Mahojiano ya Mwananchi na Balozi wa Uswisi Tanzania

Thursday November 25 2021
uswispic

Sehemu ya wafanyakazi wa ofisi ya ushirikiano u-balozi wa Uswisi Tanzania wakiwa na wafanyakazi kutoka Kampuni ya Mwananchi Communications Limited.

Katika kuadhimisha miaka 40 ya ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Uswisi na Tanzania, gazeti la Mwananchi limefanya mahojiano ya kina na Balozi wa Uswisi nchini, Didier Chassot na mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo:-

Tanzania na Uswisi zinadumisha uhusiano wao imara ulioanzia miaka ya 1960; nini kimeumarisha uhusiano huo wa karibu hadi sasa? Je, ni nini kinafanywa ili kuhakikisha unadumu kwa vizazi?

Uswisi na Tanzania zina his-toria ndefu ya ushirikiano wenye manufaa. Mabadilishano baina ya watu wetu yalianza takribani miaka 100 iliyopita. Kwa miongo kadhaa iliyopita, Uswisi na Tanzania zimeendeleza ushirikiano thabiti kupitia mabadilishano ya kisiasa, na ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo.

Nchi zetu mbili zimeshuhudia maendeleo thabiti katika uhusiano wao wa pande mbili katika misingi ya kuheshimiana, kuelewana na kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya watu.

uswispiccc

Balozi wa Uswisi nchini, Didier Chassot.

Tunatazamia kuupa hadhi ushirikiano wa Uswisi na Tanzania na sura mpya, kudumisha kasi ya mabadilishano na kuimarisha zaidi ushirikiano wetu katika kutekeleza Ajenda ya 2030.

Advertisement

Mwaka 1981, Tanzania ilikuwa nchi ya kipaumbele kwa misaada ya maendeleo ya Uswisi; nini kilisababisha uamuzi huo?

Mkakati wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Uswisi unafafanua nchi zilizopewa kipaumbele kwa ushirikiano wa kimataifa wa Uswisi.

Uswisi huchagua nchi za kipaumbele kulingana na vigezo mbalimbali kama vile mahitaji yaliyotambuliwa na ongezeko la thamani ya mchango wa Uswisi.

Ushirikiano wa Uswisi hufanya kazi katika nchi na kanda ambazo zinakabiliwa na migogoro mbalimbali ya kijamii, kimazingira na kisiasa lakini pia zile zinazotengeneza mazingira bora na kujitahidi kuzingatia kanuni za utawala bora. Tanzania ilikuwa na vigezo hivi katika kipindi hiko na mpaka hivi leo.

Mwaka 2021 ni kumbukizi ya miaka 40 tangu kufunguliwa kwa Ofisi ya Ushirikiano ya Uswisi jijini Dar es Salaam. Tuambie baadhi ya hatua kuu zilizofikiwa kwa kipindi hicho.

Mwanzoni mwa miaka ya 80, Uswisi iliamua kwamba kwa kuzingatia hitaji la Tanzania la marekebisho ya muda mrefu ya kimuundo, msaada wa sekta mbalimbali ulikuwa muhimu na ulijumuishwa katika mpango wa msaada wa jumla wa Uswisi.

Uswisi iliidhinisha programu yake ya kwanza iliyotekelezwa kwa miaka mingiya muda mrefu mwaka wa 1986 na tangu wakati huo, tumekuwa na programu sita nchini zilizofanikiwa, programu ya saba imeanza mwaka huu.

Uswisi imechangia zaidi ya Dola bilioni 1 katika kuboresha maisha ya mamilioni ya Watanzania; ni yapi baadhi ya maeneo ya kipaumbele na matokeo yake yalikuwaje?

Ushirikiano wa maendeleo wa Uswisi na Tanzania umekuwa na mafanikio kadhaa. Uswisi imechangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya, hasa katika ufadhili wa afya, ujenzi wa taasisi na mafunzo ya wafanyakazi na wataalamu wa afya.

Moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika vita dhidi ya ugonjwa wa malaria, ambapo Uswisi imechangia kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizo mstari wa mbele katika kupambana na ugonjwa huo.

Kutokana na msaada wa Uswsi kwa Taasisi ya Afya ya Ifakara, kwa mfano, na kwa ushirikiano na vikundi vingine vya utafiti vya kimataifa vya Uswisi na visivyo vya Uswisi, taasisi imeshuhudia uundwaji wa sera za afya ya umma.

Uswisi imeshiriki katika mazungumzo ya kisera yaliyoegemea katika utafiti na imekuwa mstari wa mbele katika kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya.

Utawala bora ni eneo lingine muhimu ambalo Uswisi inajitahidi kuchangia kwa kiasi kikubwa iwezekanavyo nchini.

Uswisi imetoa wataalamu wake wa muda mrefu kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) tangu 2016.

Hili limekuwa na mchango mkubwa katika juhudi za Serikali za kupambana na rushwa. Kwa miaka mingi, Uswisi pia imekuwa ikisaidia Asasi za Kiraia (AZAKI) katika kuimarisha uwajibikaji na vyombo vya habari ili kuwezesha vyombo hivyo kuwa huru na kuboresha ubora wa kuripoti matukio.

Katika sekta ya kilimo, msaada na ushiriki wa Uswisi ulikuwa muhimu katika kufafanua Mkakati wa Kitaifa wa Baada ya Mavuno na Mpango Kazi ili kupunguza hasara baada ya mavuno na ilichochea maendeleo ya soko la msingi la sekta binafsi kwa minajili ya teknolojia baada ya mavuno.

Uimarishaji wa taasisi na kuboresha maisha ya vijana vimeainishwa kama maeneo muhimu chini ya Mpango wa Ushirikiano wa Uswisi kwa Tanzania. Je, ubalozi umetekeleza vipi mikakati ya shughuli hizi?

Mpango mpya wa Ushirikiano wa Uswisi kwa Tanzania ndio umeanza mwaka huu. Lengo kuu la mpango huu ni kuwawezesha vijana hususani wasichana kujiendeleza kijamii na kiuchumi.

Uswisi itaendelea kuchan-gia katika kuimarisha utawala wa kidemokrasia na kusaidia mageuzi ya taasisi za Serikali ili kuongeza mapato ya umma, kugatua rasilimali na kutoa huduma bora za umma, zenye usawa na zinazotatua changamoto kwa wananchi wote.

Msaada wetu pia unaweka mkazo katika kukabiliana na rushwa, ambayo ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya nchi yoyote. Ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi wa matumizi ya fedha za umma, tunaisaidia Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi pamoja na kazi za ukaguzi wa ndani ya Wizara ya Fedha na vyombo mbalimbali vya Serikali katika ukaguzi wao wa matumizi ya fedha za umma.

Uswisi pia inasaidia wanananchi, vyombo vya habari na Azaki katika kuiwajibisha Serikali kuu na za mitaa na kuhakikisha kuwa sauti za wananachi zinasikika katika kufanya maamuzi ya umma.

Kuongezeka kwa idadi ya vijana Tanzania kunatoa fursa kubwa ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuliwezesha kundi hili kuwa chachu kwa maendeleo ya baadaye ya nchi.

Uswisi imejidhatiti kupunguza vikwazo vya kijamii na kiuchumi, kusaidia masuluhisho ya kibunifu na kuimarisha matarajio ya kiuchumi kwa vijana, hasa wasichana, kupitia upatikanaji wa elimu ya ufundi stadi, mafun-zo na masoko.

Kulingana na uzoefu na shughuli yetu wenyewe nchini, Uswisi, tunaamini kwamba Ukuzaji wa Stadi za Ufundi (VSD) unaweza kusaidia kupatikana kwa fursa za ajira kwa urahisi, zenye tija na zenye mapato stahiki, katika mazingira ambayo yanakidhi mahitaji ya kiuchumi.

Upatikanaji wa ujuzi ni changamoto kwa vijana wa Kitanza-nia. Sambamba na Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Stadi za Ufundi (NSDS), Uswisi iliamua kusaidia Mpango wa Ujuzi kwa Ajira Tanzania (SET). Mpango huu unalenga kuboresha upatikanaji, umuhimu na ubora wa ukuzaji wa stadi za ufundi ili kuboresha matarajio ya vijana wenye kujiajiri.

Uboreshaji wa huduma za afya nchini daima imekuwa kipaumbele kwa Uswisi kabla na baada ya kuanzishwa kwa SDC; ni maendeleo gani yamepatikana katika sekta ya afya na ni mipango gani inayoendelea?

Kufikia afya bora bado ni kipengele muhimu katika Mpango wa Ushirikiano. Uswisi inalenga kuimarisha uwezo wa sekta ya afya, kuwezesha shughuli za kiraia kuhusu utawala wa afya, na kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya, ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya afya ya jinsi, uzazi na unyanyasaji wa kijinsia.Tumeanzisha, kwa ushirikiano na UNFPA, Mpango wa Ulinzi wa Vijana (SYP) hapa nchini.

 SYP ni mpango wa ziada ulio-po katika programu zetu zinazolenga vijana. Unalenga usawa wa kijinsia na upatikanaji zaidi wa afya ya jinsi na uzazi, na haki kwa vijana wote wa Kitanzania. Lengo la mpango huo ni kuwajengea uwezo watoto na vijana wenye umri kati ya miaka 10 hadi 24, huku msisitizo ukiwa zaidi kwa mabinti waliobalehe, ili waweze kujikinga dhidi ya magonjwa ya zinaa yakiwemo VVU, mimba zisizotarajiwa, utoaji mimba usio salama, ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia na mila hatarishi zilizopitwa na wakati.

SYP pia inalenga kukuza kanuni za usawa wa kijinsia na taratibu za ulinzi katika nchi mbalimbali.Niliitaja Taasisi ya Afya ya Ifakara tayari lakini niongeze kuwa pamoja na mchango huo katika mpango mkakati wake wa miaka mitano, Uswisi inatoa mtaji wa kuanzisha Kituo cha Ubunifu cha Ifakara, ambacho kinaelekeza nguvu zake katika kutoa suluhisho la changamoto za maisha zinazowakabili vijana wa mkoa huo.

Uswisi ilikuwa na ushawishi mkubwa katika kukuza uwezeshaji wa huduma za afya bora nchini kupitia SDC; tuambie jinsi mawazo ya kibunifu yaliyotekelezwa yamekuwa muhimu katika kuboresha maisha na ustawi wa mamilioni ya Watanzania.

Uswisi imepitisha mtazamo wa pande mbili za uwezeshaji kifedha wa huduma za afya nchini. Kwa upande mmoja, pamoja na washirika wengine, Uswisi imesaidia Mfuko wa Pamoja wa Afya (HBF) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999.

HBF ni utaratibu wa pamoja wa ufadhili unaoruhusu fedha za ndani na nje kufadhili mpango mkakati wa sekta ya afya nchini na baadae mipango ya kila mwaka ya afya katika ngazi ya serikali kuu, mkoa, wilaya na vituo vya afya. Tangu mwaka wa 2018, HBF imefuata utaratibu bunifu ufadhili wa moja kwa moja wa vituo vya afya ambapo asilimia 90 ya fedha za mfuko huelekezwa moja kwa moja kwa zaidi ya vituo 6,000 vya afya vya umma kote nchini.

 Upatikanaji wa fedha katika ngazi ya vituo vya afya umeboresha usimamizi wa fedha za umma na kuwezesha wilaya kutoa hudu-ma bora za afya.Kwa upande mwingine, Uswisi ilizindua mwaka 2010 programu yake ya Ukuzaji Afya na Uimarishaji wa Mfumo (HPSS). Lengo la HPSS ni kutoa huduma ya msingi ya matibabu kwa wakazi wa vijijini kupitia mfuko wa bima ya afya ya jamii.

Mfumo wa bima ya simu za mkononi huruhusu wakazi wa vijijini kupata huduma za afya popote nchini.Ubalozi pia ulishirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuweka mfu-mo wa kikanda wa ‘Jazia’ Prime Vendor kama suluhisho la kuzuia upungufu wa dawa na vifaa tiba kwenye zahanati.

Vile vile tumeanza mazung-umzo kuhusiana na jambo hili na wahusika waliopo Zanzibar na tunatarajia kuunga mkono juhudi hizo katika mwelekeo huo huo.

Vile vile kwa namna gani Uswisi imeisaidia Tanzania kukabiliana na janga la Uviko-19?

Ubalozi ulichukua hatua za haraka mapema katika janga hili kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya Uviko-19. Uswisi ilishiriki kika-milifu katika uratibu wa wafadhili na ilijadiliana na wenzao wa serikali kuhusu masuala kadhaa muhimu.

Maandalizi ya awali ya janga na mpango wa kukabiliana nalo ulibainisha uwezo mdogo wa ufanyaji vipimo wa Maabara ya Taifa. Kwa ombi la serikali na kwa ushirikiano na Taasisi ya Fondation Botnar, Aprili 2020, Ubalozi uliiagiza Taasisi ya Afya ya Ifakara kununua mashine 10 za PCR na vitendanishi ili kusaidia upimaji wa ugatuaji katika vituo 10 nchi nzima, vikiwemo vitatu vya Zanzibar.

Mpango huo huo ulilazimi-sha upanuzi wa namba ya simu maalumu ya taifa kwa ajili ya Uviko-19, ambayo hapo awali ilikuwa ikiendeshwa na wahudumu sita pekee.

Tulisaidia kuongeza uwezo wa namba hiyo kuendeshwa na watu takriban 30 wanaopatikana kila siku kwa saa 24 kwa siku 7 kwa wiki. Aidha, Ubalozi ulitoa ufadhili maalum kwa UNFPA kuendesha dawati la ukatili wa kijinsia ndani ya kituo cha mawasiliano.

Uswisi pia ilisaidia kuendeleza huduma za kawaida za afya ya msingi nchini kote, na WHO na ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa kuimarisha uratibu wa kukabiliana na janga hilo na Serikali na washirika wa nje.

Kukuza mageuzi ya kuwezesha serikali ya Tanzania kutoa hudu-ma bora za msingi kwa raia wake ni moja ya miongozo ya jadi ya Uswisi; ni mageuzi gani makubwa yaliyofanyika?

Uswisi ilisaidia sehemu kubwa ya mageuzi muhimu katika sekta ya afya. Moja ilikuwa kusaidia ugawanyaji wa fedha wa asilimia 90 ya msaada wa sekta ya nje kwa zaidi ya kliniki 6,000 za umma kote nchini.

Uswisi pia ilisaidia upanuzi wa uwezeshaji wa sekta ya afya kupitia bima ya jamii kwa kuunda "Mfuko wa Afya ya Jamii Ulioboreshwa" (iCHF) ili kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watu katika sekta isiyo rasmi.

 Nyingine ni pamoja na dhana ya bima ya lazima ya afya kwa wote, kushughulikia uhaba wa dawa na vifaa vya matibabu, na uwekaji wa mfumo wa kidijitali wa afya.

Uswisi daima imekuwa ikihimiza ubia. Katika miaka 40 ya SDC, ubalozi wa Uswizi Uswisi umefanya kazi vipi na sekta binafsi na serikali kufikia malengo ya pamoja ya maendeleo?

Tunaamini kuwa sekta bin-afsi ina jukumu muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote. Leo, kupitia ushirikiano na sekta binafsi, tayari tunachochea maende-eo ya ubunifu kuhusu mageuzi ya mfumo, teknolojia na mabadiliko ya kijamii ambayo yataathiri vyema maisha ya vijana, hasa wasichana.

 Hii hutokea, kwa mfano, kupitia matibabu ya masafa, mifu-mo ya kisasa ya kujiendesha, usimamizi wa fedha za umma, upelekaji wa usimamizi wa afya kidijitali na msaada wa mitaji ya kuanzisha biashara.

Kupitia "Mpango wetu mpya wa Ubunifu kwa Mabadiliko ya Kijamii", Uswisi itashirikiana na washirika wa sekta binafsi ili kuanzisha Mfuko wa Uchagizaji Ubunifu (Innovation for Social Change Programme) ambao hutoa fedha zinazohusiana na athari na kujenga uwezo wa kiufundi kwa makampuni ya kijamii yenye athari katika jitihada zao za ukuaji.

Orodha inaendelea. Hakika tunalenga kuongeza zaidi wigo wa ushiriki wetu wa sekta binafsi nchini Tanzania.

Mradi wa Fursa kwa Ajira za Vijana (OYE) chini ya ubia wa Uswisi na Tanzania umesaidia wajasiria-mali vijana wa Kitanzania kuanzisha biashara; ni vijana wangapi wamefaidika moja kwa moja na mradi huo na lengo kubwa ni lipi?

Mradi wa OYE unalenga kuon-geza ajira na mapato ya vijana kwa kukuza ujuzi na umahiri kupitia mafunzo mahsusi ya stadi za maisha za kiufundi na kiujuzi, uanagenzi na msaada baada ya mafunzo.

Matokeo yake, vijana wanatayarishwa kwa fursa za soko la ndani kwa ajili ya ajira na maendeleo ya biashara katika sekta zenye uwezekano madhubuti wa kuten-geneza ajira.

Kuanzia 2016 - 2019, mradi huo ulinufaisha zaidi ya vijana wa kike na wa kiume 16,000 kupitia mafunzo ya kiufundi, maisha na ujuzi wa biashara.Awamu ya pili ya mradi wa OYE ilizinduliwa mwaka huu na inatarajiwa kuwa na athari zaidi.

Majadiliano ya mabadiliko ya tabi-anchi ni kipaumbele kwa serikali ya Uswisi. Zaidi ya mikataba na majukwaa ya kimataifa, je, kuna juhudi nyingine zilizoongezwa za kuishirikisha Tanzania katika suala la mabadiliko ya tabianchi na kutekeleza Mkataba wa Paris miaka 40 iliyopita?

Nchini Tanzania misitu ya asili inatoweka. Ukataji miti huchangia matatizo mbalimbali ya mazingira ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa, upotevu wa viumbe hai, mafuriko, kupungua kwa mtiririko wa mito wakati wa kiangazi na maporomoko ya ardhi. Ukataji miti mwingi hutokea kwenye ardhi ya kijiji, na kilimo na uzalishaji wa mkaa ndio vichocheo vyake kuu.

Hivi sasa takriban asilimia 85 ya mahitaji ya nishati ya Tanzania yanatoshelezwa kwa kutumia mkaa na kuni, ambayo ni ya gharama nafuu na inapatikana ndani ya nchi.

Wakati matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati vikiendelea, inatarajiwa kwamba hii itabaki kuwa chanzo kikuu cha nishati kwa angalau miaka 20.

Tangu mwaka wa 2012, Uswisi imekuwa ikiunga mkono modeli ya usimamizi wa misitu katika jamii (CBFM) yenye biashara endelevu za misitu ya asili, kama vile uzalishaji wa mkaa na uvunaji wa mbao.

Mtindo huu umeoneka-na kuwa mzuri katika kuhamasisha jamii kuhifadhi misitu kwenye ardhi ya kijiji kwa kuboresha kipato kwa wazalishaji, kurasimisha uzalishaji na kupata mapato ya miradi ya maendeleo ya jamii. Katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya programu, upunguzaji mkubwa wa viwango vya ukataji miti ulisajiliwa.

Hata hivyo, hali hii inaonekana sasa kuwa nyuma, ambayo ni sababu ya wasiwasi. Uswisi iliunga mkono serikali katika jiti-hada zake za kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Sera ya Misitu (2021 - 2031) unaowe-ka lengo la kuongeza maeneo ya CBFM kutoka milioni 2.7 leo hadi hekta milioni 16 mwaka 2031.

Je, wewe kama balozi unajivunia nini zaidi, na huduma yako inapoisha, ni urithi gani ungependa kuacha kama taswira ya uhusiano mpana wa Uswisi na Tanzania?

Sio suala la kujivunia sana lakini natumai, wakati ukifika, kuweza kutazama nyuma na kusema kwamba pamoja na timu ya Ubalozi tulifanya kila tuliloweza na kusaidia zaidi kisiasa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania na kuongeza wigo wa uhusiano na kuimarisha urafiki kati ya nchi zetu mbili, kwa moyo huohuo wa kuheshimiana, faida na ustawi ambao umetupa msukumo hadi sasa.

Lakini, jamani!, bado nina miaka michache katika nchi hii nzuri kwa hivyo tafadhali msiwe na haraka ya kuniona nikiondoka

 #SDC40TZ  #SwissEmbassyTZ


Advertisement