Dodoma.

Jumla ya hati za utambuzi 67 zilikabidhiwa, kati ya hizo 62 ni za balozi za nchi na tano ni za mashirika ya kimataifa.

“Kama Somalia wanahitaji chakula waje wanunue hapa, kama South Sudan (Sudan Kusini) wanahitaji waje wanunue hapa, kama DRC wanahitaji waje kununua hapa,” alisema.

Rais alisema, “Kama kuna chakula kinatakiwa kupelekwa kwa refugees (wakimbizi), kwa nini mkanunue chakula kutoka nje huko Ulaya na kukisafirisha kwa gharama kubwa, si chukua hapa tu Songea.”

Rais Magufuli alisema alikutana na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), David Beasley ambaye alijionea ziada ya chakula iliyopo nchini.

Akizungumzia uamuzi wa kutoa viwanja kwa balozi na mashirika ya kimataifa alisema unalenga kurahisisha mchakato wa kuhamia makao makuu ya nchi jijini Dodoma.

Aliwaomba mabalozi kuchochea maendeleo nchini kwa kuleta wawekezaji kutoka kwenye nchi zao akiwahakikishia kwamba Dodoma ni sehemu nzuri ambayo ina miundombinu na huduma muhimu za kijamii.

Alisema viongozi wengi wa Serikali wamekwishahamia wakiwamo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri, makatibu wakuu na baadhi ya wakurugenzi. “Nami nimepanga kabla mwaka huu haujamalizika nitahamia Dodoma,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Serikali imeanza kuboresha mazingira ya Jiji la Dodoma ili liwe na hadhi ya makao makuu ya nchi kwa kujenga miundombinu ya barabara.

Rais Magufuli alisema takwimu zinaonyesha Jiji la Dodoma linaongoza kwa ukusanyaji wa mapato. Alisema Tanzania kuna halmashauri za manispaa 21, za miji 22, za wilaya 137 na majiji sita. Alisema kati ya majiji, Dodoma inaongoza kwa makusanyo ya mapato ya Sh24.2 bilioni ikiwa ni asilimia 123 ya makisio yao ya Sh19 bilioni.

Alisema Jiji la Dar es Salaam ambalo ni kongwe kuliko yote lilikusanya Sh15.3 bilioni, Arusha (Sh10.3 bilioni), Mwanza (Sh9.3 bilioni), Tanga (Sh9.1 bilioni) na Mbeya (Sh4.2 bilioni).

Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema wamejipanga kuwa makao makuu ya nchi na wameweka miundombinu muhimu kwa ajili ya watu wanaokwenda huko.