Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yaamuru kutaifishwa Sh185 milioni za raia wa China

Raia wa China, Xie Xiaomao(kushoto) akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kuhukumiwa kulipa faini Sh2 milioni au kwenda jela miaka mitano, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Mchina huyo ametiwa hatiani kwa kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetaifisha Sh185.787 milioni kuwa mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya raia wa China, Xie Xiaomao kukiri shtaka la kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na leseni inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mahakama pia imemhukumu Xiaomao (38) kulipa faini ya Sh2 milioni au kwenda jela miaka mitano, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa hilo. Amelipa faini hiyo.

Hukumu imetolewa leo Julai 11, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi baada ya mshtakiwa kukiri shtaka katika kesi hiyo ya jinai namba 45167 ya mwaka 2024.

Xiaomao maarufu Celina, ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Masaki, anadaiwa kujihusisha na biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na leseni kinyume cha Kanuni za 4(1) na (2) za Sheria ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2023 ambayo inasomwa kwa pamoja na kifungu cha 13(1), (2)(a) na cha (3) vya Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992.

Hakimu Mushi amesema mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa, hivyo inatoa adhabu na kutaifisha fedha hizo kuwa mali ya Serikali.

“Mshtakiwa ni mkosaji kwa mara ya kwanza, amekiri kosa na hajaisumbua mahakama, hivyo inamhukumu kulipa faini ya Sh2 milioni na akishindwa atatumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela,” amesema.

“Kuhusu kielelezo alichokamatwa nacho mshtakiwa ambazo ni Sh16,797,000 na Dola 64,255 za Marekani (Sh168,990,650) na fedha za China 500 zote zimetaifishwa na Mahakama na kuwa mali ya Serikali. Kama kuna upande wowote haujaridhika na adhabu iliyotolewa unaweza kukata rufaa,” amesema.

Kwa mujibu wa kiwango cha kubadlisha fedha kilichotajwa mahakamani Dola moja ni sawa na Sh2,630, hivyo Dola 64,255 ni sawa na Sh168,990,650.

Kabla ya adhabu kutolewa kwa mshtakiwa, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christine Joas, ameiomba mahakama itoa adhabu kwa kuzingatia kifungu cha 13(1), (2)(a) na kifungu cha (3) cha Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992.

“Upande wa mashtaka hatuna rekodi ya makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa,” amesema.

Wakili Joas amedai vifungu hivyo vinaelekeza mtu akitiwa hatiani anatakiwa kulipa faini mara tatu ya thamani iliyokamatwa.

“Pia tunaomba fedha zote alizokamatwa nazo mshtakiwa zitaifishwe na kuwa mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ameomba.

Mahakama ilipotoa nafasi kwa mshtakiwa kueleza ni kwa nini asipewe adhabu kali, Xiaomao kupitia wakili wake, Mrisho Mrisho ameomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza.

“Mteja wangu amekiri shtaka, hajaisumbua mahakama, hivyo naomba mahakama ione huruma kwa sababu huyo ni raia wa kigeni,” amedai Mrisho.

Hakimu Mushi baada ya kusikiliza hoja za pande zote amemhukumu mshtakiwa kulipa faini ya Sh2 milion au kutumikia kifungo cha miaka mitano jela na kutaifisha fedha zote alizokutwa nazo mshtakiwa.

Awali, akisoma hati ya mashtaka, wakili Joas amedai mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja la kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na kibali kutoka BoT.

Anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2024 na Mei 16, 2024 katika supamaketi ya Peninsula iliyopo Oysterbay wilayani Kinondoni.

Wakili Joas alimsomea maelezo ya awali akidai walipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna mtu anaendesha biashara hiyo bila kuwana leseni ya BoT, hivyo uliwekwa mtego.

Mei 15, 2024, mtoa taarifa huyo alienda eneo hilo na kuomba abadilishiwe fedha kutoka za Tanzania kwenda Dola ya Marekani.

“Mashtakwa alikubali kubadilisha fedha hizo za mtego ambazo zilikuwa Sh2.81 milioni,” amedai.

Inadaiwa akiwa katika hatua ya ubadilishaji fedha hizo, alikamatwa na upekuzi ulifanyika eneo hilo ambako zilikutwa fedha hizo.