Magufuli ataka miradi ya maji Tabora ikamilishwe

Muktasari:

  • Mradi huo wa maji utakaotoa huduma mkoani Tabora na vijiji vyake zaidi ya 60, umetokana na fedha za wahisani Sh900 bilioni.

Rais John Pombe Magufuli ameagiza makandarasi kutoka nchini India na ndani ya nchi wanaosimamia mradi wa maji wa Manispaa ya Tabora kuhakikisha wanakamilisha ujenzi kwa wakati na ubora.

Magufuli ameyasema hayo leo Jumanne Julai 24 wakati akizindua jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo wenye tanki la maji lenye ujazo wa lita zaidi ya milioni moja, utakaotumia maji ya Ziwa Victoria.

“Napenda kuwaasa makandarasi waliotoka India wasimamie vizuri mradi huu, licha ya kwamba ni wa miaka miwili unusu hamuwezi kusubiri muda wote huo ndipo mkamilishe, nawaagiza mnaweza kufanya kwa kipindi kifupi ili mradi mfanye kwa umakini na ubora unaotakiwa, Wanatabora wameisubiri huduma hii kwa muda mrefu,” amesema Magufuli.

Mradi huo wa maji utakaotoa huduma mkoani Tabora na vijiji vyake 69, umetokana na fedha za wahisani Sh900 bilioni kutoka nchini India.

“Naishukuru Serikali ya India kwa heshima kubwa wanayotoa katika kuiamini Tanzania, tunaamini huduma hii itaendelea kusogea Nzega, Igunga lakini baada ya fedha hizi kuja tukaamua mradi huu uje Tabora na si mahala pengine,” amesema.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Balozi wa India nchini Tanzania, Sandeep Arya amesema India inajitahidi kushirikiana na Tanzania ili kuboresha miundombinu na itakuwa ni mwendelezo wa urafiki na ushirikiano mwema baina ya nchi hizo mbili.

“Kupitia Rais Magufuli tunashirikiana katika miradi ya maji na umwagiliaji, tuna mipango mingine ya ushirikiano wa Tanzania katika sekta ya maji kwani imetokea kuwa nguzo ya ushirikiano na maelewano ya kisiasa, kiuchumi na kibiashara, kitamaduni, kielimu, kiafya nk,” amesema Balozi Sandeep.