MAHUBIRI: Usikubali kupokea taarifa mbaya
Daima usikubali kirahisi kupokea taarifa mbaya
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Naamini kwa neema ya Mungu unaendelea vizuri na ninamtukuza Mungu kwa kukupa kibali tena leo kusoma ujumbe huu, ni maombi yangu kuwa Roho Mtakatifu atakusaidia kuelewa.
Nikukaribishe katika tafakari ya ujumbe wa leo unaosema “Usikubali kirahisi kupokea taarifa mbaya”. Taarifa ni ujumbe anaopokea mtu juu ya jambo fulani, ujumbe huo waweza kuwa mzuri au mbaya.
Taarifa mbaya ni ile inayokufanya ukose amani au kupoteza tumaini na wakati mwingine usijue cha kufanya. Leo natamani nikutie moyo kuwa unapokutana na taarifa za kuumiza moyo, usikubaliane nazo kwa wepesi kwa sababu ipo nafasi ya wewe kuweza kufanya jambo ambalo linaweza kubadili taarifa hiyo mbaya na kugeuka kuwa nzuri au ya amani.
1Samweli:3:13-18 ni habari za mtumishi wa Mungu Eli pamoja na watoto wake (Hofni na Finehasi) Samweli anapewa ujumbe juu ya nyumba ya Eli kuwa kwa sababu ya uovu walioutenda na wala baba yao hakuwazuia basi watakufa, taarifa hii haikuwa nzuri kwa Eli lakini jambo la kushangaza ni kwamba Eli anapoipokea habari hiyo anasema “Ndiye Bwana; na afanye alionalo kuwa ni jema” naweza sema kuwa jibu la huyu mtu wa Mungu ni la kukata tamaa, yamkini uovu wa wanaye ulishamuumiza kiasi kwamba hakuona sababu ya yeye kuwaombea radhi, yamkini kama baba alipambana kuona wanaye wanafuata njia zake lakini jitihada zake zikagonga mwamba. Pamoja na kwamba alikuwa mtumishi si ajabu alikuwa na kidonda cha kudumu juu ya watoto wake kwa kutofuata njia ipasayo na tayari aliwakatia tamaa.
Mtumishi wa Mungu Eli ni mfano mzuri wa wazazi wengi ambao tumepitia changamoto nyingi juu ya malezi ya watoto wetu, tulitamani watoto wetu wawe kama sisi (kama tu uko vizuri), wafanye kazi kama zetu au nzuri zaidi lakini maumivu yamekuwa ni makubwa kwa sababu vile tulitamani wawe haiko hivyo. Mpendwa leo Mungu analo neno la faraja juu yako na familia yako, haijalishi nyumba yako si mahali pa kukimbia tena au kazini kwako, nataka nikutie moyo kuwa bado tumaini lipo kama utachagua kumtegemea Mungu.
Nikutie moyo kupambana, usikate tamaa. Mungu anajivunia wewe, mwambie tu Mungu taarifa hii mbaya nimeisikia lakini si yangu. Haijalishi umefukuzwa kazi, mumeo au mkeo ana mchepuko, umetengwa kwa sababu ya uaminifu na utii wako, cheo kazini umeshushwa, madeni yamekuwa mengi hata huoni wapi pa kushika. Mpendwa, bado unayo nafasi ya kubadilisha yote hayo, jitie nguvu katika Bwana na songa mbele.
Isaya 38. 1-5. Baada ya Hezekia kuugua kwa muda mrefu, nabii Isaya anatumwa kumwambia “Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa wala hutapona”. Taarifa hii ni ya kuogopesha na kutia hofu pamoja na kukatisha tamaa.
Lakini pamoja na kwamba Hezekia yuko kitandani hajiwezi, jambo la kutia moyo ni kwamba hakubaliani kabisa na taarifa hii, anachokifanya, anageuka (yamkini alitambua wapi alikosea akaanza kutengeneza na Mungu wake).
Baada ya hapo sasa anaanza kumkumbusha Mungu juu huduma yake, alivyojitoa katika utumishi, mema aliyotenda, kazi alizofanya na kila kitu ambacho kingeweza kumsaidia ili aepukane na balaa lililokuwa mbele yake, Hezekia anangangana! Anaomba kwa machozi ili Mungu aweze kumsikia na kumrehemu na Mungu alisikia Maombi yake na hatimaye kumuongezea miaka kumi na mitano.
Mpendwa inawezekana kabisa taarifa mbaya kugeuka na kuwa taarifa nzuri na mara zote nyuma ya tarifa mbaya huwa iko neema ya Mungu. Wako watumishi wengi waliopambana baada ya kupokea habari mbaya, tumesikia kwa habari ya Ester juu ya kuuliwa kwa Wayahudi na kile Mungu alifanya kwa ajili yao baada ya kuomba (Esta:…) Tumesikia kwa habari ya wapelelezi waliotumwa na Musa kuipeleleza nchi ya kanani walileta taarifa mbaya kwa Waisrael kuhusu nchi ile, lakini Musa hakuridhika na habari ile alipambana na kuwatuma wengine na wakaleta habari njema kwao (Hesabu 13).
Mtumishi wa Mungu Yona anatumwa Ninawi na anapeleka taarifa mbaya kwao, na kuwaambia “Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa” taarifa hii watu wa Ninawi pamoja na mfalme wao wanapoisikia hawakunyamaza, wanaanza kapambana kufunga na kuomba ili Mungu aweze kuwanusuru na ghadhabu hiyo na Mungu kwa rehema yake kuu anausamehe mji wa Ninawi.
Ujumbe wa leo umekuja mahususi kwa ajili yako, sijui unataarifa gani mbaya inayokusumbua, Mungu amekuona na anatamani kukusaidia.
Nikutie moyo tu kuwa nyuma ya hiyo taarifa mbaya iko neema ya Mungu, usiseme na iwe kama Bwana alivyokusudia hapana! Geuka kama Hezekia, mlilie Mungu, mkumbushe juu ya yale mema umekuwa ukitenda na mwambie aingilie kati ili kukusaidia.
Ni maombi yangu kwako kuwa taarifa hiyo mbaya itageuka na kuwa ushuhuda. Bwana Yesu asifiwe. Nikutakie Baraka za Bwana na Mungu akubariki kwa kusoma ujumbe huu.
Mwalimu Peace Marino
Usharika wa KKKT Ebeneza Nyashimo
Kwa maombi na ushauri 0783999044.