Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yakataa kupokea video kesi ubunge wa Baba Levo

Muktasari:

  • Mbunge wa Kigoma Mjini,   Baba Levo anakabiliwa na kesi ya uchaguzi ambayo imeendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa walalamikaji wanaopinga ushindi wake.



Kigoma.   Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma imekataa kupokea kiungo (link) ya  picha Jongefu (Video) kuwa sehemu ya ushahidi katika kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando, maarufu Baba Levo (CCM).

Shahidi hiyo  ambaye ni mmoja wa walalamikaji ameiomba mahakama hiyo ikipokee kiungo hicho cha video hiyo leo Jumatano Julai 8, 2026 wakati kesi hiyo ilipoendelea kusikilizwa.

Baba Levo alitangazwa mbunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025,  akimshinda mpinzani wake mkubwa kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Zitto Kabwe.

Shahidi huyo Pendo na wenzake watatu, Johary Kabourou, Lumu  Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali wamefungua kesi wakipinga ushindi wake.

Kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya Mwaka 2025 mbali na Baba Levo ambaye ni mlalamikiwa wa pili katika kesi hiyo  walalamikiwa wengine ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Walalamikaji hao wanadai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za Sheria na Kanuni za Uchaguzi.

Wanabainisha kasoro hizo kuwa ni pamoja  na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na Sheria za Uchaguzi, vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.

Hivyo wanaiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.

Akiongozwa na wakili wa walalamikaji shahidi huyo ameieleza mahakama kuwa atatoa ushahidi wake kwa njia ya maandishi, ambayo tayari yalishawasilishwa mahakamani na akaiomba  Mahakama iupokee.

Pia ameieleza kuwa katika ushahidi wake kuna kiungo (link) cha picha jongefu ambayo ameiomba Mahakama iisikilize.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Mark Mulwambo na wakili wa Baba Levo, Thomas Msasa wamesema kuwa hawana pingamizi ushahidi wake huo wa maandishi kupokewa.

Hata hivyo  wamepinga ombi la Mahakama kusikiliza video hiyo wakidai kuwa si sehemu ya ushahidi wake na kwamba katika maelezo yake ya maandishi hakuomba video hiyo isikilizwe.

Hata hivyo wakili John Seka amepinga hoja hizo akidai kuwa kiungo hicho ni sehemu ya ushahidi wake wa maandishi kwa kuwa amekielezea katika ushahidi huo na mara tu maelezo yake yanapopokewa anakuwa huru kuomba chochote.

Wakili Seka amedai kuwa haoni tatizo la kisheria katika hilo na  hata mawakili wa walalamikiwa hawajataja kifungu chochote cha sheria ambacho kimekiukwa, hivyo akaiomba Mahakama hiyo ilitupilie mbali pingamizi hilo.

Jaji Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo baada ya kusikiliza hoja za pingamizi hilo kwa pande zote katika uamuzi wake amekubali kupokea ushahidi wa maandishi wa shahidi huyo kuwa sehemu ya ushahidi wake.

Hata hivyo amekubaliana na pingamizi kuhusu kusikilizwa kwa video ambayo kiungo chake amekibainisha katika maelezo yake.

Jaji Nongwa amesema kuwa kwa kuwa vielelezo hivyo vilishawasilishwa mahakamani wakati wa usikilizwaji wa awali, basi mahakama itaangalia kama kiungo cha video hiyo ni mojawapo ya vielelezo hivyo vilivyopokewa wakati wa usikilizwaji wa awali.

Amesema kuwa kama  kiungo cha video hiyo ni sehemu ya vielelezo hivyo vilivyopokewa mahakamani wakati wa usikilizwaji wa awali basi Mahakama itauchukulia ushahidi wake huo kwa kadri utakavyokuwa.

Baada ya uamuzi huo, shahidi huyo ameanza kuhojiwa maswali ya dososo na mawakili wa walalamikiwa, ambao wamemuhoji maswali mbalimbali kuhusiana na ushahidi wake huo wa maandishi.