Magufuli aivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ilala kuwa Jiji

Magufuli aivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ilala kuwa Jiji

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumatano Februari 24, 2021 ameivunja Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumatano Februari 24, 2021 ameivunja Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji.

Taarifa iliyotolewa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo imesema Rais Magufuli ametumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 84 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Miji) Sura ya 288 kufanya mabadiliko hayo.

“Kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288, rais  Magufuli ameipandisha hadhi Halmashauri ya manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kuanzia leo,” imesema taarifa iliyosainiwa na Waziri Jafo.

Amesema taarifa nyingine zitakamilishwa ikiwa ni pamoja na kuhamisha shughuli za iliyokuwa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam ambayo imevunjwa leo kwenda Halmashauri mpya ya jiji hilo na kuwapangia vituo vipya vya kazi watumishi wa halmashauri iliyovunjwa.

“Aidha, mgawanyo wa mali na madeni ya iliyokuwa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam ambayo imevunjwa itafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) sura ya 288 na Sheria nyingine zinazohusika,” amesema Waziri Jafo.

Awali, Rais Magufuli alieleza kusudio la kuchukua hatua hiyo leo asubuhi alipokuwa akizindua barabara ya juu ya Kijazi Interchange.