Mahindi yaliyozuiwa Kenya kuuzwa nchini
Muktasari:
- Wakati tani 432 za mahindi zikikwama katika Mpaka wa Holili wilayani Rombo baada ya zuio la kuingizwa kwa bidhaa hiyo Kenya kwa madai ya sumu kuvu, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amezitaka taasisi na wananchi kujitokeza kununua mahindi hayo.
Rombo/Arusha. Wakati tani 432 za mahindi zikikwama katika Mpaka wa Holili wilayani Rombo baada ya zuio la kuingizwa kwa bidhaa hiyo Kenya kwa madai ya sumu kuvu, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amezitaka taasisi na wananchi kujitokeza kununua mahindi hayo.
Mghwira alitoa rai hiyo jana alipokutana na kamati ya usalama ya mkoa huo kujionea hali halisi katika mipaka ya Holili na Tarakea baada ya kukwama kwa mahindi hayo kwa zaidi ya siku 21 sasa.
“Nitoe hofu kwa Watanzania na walimwengu wote kuwa mahindi yetu ni salama na yamethibitishwa na wataalamu wetu, naomba hili lifahamike kabisa,” alisema Mghwira.
“Kama kuna taasisi au mtu binafsi anahitaji mahindi, wafike ofisi ya mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya ya Rombo apate maelekezo mahindi yalipo ili anunue,” alisema Mghwira.
Alisema kutokana na changamoto ya zuio la bidhaa hiyo ya mahindi, magendo katika mipaka hiyo yameongezeka kwa kasi.
“Hatari iliyopo ni kwamba ukizuia bidhaa wakati inahitajika moja kwa moja sokoni, inakaribisha bidhaa za magendo na ndio maana magendo yameongezeka kwa kasi na taarifa yake tutaitoa baadaye,” alisema Mghwira.
“Niwaombe wafanyabiashara waendelee na utaratibu mwingine wa biashara, lakini mjiepushe kabisa na biashara ya magendo kama inayoendelea sasa hivi, yeyote atakayekamatwa asije akalaumu anaonewa.”
Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Dk Athumani Kihamia alisema mpaka sasa malori 16 yamekwama katika mpaka wa Holili ambayo yana tani 432 za mahindi yaliyozuiliwa kuingia nchini Kenya.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe alisema shehena ya mahindi hayo imelazimika kurejea nchini kutokana na kutopatikana mwafaka.
“Wameanza kuondoa mahindi hapa mpakani kwa kuwa bado taratibu rasmi hazijatolewa na Serikali ya Kenya na jambo hili limekuwa na hasara kubwa kwa wakulima na wafanyabiashara,” alisema Mwaisumbe.
Wiki iliyopita, baadhi ya maofisa wa Serikali ya Kenya waliwataka wafanyabiashara nchini kupima mahindi yao kama hayana sumu kuvu kabla ya kufika mpakani na kugawanya mifuko ya mahindi katika kilo 50 badala ya kilo 100.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wa Mahindi katika mpaka wa Namanga ambaye ni raia wa Kenya, Daniel Wainaina aliomba kusitishwa agizo la kuzuiwa mahindi kuingia Kenya akisema ni hasara kwa wafanyabiashara na wakulima.
Alisema gharama za kuegesha magari katika mpaka huo ni Dola 200 za Marekani kwa siku, jambo ambalo limeongeza gharama kwa wafanyabiashara na baadhi kuamua kurejea Tanzania.