Mahakama yaikubali kesi kumpinga Spika kumhoji CAG

Muktasari:

Leo Jumatatu, Mahakama Kuu ya Tanzania imeisajili kesi iliyofunguliwa na kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kupinga Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuhojiwa na Bunge 

Dar es Salaam. Hatimaye Mahakama Kuu Tanzania imekubali kuisajili kesi ya kikatiba, kupinga Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kuhojiwa katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Mahakama hiyo imekubali kuisajili kesi hiyo iliyofunguliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai leo Jumatatu Januari 21, 2019, baada ya kumalizika kwa mvutano wa usajili wa kesi hiyo uliodumu kwa juma zima.

Zitto ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo anaiomba Mahakama Kuu itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo Kikatiba na pia kutoa tafsiri ya Sheria ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau Bunge.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, wakili wa Zitto, Fatma Karume amesema alipewa taarifa za kuikubali kesi hiyo na kumtaka alipie gharama za usajili.

“Tayari nimeshalipia kabisa na hivyo sasa tunasubiri tu kupatiwa namba ya usajili,” amesema Karume, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Hata hivyo, wakati kesi hiyo ikisajiliwa, leo Jumatatu CAG Profesa Assad, ameitikia wito huo wa Spika na amefika mbele ya kamati hiyo kuhojiwa kwa madai ya kulidhalilisha Bunge kutokana na kauli aliyoitoa hivi karibuni kuwa Bunge la Tanzania ni dhaifu.

Awali, kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani hapo Jumatatu ya Januari 14, 2019 na wabunge watano, kutoka vyama vitatu vya siasa vya upinzani, wakiongozwa na Zitto.

Wabunge wengine walikuwa ni Saed Kubenea (Ubungo- Chadema); Salome Makamba (Viti Maalum- Chadema); Hamidu Bobali (Mchinga- CUF) na Anthony Komu (Moshi Vijijini- Chadema).

Walifikia uamuzi huo kutokana na taarifa ya Spika Ndugai kupitia vyombo vya habari na baadaye kumwandikia barua CAG akimtaka afike mbele ya kamati hiyo ya Bunge kuhojiwa kutokana na kauli yake aliyoitoa akiwa nchini Marekani kuwa Bunge la Tanzania ni dhaifu. Hata hivyo, Mahakama Kuu ilikataa kuisajili huku ikibainisha kasoro mbili.

Mahakama Kuu katika barua yake ya Januari 16, 2019 kwenda kwa Wakili Karume iliyosainiwa na Naibu Msajili aliyejitambulisha kwa jina la S.S. Sarwatt, ilibainisha kasoro hizo kuwa ni pamoja na wadai wengine wanne kutokuambatanisha hati za viapo vyao katika kesi hiyo.

Sababu au kasoro nyingine ni kutokuwepo kwa nakala ya wito wa Spika kwa CAG na au kutokuwepo kwa kiapo cha CAG kuunga mkono kesi hiyo.

Hatua hiyo iliibua mvutano baina ya pande hizo mbili na kuwalazimu Zitto na Wakili Karume kuwasilisha malalamiko yao kwa Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma.

Jaji Mkuu Profesa Juma baada ya kusikiliza malalamiko aliwaeleza suala hilo liko katika mamlaka ya Jaji Kiongozi na kwamba hata huyo naibu msajili aliyekataa kusajili kesi hiyo naye yuko katika mamlaka ya Jaji Kiongozi.

Hata hivyo, Jaji Profesa Juma alimwandikia barua Jaji Kiongozi, Dk Eliezer Feleshi, akimwelekeza alishughulikie suala hilo, ambayo aliwakabidhi kina Zitto wampelekee.