Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MAHUBIRI: Mungu akupe neema kuona kwa usahihi

Mhubiri Peace Marino anapatikana Kanisa la KKKT Nyashimo, Busega mkoani Simiyu. Kwa maombi, ushauri na sadaka; 0783 999 044.

Muktasari:

  • Macho haya wakati mwingine hayaoni kwa usahihi, wengi tumefanya uchaguzi kwa sababu ya kile macho yetu yameona, tumevutwa na tamaa ya macho na kwa namna moja ama nyingine tukajikuta tuko kwenye shida kwa sababu ya uamuzi tuliofanya baada ya macho kuona.

Mpendwa, nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliyehai. Ni imani yangu kuwa unaendelea vizuri na Mungu anaendelea kukutetea kila siku iitwapo leo. Ninamtukuza Mungu kwa ajili yako kwa neema aliyokupa kusoma ujumbe wa leo hakika wewe ni wa thamani sana kwetu na Mungu akubariki.

Ujumbe wa leo unasema “Mungu akupe kuona kwa usahihi”, Msingi wa neno hili tunaupata kutoka katika kile kitabu cha Mwanzo:13. Ni habari za Abramu na Lutu, Mungu aliwabariki na mali nyingi na mahala walipokuwa wakiishi hapakuwatosha na ukazuka ugomvi kati ya wachungaji wa Abramu na Lutu, kwa hekima za Abramu (ambaye alikuwa baba mkubwa wa Lutu) akaamua watengane na akampa nafasi Lutu ya kuchagua ni upande gani ataelekea. Mstari wa 10 neno la Mungu linasema Lutu akainua macho yake, akaliona bonde lote la Yordani ya kwamba lote pia lina maji.

Kabla Bwana hajaharibu Sodoma na Gomora lilikuwa kama bustani ya Mungu. Nini tunajifunza hapa, Lutu aliangalia kwa macho ya nyama, akaona ni upande gani unavutia hakupata muda wa kumuuliza Mungu ni mahala gani sahihi kwakwe pa kwenda.

Mpendwa macho haya wakati mwingine hayaoni kwa usahihi, wengi tumefanya uchaguzi kwa sababu ya kile macho yetu yameona, tumevutwa na tamaa ya macho na kwa namna moja ama nyingine tukajikuta tuko kwenye shida kwa sababu ya uamuzi tuliofanya baada ya macho kuona.

Ndoa nyingi siku hizi zinapitia changamoto mbalimbali kwa sababu wengi tumedanganywa na macho, wanaume wakitaka kuona wanaangalia miguu mizuri, umbo zuri, macho, mazuri, sura ya kuvutia kisha macho yakiridhika anasema hapa nimepata mke lakini hata muda wa kuomba hana. Akiingia kwenye ndoa ndipo anagundua kuwa umbo zuri alilopenda haliwezi kufanya majukumu ya mke. Vivyo hivyo kwa wanawake pia wanamachaguo yao kwa kadri macho yao yanavyovutiwa, macho yanavutiwa na kijana mrefu, six pack, awe na fedha, gari haijalishi vitu hivyo kavipata wapi. Akifika ndani kilio kinaanza anagundua kuwa alifanya uamuzi ambao siyo sahihi. Mithali 19:14. Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana. Ukitaka mke au mume mwema omba kwa Mungu atakupatia wa kufanana na wewe, macho yasikudanganye.

Mstari wa 13. Lakina watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya Bwana. Watu hawa ndio ambao Lutu anaenda kukaa nao, watu ambao wamefanya machukizo mengi mbele za Bwana na gadhabu ya Mungu tayari ilikuwa juu yao na kwa sababu Lutu alidanganywa na macho yake anajikuta anaishi na watu hawa. Ninakuombea siku ya leo, katika Jina la Yesu Mungu akupe kuona kwa usahihi.

Abramu anapata neema kutoka kwa Mungu, baada ya kutengana na Lutu Mungu anamwambia inua macho yako ukatazame kutoka hapo ulipo upande wa kaskazini, kusini, mashariki na magharibi maana nchi hii yote uionayo nitakupa wewe na uzao wako hata milele (Mart 14-15) Mungu akiwa upande wako atakupa kuona hazina zilizofichika ambazo kwa macho ya kawaida huwezi kuona. Abramu akapata kibali kutoka kwa Bwana, akaongezeka na kuzidi sana.

Mpendwa kuna faida nyingi kumtegemea Mungu na kumshirikisha katika kila jambo unaloyafanya, yapo mambo mengi yanayoendelea katika ulimwengu wa roho ambayo hatuwezi kuyaona kwa macho ya kawaida, mfano ni ujumbe unaopatikana 2Wafalme 6:15-17.

Hata asubuhi na mapema mtumishi wake Yule mtu wa Mungu alipoondoka na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu na farasi na magari wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia ole wetu Bwana wangu tufanyeje? Akamjibu usiogope maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. Elisha akaomba akasema Ee! Bwana nakusihi mfumbue macho yake apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi naye akaona na tazama kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.

Tumezingirwa pande zote na jeshi la malaika wa Bwana, adui hawezi kutupata. Tatizo ni kwamba hatuoni vile tunavyolindwa na Bwana, unaweza kuwa na wasiwasi mwingi lakini nikutie moyo wewe ambaye unamcha na kumtegemea Bwana uwe na uhakika ya kuwa Mungu siku zote anatulinda hivyo hauna cha kuogopa. Neno la Mungu linasema tunamacho lakini hatuoni (Ezekieli 12:2) kwa sababu gani ili uweze kuona kwa usahihi unahitaji jicho la ki-Mungu.

Ni maombi yangu siku ya leo kuwa Mungu afumbue macho yako, uone sawa sawa na aonavyo yeye, yule mtumishi wa Elisha kama asingefumbuliwa macho ya rohoni hangeweza kuona jeshi kubwa la mbinguni ambalo mara zote lilikuwa likimlinda Elisha.

Sisi tunalindwa na Bwana. Watutafutao ni wengi, watuwindao ni wengi lakini kwa sababu ya upendo mkuu wa Mungu kwetu ndio maana tu hai, ndio maana tuko hivi tulivyo kwa sababu yeye Bwana siku zote hutulinda. Mungu akubariki, Mungu afumbue macho yako, Mungu akupe macho ya kuona. Amen.


Mhubiri Peace Marino anapatikana Kanisa la KKKT Nyashimo, Busega mkoani Simiyu. Kwa maombi, ushauri na sadaka; 0783 999 044.