Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yatupilia mbali shauri dhidi ya TLS

Muktasari:

  • Mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bartazary Mahai aliwasilisha maombi akiomba zuio muda la kuwasilishwa na kujadiliwa kwa ajenda namba 11 katika mkutano mkuu wa chama hicho wa Aprili 30 hadi Mei 2, 2026 kwa madai kuwa baraza la uongozi la chama hicho

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, imetupilia mbali ombi la mapitio ya mahakama (judicial review) lililowasilishwa na mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bartazary Mahai.

Mahai aliyewasilisha maombi hayo chini ya hati ya dharura alikuwa akiomba zuio la muda la kuwasilishwa na kujadiliwa kwa ajenda namba 11 katika mkutano mkuu wa mwaka 2026 wa chama hicho na kuomba Mahakama hiyo imruhusu kufungua shauri la mapitio ya kimahakama dhidi ya TLS pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Aisha Bade, Aprili 30, 2026 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Jaji Bade amesema ombi hilo liliwasilishwa mapema kaba ya kukamilika kwa taratibu za ndani za chama hicho na kuwa Mkutano Mkuu wa TLs ndiyo chombo kikuu cha maamuzi, ulikuwa bado haujafanyika kikamilifu na ajenda iliyolalamikiwa bado ilikuwa kwenye ratiba.

Amesema mwombaji alikuwa na fursa ya kushiriki, kujadili na kutoa hoja zake ndani ya mkutano huo na kueleza mamlaka ya mapiti ya mahakama hutumika pale taratibu za kawaida au za ndani zimeshindwa ila siyo kwa kuingilia michakato ambayo bado inaendelea.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama iliamua kuwa ombi hilo lilikuwa la mapema na halikukidhi masharti ya kisheria, hivyo kulitupilia mbali.


Msingi wa maombi

Mahai aliwasilisha maombi hayo chini ya hati ya dharura na miongoni mwa nafuu alizokuwa akiomba mahakama hiyo ni ruhusa ya kufungua shauri la mapitio dhidi ya TLS.

Pia aliomba zuio la muda dhidi ya kuwasilishwa na kuajdiliwa kwa ajenda namba 11 katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa chama hicho uliopangwa kufanyika kuanzia Aprili 30 hadi Mei 2, 2026, kiini cha malalamiko yake ni kuwa Baraza la uongozi la chama hicho kupitia mikutano yake ya Aprili 13 na 17, 2026, lilikataa kinyume cha sheria baadhi ya hoja zilizowasilishwa na wanachama kwa ajili kuwasilishwa katika mkutano mkuu wa mwaka.

Wakati maombi hayo yalipowasilishwa mahakaamni hapo mjibu maombi wa kwanza (TLS), aliwasilisha pingamizi la awali lililokuwa na sababu tatu ikiwemo ombi hilo limewasilishwa mapema kwa sababu wakitaka ombi hilo litupiliwe mbali,wakiwasilisha hoja tatu.

Hoja ya kwanza, walidai kuwa ombi hilo lilikuwa la mapema (premature) kwa sababu hakukuwa na uamuzi wa mwisho uliotolewa na Baraza la Uongozi au Mkutano Mkuu ambao ungeweza kupitiwa na mahakama.

Kwa mujibu wao, kile kilichowasilishwa na Mahai kilikuwa ni kumbukumbu za majadiliano tu, si uamuzi rasmi.

Pili, walisisitiza kuwa mwombaji alishindwa kutumia taratibu za ndani za TLS ambazo zipo kwa ajili ya kushughulikia malalamiko ya wanachama.

Walieleza kuwa TLS ina mfumo kamili wa kikatiba unaoruhusu wanachama kuwasilisha, kujadili na kupiga kura kuhusu hoja katika Mkutano Mkuu, ambao ndio chombo cha juu cha maamuzi.

Kwa mujibu wa upande huo, Mahai alikuwa na haki ya kuhudhuria mkutano huo na kuwasilisha hoja zake badala ya kukimbilia mahakamani kabla ya mchakato huo kukamilika.

Tatu, walidai kuwa ombi hilo lilikuwa matumizi mabaya ya mchakato wa mahakama, wakieleza kuwa mwombaji alikuwa akitaka kuzuia ajenda ambayo tayari ilikuwa imeorodheshwa rasmi katika taarifa ya mkutano.

Walisisitiza kuwa hatua hiyo ilikuwa ya kubahatisha na ingeweza kuvuruga shughuli halali za chama.


Hoja za mwombaji

Kwa upande wake, Mahai alipinga pingamizi hilo akidai kuwa halikukidhi vigezo vya kisheria vya pingamizi la awali kwa kuwa lilihusisha masuala ya ukweli yanayohitaji ushahidi.

Ameeleza kuwa kile alichokiwasilisha mahakamani kilikuwa ni ushahidi wa uwepo wa uamuzi usio halali uliofanywa na Baraza la Uongozi, na hivyo kulikuwa na msingi wa mahakama kuingilia kati.

Kuhusu hoja ya kutotumia taratibu za ndani, Mahai alidai kuwa hakukuwa na mfumo wa ndani uliokuwa na uwezo wa kumpatia haki kwa wakati, hivyo akaona ni sahihi kuja mahakamani.

Aidha, alikanusha madai ya matumizi mabaya ya mchakato wa mahakama, akisisitiza kuwa alikuwa akitumia haki yake ya kisheria kulinda maslahi yake na ya wanachama wengine.


Uamuzi wa mahakama

Katika uamuzi wake, Jaji Bade alianza kwa kuchambua kama pingamizi la awali lilikuwa halali na kueleza kuwa kwa mujibu wa kanuni za kisheria, pingamizi la awali linaweza kusikilizwa iwapo linahusu hoja safi za kisheria ambazo hazihitaji ushahidi wa ziada.

Alibainisha kuwa hoja ya kutotumia taratibu za ndani ilikuwa ni hoja ya msingi ya kisheria inayoweza kuamua shauri lote bila kuingia kwenye uchambuzi wa kina wa ushahidi.

Akizungumzia suala la kutotumia taratibu za ndani, Jaji Bade amesisitiza kuwa mahakama haziingilii michakato ya taasisi pale ambapo kuna mifumo ya ndani inayoweza kushughulikia mgogoro huo.

Alieleza kuwa Mkutano Mkuu wa TLS ndio chombo cha juu kabisa chenye mamlaka ya kufanya maamuzi, na mwombaji alikuwa na fursa ya kushiriki kikamilifu katika mkutano huo.

“Nakubaliana na sababu ya kwanza na pili ya pingamizi la awali,ombi hili ni la mapema na haliwezi kutatuliwa kwa kushindwa kutumia mifumo ya ndani wa mjibu maombi wa kwanza (TLS) ,”amesema

Jaji Bade ameeleza kuwa mapitio ya kimahakama hulenga uamuzi uliokamilika, si majadiliano au hatua za awali ambazo bado zinaweza kubadilika,alibainisha kuwa ajenda namba 11 bado ilikuwa sehemu ya mkutano na kwamba mwombaji alikuwa na nafasi ya kushiriki katika mjadala wake.

Katika hitimisho lake, Jaji Bade alikubaliana na pingamizi la kwanza na la pili na hivyo kulitupilia mbali ombi lote na kuwa mwombaji ana haki ya kurejea mahakamani endapo hajaridhika na maamuzi yoyote ya mwisho yatakayofanywa baada ya kukamilika kwa taratibu za ndani.

Mahakama pia iliamua kuwa kila upande ubebe gharama zake.