Mahakama yamuamuru mzabuni arejeshe Sh8.5 bilioni za Tanesco

Muktasari:

  • Tanesco iliishtaki mahakamani kampuni ya Intertrade kwa kukiuka mkataba wa zabuni ya vifaa vya umeme na vitendea kazi licha ya kuilipa.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeiamuru kampuni ya Intertrade Commercial Services (P) Limited kurejesha fedha ilizolipwa na Shirika la Umeme (Tanesco) zaidi ya Sh8.5 bilioni katika zabuni vifaa vya umeme na vitendea kazi, lakini ikatokomea bila kuikabidhi vifaa hivyo.

  

Mahakama hiyo imetoa amri hiyo jana Jumanne, Februari 6, 2024 kufuatia kesi iliyofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tanesco dhidi ya kampuni hiyo inayojihusisha na uagizaji na usambazaji wa vifaa kusafirishia na kusambazia umeme kwa kukiuka mkataba wa zabuni hizo.

Katika hukumu hiyo kwenye kesi iliyosikilizwa upande mmoja bila mdaiwa, mahakama hiyo imeiamuru kampuni hiyo kurejesha pesa hizo na fidia ya Dola za Marekani 200,000 (zaidi ya Sh500 milioni) kwa kuvunja mkataba.

Pia mahakama imeiamuru kampuni hiyo kuilipa Tanesco riba ya asilimia 7 ya pesa hizo zote ilizoamuriwa kulipa, kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu hiyo mpaka tarehe ya kukamilisha malipo yote; pamoja na gharama za kesi.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, kulingana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Tanesco iliingia mikataba miwili tofauti na kampuni hiyo kwa nyakati tofauti, mwaka 2013 na 2015.

Mikataba hiyo yote kwa pamoja ilikuwa na thamani ya zaidi ya Sh41 bilioni na zaidi ya Sh1.47 bilioni.

Mkataba wa kwanza ulisainiwa Oktoba 25, 2013 kwa ajili ya kuisambazia Tanesco mita za umeme kwa wateja wakubwa na mita za kupimia umeme kwa wateja wote, wakubwa na wadogo katika eneo maalumu

Mkataba huo ulipaswa kutekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia 2015-2017.

Mkataba wa pili ulisainiwa Aprili 23, 2015 wa kuisambazia Tanesco vitendea kazi vya usambazaji umeme, wenye thamani ya Dola za Marekani 476,566.999 (zaidi ya Sh1.1 bilioni).

Utaratibu wa malipo kwa mikataba yote ulikuwa ni wa kidogo kidogo na pande zote zilikubaliana kwamba mdaiwa angelipwa asilimia 10 kama malipo ya awali, asilimia 40 wakati wa kupakia vifaa melini na asilimia 50 baada ya Tanesco kupokea vifaa husika.

Mkataba wa kwanza ulitekelezwa vema katika miaka miwili ya kwanza lakini katika mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa mkataba huo yaani 2016/2017 kampuni hiyo haikuipelekea Tanesco vifaa hivyo licha ya shirika hilo kutimiza wajibu wake, yaani kulipa malipo ya awali na ya kati.

Vilevile katika mkataba wa pili tayari Tanesco ilikuwa imeshalipa malipo ya awali ya asilimia 10 na malipo ya asilimia 45 kwa ajili ya usafirishaji vifaa hivyo, lakini pia haikupokea vifaa hivyo.

Hivyo, Tanesco ilifungua kesi ikiiomba mahakama hiyo iiamuru kampuni hiyo jumla ya Dola za Marekani 6,945,750.91 (zaidi ya Sh17.3 bilioni na Sh810, 928, 503, ilizodai kuwa ni jumla ya pesa ilizokuwa imeilipa kampuni, ambazo ni asilimia 55, kwa vifaa ambavyo haikuvipokea katika mikataba yote miwili.

Pia Tanesco ilioomba kampuni hiyo iirejeshee Sh3.78 bilioni ilizodai kuwa ilikuwa imezilipa kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) kama Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa niaba ya kampuni hiyo.

Vilevile TRA iliomba ilipwe fidia ya madhara ya jumla kwa usumbufu na hasara iliyoipata kutokana na kampuni hiyo kukiuka mkataba kiasi cha Sh1 bilioni, riba kuanzia Agosti mosi 2017 mpaka tarehe ya hukumu na gharama za kesi.

Kampuni hiyo katika hati yake ya majibu ilikana madai hayo ya Tanesco, huku nayo ikiwasilisha madai kinzani dhidi ya Tanesco ikidai kuwa shirika hilo lilikiuka makubaliano ya mkataba kwa kuchelewa au kushindwa kufanya malipo.

Hivyo nayo iliiomba mahakama iiamuru Tanesco iilipe jumla ya Dola za Marekani 97,658,563.26 (zaidi ya Sh244.1 bilion).

Kati ya hizo, Dola za Marekani 1.125 milioni ilizodai kuwa ni mkopo iliouchukua kuwezesha utekelezaji wa mkataba, Dola za Marekani 1.8 milioni, malipo iliyoyatoa kwa mtengenezaji wa vifaa husika; Dola 19,733,563.26 kama hasara halisi na Dola 75 milioni kurejesha hasara iliyoipata.

Pia iliiomba mahakama iiamuru Tanesco iilipe zaidi ya Sh3.8 bilioni kama malipo yaliyozuiliwa, riba na gharama za kesi.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Tanesco iliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Consesa Kahendaguza, Steven Urasa na Angelina Ruhumbika, lakini mdaiwa kampuni hiyo haikutokea mahakamani na juhudi za kumpatia hati ya wito moja kwa moja na kwa njia mbadala hazikuzaa matunda.

Hivyo mahakama iliendelea na usikilizwaji wa upande mmoja chini ya Amri ya IX Kanuni ya 8 na madai ya kampuni hiyo yaliondolewa chini ya Amri ya IX Kanuni ya 5 za Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai, Sura 33.

Katika kuthibitisha madai yake Tanesco iliwaita mashahidi watatu akiwemo f0undi mkuu wa Tanesco anayefanya kazi katika karakana ya mita na mhasibu wake.

Tanesco katika ushahidi wake mbali na kuwasilisha mahakamani vielelezo kuthibitisha malipo, pia ilidai kuwa kutokana na mdaiwa kushindwa kutekeleza mkataba wake ilipata hasara kwa kushindwa kuwaunganisha na huduma wateja wake 250,000 na kupoteza imani kwa umma na kuingia bajeti nyingine.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake imekubaliana na madai mengine ya Tanesco lakini ikakataa malipo ya Sh3.78 ya VAT kwa TRA, ambayo Tanesco ilidai kuwa iliyalipa kwa niaba ya kampuni hiyo; ikisema kuwa hayajaungwa mkono na ushahidi wowote.

Kuhusu fidia ya hasara ya jumla ya Sh1 bilioni mahakama imesema baada ya kutathmini imeona kuwa Dola 200,000 (Sh500 milioni) inafaa na kuhusu riba ya asilimia 30 ambayo Tanesco iliomba, mahakama imekataa kiwango hicho badala yake imetoa riba ya asilimia 7 kwa mwaka.