Mahakama yaelezwa jinsi Padri Soka alivyodaiwa kubaka mtoto

Muktasari:

Padri Soka anashitakiwa kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 12 aliyekuwa akishiriki mafundisho ya kipaimara kanisani.

Moshi. Mshtakiwa katika kesi ya ubakaji namba 45 ya mwaka 2022, Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Deonis Aropagita katika Jimbo la Moshi, Sostenes Bahati Soka, amesomewa maelezo ya awali.

Padri Soka amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi, Kilimanjaro leo Jumatatu Oktoba 10, 2022 na kusomewa maelezo ya awali akituhumiwa kumbaka mtoto wa miaka 12.

Akisomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Salome Mshasha, Wakili wa Serikali Kasimu Nasiri, amedai kuwa mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 12, 2022 ambapo wakati wa tukio hilo mtoto huyo alikua akishiriki mafundisho ya kipaimara kanisani hapo.

Amedai kuwa mtoto huyo baada ya kumaliza mafunzo hayo majira ya jioni, alikwenda kwa mshtakiwa kwa nia ya kuungama dhambi zake, alipofika alimkuta mshtakiwa amekaa kwenye kiti na kuanza kupiga magoti na kuungama dhambi zake.

Hata hivyo, mshtakiwa alipotaka kumpa kitubio chake, ndipo alimshika mabega na kumnyanyua kutoka kupiga magoti hadi kusimama kisha akampakata.

Alidai kuwa baada ya kumpakata ndipo alimtomasa sehemu mbalimbali za mwili kisha akampeleka ukutani, akaishusha sketi ya mtoto na kumwambia ashike sketi yake, mtoto akashika na padri huyo akazivua nguo zake za ndani na yeye kuvua kanzu yake na kutoa uume uliokua umesimama na kisha kumuingizia.

Wakili huyo aliendelea kudai kuwa wakati akiendelea na tukio hilo alikuwa akimtomasa tomasa mwilini hadi alipomaliza haja zake ndipo akamruhusu mtoto huyo kuvaa nguo zake na kuondoka.

Amedai kuwa mtoto huyo akiwa anazungumza na wazazi wake nyumbani mazungumzo kati ya mama na mwana, ndipo mtoto alimweleza kuwa Padri huyo amemfanyia vitendo vya kikubwa. Maelezo hayo ya mtoto yalimshtua mama yake ambaye alichukua hatua ya kwenda kutoa ripoti kituo cha polisi na kwamba, ripoti ya uchunguzi  ilionyesha mtoto huyo ameingiliwa. Mshitakiwa alipelekwa kwenye gwaride maalumu la utambuzi na akatambulika na hatimaye sheria kuanza kuchukua mkondo wake ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Kwa upande wake, mshitakiwa amekana kuwa sio kweli isipokua  alitambulika kwenye gwaride maalumu la utambuzi lililofanywa na polisi.

Hata hivyo, Wakili wa utetezi Edwin Silayo ameomba kuahirishwa kwa kesi hiyo kutokana na sababu kuwa leo Jumatatu Oktoba 10, 2022 ndio mara yake ya kwanza kukutana na mteja wake hivyo, kuna nyaraka na maelezo hajapewa.

Hakimu Salome ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 12, 2022 ambapo mashahidi wanne watafika kutoa ushahidi.