Mahakama yatupa pingamizi la Selasini, Mbatia
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini.
Muktasari:
Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, jana ilitupa hoja za pingamizi zilizowekwa na Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini dhidi ya aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Samora Kanje (CCM).
Moshi. Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, jana ilitupa hoja za pingamizi zilizowekwa na Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini dhidi ya aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Samora Kanje (CCM).
Akitoa uamuzi huo mbele ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Janeth Makondoo na wakili Simon Mrutu anayemtetea Selasini, Jaji Benedict Mwingwa alisema kwa kuzingatia hoja za pande zote mbili, hoja iliyotolewa na Selasini haina mashiko kisheria.
Alisema mahakama hiyo inafuata utaratibu na masharti ya kiufundi katika kutenda haki kulingana na kifungu cha Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, kipengele cha 117(a), 2(e) .
Alisema haki lazima itendeke kwa kufuata utaratibu, bila kuzuia utaratibu mwingine wa kutenda haki kuendelea kutendeka katika mashauri yanayoendelea mahakamani.
Machi 2, upande wa mjibu maombi wa kwanza anayewakilishwa na wakili Roman Masumbuko, Selasini, aliwasilisha pingamizi mahakamani hapo dhidi ya mleta maombi (Kanje) baada ya kufanya marekebisho ya maombi yake.
Selasini anadai kuwa Kanje alipeleka maombi yake upya yaliyoongezewa vitu vipya katika marekebisho anayotaka yafanyike nje ya muda wa kisheria.
Pia, alikuwa anadai kuwa katika maombi yake hayo mapya, hajaweka vifungu vya sheria vinavyoipa mahakama mamlaka ya kusikiliza maombi yake.
Hata hivyo, Jaji Mwingwa alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa katika hatua za awali Machi 14 na kuwataka mawakili kuzingatia muda kwani kesi hizo zina kikomo.
Wakati huohuo, mahakama hiyo jana ilitupilia mbali hoja za pingamizi zilizowekwa na Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa ubunge wa jimbo hilo (TLP), Augustino Mrema.
Akitoa uamuzi huo mbele ya wakili wa Serikali, Ellen Mwijage akisaidiana na Lilian Machagge, Jaji Mwingwa alisema mahakama hiyo baada ya kupitia hoja zote zilizotolewa, imeona hazina mashiko kisheria.
Machi 2, Mbatia kupitia wakili wake, Mohamed Tibanyendera, aliwasilisha hoja ya pingamizi akidai maombi ya pingamizi yaliyotolewa na Mrema hayakusainiwa na wakili na badala yake alisaini mleta maombi mwenyewe.
Pingamizi jingine linakinzana na kipengele cha tano na fomu A ya Sheria ya Uchaguzi na taarifa alizonazo mleta maombi zinatofautiana.
Kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa Machi 14.
Utata waibuka kesi ya ubunge Longido
Katika hatua nyingine, jalada la kesi ya kupinga ushindi wa ubunge wa Onesmo ole Nangole katika Jimbo la Longido (Chadema) limehamishiwa Mahakama ya Rufaa baada ya kuibuka utata wa kisheria.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Sivangilwa Mwangesi alitoa uamuzi huo jana.
Akifafanua kuhusu utata huo, Wakili Edmund Ngemela alisema Kanuni ya 21 A ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010, zinatoa mwongozo kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Jaji Mkuu 2012 ambaye aliamua kufanya marekebisho ya kanuni hiyo kupitia tangazo la Gazeti la Serikali namba106 mwaka 2012.