Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yaamuru taasisi kulipa Sh363.6 milioni NSSF

Muktasari:

  • Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Mwanza, imeamuru Wadhamini Waliosajiliwa wa taasisi ya Progressive Islamic Education Foundation kulipa zaidi ya Sh363.6 milioni kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutokana na michango ya wafanyakazi ambayo haikuwasilishwa kwa wakati pamoja na adhabu zake.

Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Mwanza, imeamuru Wadhamini Waliosajiliwa wa taasisi ya Progressive Islamic Education Foundation, wanaosimamia Shule ya Awali na Msingi ya Bismack, kulipa zaidi ya Sh363.6 milioni kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutokana na madeni ya michango ya wafanyakazi na adhabu za ucheleweshaji.

Hukumu hiyo imetolewa Juni 12, 2026 na Jaji Emmanuel Ngigwana aliyekuwa akisikiliza kesi ya madai namba 10133/2026 iliyokuwa imefunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa NSSF na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) dhidi ya taasisi hiyo ya elimu.

Mahakama ilitoa hukumu hiyo baada ya kubaini kuwa mdaiwa hakuwasilisha maombi ya kutetea kesi wala kujibu madai ndani ya muda unaotakiwa na sheria.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, taasisi hiyo imeamriwa kulipa zaidi ya Sh187 milioni ambazo ni michango ya kisheria ya wafanyakazi ambayo haikuwasilishwa NSSF kwa kipindi cha Januari 2018 hadi Februari 2024.

Pia imeamriwa kulipa zaidi ya Sh176.6 milioni ikiwa ni adhabu na michango ya ziada iliyotokana na ucheleweshaji wa kuwasilisha michango hiyo katika vipindi mbalimbali.

Mbali na kiasi hicho, mahakama imeagiza kulipwa kwa riba ya asilimia saba kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu hadi fedha zote zitakapolipwa kikamilifu pamoja na gharama za kesi.

Katika shauri hilo, NSSF ilidai kuwa taasisi hiyo ilisajiliwa kama mwajiri anayechangia mfukoni humo, hivyo ilikuwa na wajibu wa kisheria wa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wake kwa wakati.

Walalamikaji waliieleza mahakama kuwa baada ya kufanya ukaguzi wa kawaida walibaini uwepo wa deni kubwa la michango ya wafanyakazi ambalo halikuwa limewasilishwa kwa mfuko huo kwa mujibu wa sheria.

Mahakama ilielezwa kuwa licha ya NSSF kufanya ufuatiliaji na kutuma barua za madai mara kadhaa, taasisi hiyo haikurekebisha dosari hizo wala kulipa kiasi kilichokuwa kinadaiwa.


Uamuzi wa Mahakama

Katika uchambuzi wake, mahakama ilibainisha kuwa kesi hiyo iliwasilishwa chini ya utaratibu wa muhtasari (summary procedure), ambao unaruhusu mahakama kutoa hukumu haraka pale madai yanapoonekana kuwa wazi na mshtakiwa hajawasilisha utetezi wenye hoja zinazostahili kusikilizwa.

Mahakama ilieleza kuwa mshtakiwa alipatiwa nyaraka za kesi Mei 13, 2026, lakini hakuchukua hatua yoyote ya kuomba ruhusa ya kutetea shauri hilo ndani ya siku 21 zilizowekwa na sheria.

Kutokana na hali hiyo, madai yaliyowasilishwa na NSSF yalichukuliwa kuwa yamekubaliwa kwa mujibu wa sheria.

Jaji amesema nyaraka zilizowasilishwa na walalamikaji, zikiwemo cheti cha usajili wa mwajiri, ripoti za ukaguzi, ratiba za michango isiyolipwa pamoja na barua za madai, zilitosha kuthibitisha uwepo wa deni hilo.

“Walalamikaji wamethibitisha kwamba mshtakiwa, akiwa mwajiri aliyesajiliwa na NSSF, alishindwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria wa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wake,” ilieleza sehemu ya hukumu hiyo.

Mahakama ilikubaliana na madai ya NSSF kuwa ucheleweshaji huo uliathiri utekelezaji wa majukumu ya mfuko huo ya kukusanya na kuhifadhi michango ya wafanyakazi kwa ajili ya mafao yao ya baadaye.

Kutokana na ushahidi uliowasilishwa na kutokuwapo kwa utetezi wowote kutoka upande wa mdaiwa, mahakama iliamua kutoa hukumu hiyo na kuamuru taasisi hiyo kulipa zaidi ya Sh363.6 milioni, mbali na riba na gharama za kesi kama ilivyoamuriwa na mahakama.