Prime
Mahakama yasikiliza shauri la kupinga Tume ya Jaji Lila, uamuzi Julai 17
Muktasari:
- Rais aliunda na kuteua makamishna wa Tume ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, lakini uteuzi huo ulipingwa mahakamani na wananchi wawili. Shauri hilo limesikilizwa leo na Mahakama imepanga kutoa uamuzi Julai 17.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma, leo Julai 10, 2026 imesikiliza shauri la kupinga uteuzi wa makamishna wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Shauri hilo limesikilizwa na Jaji Wilbert Chuma ambapo mawakili wa pande zote wamevutana kwa hoja za kisheria kuhusiana na uhalali na mamlaka ya Rais.
Tume hiyo maarufu kama Tume ya Jaji Lila, imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na uteuzi wa mwenyekiti makamishna wake ulitangazwa Mei 18, 2026.
Rais Samia ameunda tume kufuatia ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.
Hata hivyo, uamuzi wake wa uundaji na uteuzi wa makamishna wa tume hiyo umepingwa mahakamani kupitia shauri hilo la mapitio ya kimahakama (judicial review) lililofunguliwa na mwanaharakati Bubelwa Ephraim Bubelwa na mwenzake Joseph Daudi Mabugo.
Walalamikiwa katika shauri hilo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila na makamisha wake watatu .
Makamishna hao wa tume hiyo ambao pia ni walalamikiwa katika shauri hilo ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Katika shauri hilo walalamikaji hao wanaiomba mahakama hiyo itengue uamuzi huo wa Rais Samia wa uteuzi wa makamishna wa tume hiyo, na amri ya kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo.
Pamoja na mambo mengine walalamikaji wanapinga uteuzi huo wakidai kuwa Rais amefanya nje ya mipaka ya mamlaka yake ya kisheria na ni kinyume cha sheria.
Pia, wanadai kuwa uteuzi hauna msingi wa kimantiki, unakwenda kinyume na matarajio halali ya waombaji na ya wananchi kwa ujumla, unahusisha matumizi mabaya ya mamlaka ya hiari, na unapingana na masharti ya Katiba.
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo leo, mawakili wa walalamikaji wameieleza mahakama kuwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32(R:E 2023) Rais hana Mamlaka ya kuunda Tume nyingine baada ya Tume ya Jaji Chande kutoa ripoti yake.
Kiongozi wa jopo la mawakili wa walalamikaji, Mpale Mpoki akisaidiana na wakili Hekima Mwasipu, amefafanua kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu cha 21(1) (a) na (b) Rais baada ya kupokea na kuisoma ripoti ya Jaji Chande, alipaswa kuelekeza wale waliotajwa katika ripoti hiyo wachukuliwe hatua za kisheria.
Pia, amedai kuwa Rais hana Mamlaka ya kuunda Tume ya Kuchunguza matukio ya kijinai bali hilo ni jukumu la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Amesisitiza kuwa DPP ndiye pekee amepewa mamlaka kikatiba na kisheria, kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Mashtaka Sura ya 430 ( Marejeo ya mwaka 2023) kuratibu na kusimamia upelelezi na uchunguzi wa makosa ya jinai bila kujali sheria nyingine zozote nchini.
Hivyo, amedai kuwa kama Rais baada ya kusoma ripoti ya Jaji Chande anaona kuna haja ya kuchunguza zaidi anatakiwa kumwagiza DPP ili aliagize Jeshi la Polisi kupeleleza zaidi.
Katika hati ya maelezo na kiapo chao cha pamoja, walalamikaji hao wanadai kuwa awali kufuatia matukio Jeshi la Polisi liliwakamata watu kadhaa maeneo mbalimbali nchini na kuwafungua kesi mbali mbali za uhaini, lakini baadaye Rais akaelekeza waachiwe.
Kisha Rais aliunda Tume ya Jaji Chande ambayo iliwasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026, ambayo katika hotuba yake ya kukabidhi ripoti hiyo mwenyekiti ilieleza kuwa watu 518 waliuawa na wengine kujeruhiwa, idadi ambayo alisema inaweza kuwa zaidi.
Tume hiyo katika hotuba yake ya kukabidhi ripoti ya uchunguzi wa matukio hayo ilipendekeza kuundwa kwa tume nyingine ya kuchunguza ujinai katika matukio mhayo ya ghasia na wakati na baada ya uchaguzi na Rais akaahidi kuunda tume hiyo.
Mawakili hao wamedai kuwa kitendo cha Rais kuunda tume kuchunguza matukio ni ukiukwaji wa dhahiri wa sheria na Katiba kuhusiana na mamlaka ya DPP kuhusiana na kesi za jinai.
Hata hivyo, akijibu madai na hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo wamepinga madai na hoja hizo.
Pamoja na mambo mengine Kalokola amedai kuwa alichokiunda Rais ni Tume ya Uchunguzi na si Tume ya Upelelezi.
Amefafanua kuwa Tume ya Jaji Chande katika mapendekezo yake, hasa pendekezo la nane ilipendekeza iundwe tume nyingine ya upelelezi lakini Rais ameamua kuunda Tume ya Uchunguzi na kwamba hizo ni tume mbili tofauti na hata tafsiri zake kisheria ni tofauti.
Akihitimisha hoja hizo Kalokola amedai kuwa kwa sababu hizo nafuu zinazoombwa katika shauri hilo haziwekani kutolewa, ameiomba mahakama ilitupilie mbali shauri hilo.
Jaji Chuma baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha shauri hilo mpaka Julai 17, 2026 atakapotoa uamuzi.