Magufuli awakingia kifua wajasiriamali

Muktasari:

Rais John Magufuli amesisitiza wafanyabiashara wadodo wenye vitambulisho vya wajasiriamali waachwe wafanye biashara bila kudaiwa chochote

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka wafanyabiashara wadogo wenye vitambulisho vya ujasiriamali kutokubali kulipa tozo au ushuru wowote kwa watendaji wa Serikali.

Magufuli ameeleza hayo leo wakati akizungumza wananchi wa Migori mkoani Iringa kwenye ziara yake ya kikazi.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli imekuja baada ya mwanamke mmoja kuelezea changamoto ya ushuru unaotozwa na manispaa katika biashara yake ya samaki licha ya kuwa na kitambulisho hicho.

Kufuatia malalamiko hayo, Rais Magufuli akatoa maelekezo kwa wajasiriamali  wadogo wote kuwa wasikubali kutozwa fedha zozote kama wana vitambulisho hivyo vinavyowatambua rasmi.

“Najua hivi vitambulisho wakurugenzi na baadhi ya watendaji kwenye halmashauri hawavitaki, sasa nimesema isitokee mtu akakulazimisha kulipa chochote kama unacho kitambulisho.”

“Nimesema hakuna wa kukutisha mimi ndio Rais kwani kuna Rais mwingine hapa zaidi ya Magufuli?, sasa nasema vaa kitambulisho chako fanya biashara popote usilipe chochote,” amesisitiza.

Amesema anataka katika awamu yake ya uongozi wanyonge wafanye biashara halali na kutajirika.