Mahakama ya Rufani yabainisha kasoro kesi mikopo mibaya

Muktasari:

  • Mahakama imeibua hoja hiyo ilipokaa kusikiliza rufaa iliyokatwa na Equity Bank (T) Limited inayotoa huduma Tanzania na Equity Bank (K) ya Kenya, dhidi ya kampuni za Nas Hauliers Limited, Everest Freight Limited na Tanga Petroleum.

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imenusa kasoro katika hukumu ya kesi ya mikopo mibaya, baina ya kampuni tatu na benki mbili.

Kasoro hiyo inahusu tofauti ya idadi ya wadaawa inayotokea katika hukumu na waliotajwa kwenye taarifa ya kukata rufaa.

Mahakama imeibua hoja hiyo ilipokaa kusikiliza rufaa iliyokatwa na Equity Bank (T) Limited inayotoa huduma Tanzania na Equity Bank (K) ya Kenya, dhidi ya kampuni za Nas Hauliers Limited, Everest Freight Limited na Tanga Petroleum.

Katika rufaa, benki hizo zinapinga hukumu ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, iliyozipa kampuni hizo ushindi katika kesi ya madai ya mkopo wa Dola za Marekani 16.275 milioni, ambao benki hizo zinadai zilizikopesha kampuni hizo lakini zimekataa kuurejesha.

Rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa Jumanne, Aprili 30, 2024 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Rehema Mkuye (kiongozi wa jopo), Abraham Mwampashi na Zainabu Muruke.

Hata hivyo, kabla ya kuanza kusikiliza rufaa hiyo, Mahakama ilibaini kuwapo tofauti ya idadi ya wadaawa walioorodheshwa katika uso wa hukumu inayopingwa na walioorodheshwa katika hati ya taarifa ya kusudio la kukata rufaa na kwenye hati ya sababu za rufaa.

Hoja hiyo iliyoibuliwa kwanza na Jaji Muruke katika hukumu inayopingwa, jumla ya wadaawa ni watano, yaani wadai watatu (kampuni hizo) na wadaiwa wawili, benki hizo za Equity Tanzania na Equity Kenya.

Lakini katika hati ya taarifa ya kukata rufaa na hati ya sababu za rufaa, inaonyesha idadi ya wadaawa ni 13, yaani warufani wawili (benki hizo za Equity) na wajibu rufani 11, yaani kampuni hizo tatu pamoja watu wengine binafsi wanane (wakurugenzi wa kampuni hizo).

Wakurugenzi hao ni Ally Hemed Said, Ahmed Hemed Said, Bahman Salim Hemed, Idrissa Said Abraham, Issa Mohamed Said, Suleiman Nassoro Mohamed, Samiha Ally Hemed Said na Alexandria Estate Limited, ambao walitoa udhamini binafsi wa mkopo unaobishaniwa.

Hawa walitokana na shauri la madai kinzani lililofunguliwa na benki hizo. Katika shauri hilo, benki hizo zilikuwa wadai na kampuni hizo pamoja na wakurugenzi wake wakiwa wadaiwa.

Hata hivyo, kwenye hukumu inayopingwa wakurugenzi hawajatajwa upande wowote (wa wadai au wadaiwa), isipokuwa wametajwa tu ndani ya hukumu kuwa walikuwa wadaiwa katika shauri la madai kinzani.

Hivyo, majaji hao kwa nyakati tofauti walihoji iwapo hati hizo mbili (ya taarifa ya kukata rufaa na ya sababu za rufaa) ziko sawa mahakamani kwa kujumuisha watu ambao hawajatajwa katika uso wa hukumu inayopingwa.

“Hapa tuko kwenye mtanziko kama notisi ya rufaa na hati ya sababu za rufaa ziliwasilishwa mahakamani kwa sahihi. Hivyo, tunahitaji mzizungumzie hizi,” alisema Jaji Mkuye.

Mawakili wa pande zote, Mpaya Kamara na Timon Vitalis wanaowawakilisha warufani (benki za Equity) na Frank Mwalongo, anayewawakilisha wajibu rufaa (kampuni wakopaji na wakurugenzi wake), walikiri kuwepo tofauti.

Walidai kasoro hiyo inaweza kuonekana ndogo ambayo haina madhara, kwani haiathiri haki ya upande wowote.

“Hata hivyo, kama tukiangalia ukurasa wa 45 na 59 wa hukumu inasema wazi kwamba madai kinzani yalifunguliwa dhidi ya wadaiwa watatu (kampuni za Nas na wenzake) na wengine wanane zaidi (wakurugenzi wake hao)," alieleza Wakili Kamara.

Alidai hakuna kasoro kwenye hati ya notisi ya kukata rufaa na hati ya sababu za rufaa kuwataja wajibu rufani wote 11, wakiwemo wakurugenzi hao wa kampuni hizo, na kama ni kasoro iko kwenye hukumu ambayo haikuwataja wakurugenzi kwenye uso wake.

"Kwa maoni yetu, hili ni kosa dogo ambalo haliendi kwenye mzizi wa kesi,” alidai Wakili Kamara.

Aliiomba mahakama itumie kanuni ya kutokuzingatia kasoro ambazo haziendi kwenye mzizi wa kesi. Wakili Mwalongo alisema kuwa na wadaawa hao (wakurugenzi) haoni kama kuna shida.

“Kwangu sioni tatizo, inatosha tu kwamba hukumu imewataja ndani," alidai Wakili Mwalongo.

Alisisitiza hakuna upande unaolalamika kuathirika kwa kasoro hiyo, kwa kuwa haigusi mzizi wa kesi, hivyo naye anaiomba mahakama itumie kanuni hiyo kutozingatia kasoro isiyoenda kwenye mzizi wa shauri.

Mahakama ilipanga kutoa uamuzi wa hoja hiyo kwa tarehe ambayo wadaawa watajulishwa.

Mahakama katika hukumu iliyotolewa na Jaji Deo Nangela Aprili 19, 2023 pamoja na mambo mengine baada ya uchambuzi ilitupilia mbali madai kinzani ya benki hizo akieleza zimeshindwa kuthibitisha madai yake kwa kiwango kinachotakiwa.

Badala yake alizipa ushindi kampuni hizo akisema zimeweza kuthibitisha madai yake.

Aliamua kampuni zilishalipa mkopo huo na benki hizo na hazina madai yoyote kwa kampuni hizo na ikaamuru kampuni hizo zirejeshewe hati zake zote za mali zilizokuwa zinashikiliwa na EBT kama dhamana ya mkopo, uamuzi ambao benki hizo zimeukatia rufaa.

Chimbuko la mgogoro

Mgogoro baina ya pande hizo mbili ni mkopo wa zaidi ya Dola 16.27 milioni, sawa na zaidi ya Sh40 bilioni.

Kwa mujibu wa hukumu, kampuni hizo ziliingia makubaliano na Equity Bank (K) Limited (EBK) wa udhamini wa hati ya muamana (barua ya kibenki inayotolewa kwa mkopeshaji wa nje kumdhamini mkopaji kwa ahadi ya kulipa yenyewe mkopo huo kama mkopaji hatalipa (SBLC/LC).

Katika makubaliano hayo ya Mei 22, 2019, EBK ilitoa dhamana (LC) kwa kampuni hizo kupata mkopo kutoka kampuni ya nje ya nchi Lamar Commodity Trading DMCC ya Uarabuni, ambayo pia ilitoa idhini kwa Dubai/Numora Trading PTE Limited kutekeleza makubaliano hayo.

Kampuni hizo zilichukua mkopo kwa ajili ya kulipa madeni ya mikopo mingine ambayo zilikuwa zinadaiwa katika benki nchini ikiwemo Equity Bank (T) Limited (EBT), Amana Bank na UBL Bank Limited, na kuongezea mtaji wake.

Fedha hizo kutoka Numora iliyopewa jukumu hilo na Lamar zilitumwa kwa EBK ambayo pia ilizituma kwa EBT iliyoiteua kuwa wakala wa dhamana zake kutoka kampuni hizo.

EBT ililipa madeni yote ambayo kampuni hizo zilikuwa zinadaiwa na ikashikilia amana za kampuni hizo zilizokuwa kwenye benki hizo na pesa zilizosalia ikazipatia kampuni hizo.

Hata hivyo, baadaye kampuni hizo zilizifungulia kesi benki hizo (EBT na EBK) pamoja na mambo mengine zikiiomba mahakama iiamuru EBT izirejeshee hati za mali zake zisizohamishika na zinazohamishika ambazo iliziweka kama dhamana ya kudhaminiwa na EBK kwa LC kupata mkopo huo.

Kampuni hizo pamoja na mambo mengine, zilidai mkopo huo wa Dola 16.27 milioni kutoka Lamar/Numora haukuwa na udhamini wa EBK, zikidai LC iliyotolewa na EBK ilikuwa na kasoro na kwamba, mkopo huo haukuwa umesajiliwa nchini na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).