Maisha na uchumi nyuma ya biashara ya bodaboda

Kinachoshuhudiwa ni wingi wake tu, lakini usichokifahamu ni kuwa hapa nchini bodaboda ni miongoni mwa bidhaa ambazo huchukua kiwango kikubwa cha fedha za kigeni kwa mwaka kuliko hata, sukari, mafuta ya kupikia hata viuatilifu.

Katika kipindi cha mwaka kilichoishia Februari 2023 thamani pikipiki zilizonunulia kutoa nje ya nchi ilifikia Dola 136.7 milioni, sawa na Sh319.87 bilioni, kiwango hicho ni zaidi ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2021/2022. Vijana wengi ambao hawana ajira mijini na vijijini hukimbilia bodaboda.

“Namshukuru Mungu japokuwa inaonekana ni kazi ya kushinda juani na kunyeshewa na mvua lakini nimejenga nyumba, nacheza mchezo kila siku Sh15, 000 mimi na mke wangu na ninasomesha watoto wangu kupitia kazi hii,” alisema Said Rupia, dereva bodaboda jijini Dar es Salaam.

Rupia, bodaboda maarufu katika kituo cha Tabata Relini anasema anaifurahia kazi yake na imemletea manufaa kadhaa na amefanikiwa kujenga nyumba yake kupitia kazi hiyo ambayo baadhi ya watu wanaweza wasiithamini kama afanyavyo yeye.

“Hii kazi kama zilivyo kazi nyingine inahitaji nidhamu kuifanya na katika matumizi kwa kile unachokipata. Kwa siku sikosi Sh40,000 hadi Sh50,000, miaka ya nyuma nilikuwa naingiza kwa siku kuanzia Sh70,000, wakati mwingine hadi 100,000,” alisema Rupia.

Anasema kabla ya kugeukia bodaboda alikuwa anaendesha magari makubwa ya safari ndefu, lakini baadaye aligundua kuwa kazi anayoifanya haiendani na malengo yake, hivyo akaamua kuacha kwa sababu hakufanikiwa kutimiza mipango yake ya maisha.

“Baada ya kuachana na malori nikaanza kuendesha bodaboda na nilikuwa nikiweka akiba kwa siku Sh30,000, namshukuru Mungu nikanunua kiwanja nikaanza ujenzi kidogokidogo,” alisema Rupia na kuongeza kuwa mpaka sasa amewashawishi vijana zaidi ya tisa kijiweni kwake kununua ardhi na kujenga.

Rupia alisema changamoto inayowakabili waendesha bodaboda ni ajali ambazo zimechukua uhai wa wengi na baadhi kusalia wakiwa walemavu wa kudumu, hivyo anatoa rai kwa waendesha bodaboda wote kuwa makini wanapokuwa barabarani na kufuata sheria zote.

Katibu wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki Mkoa wa Dar es Salaam (CMTB), Samson Njoka anasema kuendesha bodaboda yeye anaiona kama fursa ya ajira nchini, kwani imeajiri watu wengi na baadhi yao wamefanikiwa kimaisha.

Njoka, ambaye kwa sasa anamiliki bajaj iliyotokana kazi yake ya bodaboda anasema kubadilisha maisha inawezekana ikiwa mtumiaji ataiheshimu kwa kuzingatia sheria za barabarani na kuwa mwaminifu kwa wateja wake.

Anasema kusingekuwa na bodaboda huenda matukio ya uhalifu yangekuwa mengi, kwani kwa sehemu kubwa shughuli za bodaboda zimesaidia kuajiri vijana wengi, hivyo idadi ya watu wasiokuwa na shughuli ya kuingiza kipato inapungua.

“Nimeendesha bodaboda, nimefanikiwa kununua bajaj yangu ambayo ndio ninaendesha kwa sasa, naifurahia kazi yangu,” anasema Njoka, ambaye alidokeza kuwa licha ya kuwa hakuna utafiti rasmi uliofanyika, idadi ya waendesha bodaboda na bajaji kwa Jiji la Dar es Salaam pekee ni zaidi ya 10,000.


Zinasaidia wafanyabiashara

Upande mwingine wa shilingi ambao kwa watu wanaotumia bodaboda kibiashara lakini si waendeshaji, wao wameweka mitaji kwa kununua pikipiki kuwapa waendeshaji kwa mikataba ya kulipa kiasi kwa siku, wiki au mwezi.

“Huwa nina utaratibu wa kununua bodaboda mbili ninawapa vijana waendeshe, kwa siku kila mmoja ananiletea Sh10,000, baada ya mwaka mmoja inakuwa ya kwake, hapo nakuwa nimepata faida ya Sh1.2 milioni,” anasema Jackson Edward.

Edward anasema alikuwa akitoa mkataba wa mwaka mmoja kwa dereva miaka ya nyuma kabla bei ya chombo hicho haijapanda, lakini sasa anatoa mkataba wa mwaka mmoja na miezi miwili hadi mitatu. Bodaboda zinazopendwa hivi sasa ni kuanzia Sh2.7 milioni hadi Sh3 milioni.

“Mara nyingi huwa nanunua bodaboda kwa lengo fulani, mfano naweza kununua ili iwe inatoa matumizi ya kila siku nyumbani au kumhudumia mama yangu kijijini, inaniondolea ile hali ya kuwaza kuacha hela kila siku na kutakiwa kumtumia mama hela,” alisema Edward.

Ali Salehe yeye alisema baada ya bodaboda kupanda bei na hatari ya baadhi ya waendeshaji kutokuwa waaminifu amebadili muundo wake wa biashara na sasa hanunui bodaboda mpya, ananunua zilizotumika na kuwapa watu kwa mkataba wa muda mfupi ambao unamuacha na faida ya hadi Sh800, 000 pindi mkataba unapofika mwisho.

“Kuna namna nyingi ya kufanya biashara ya bodaboda, unaweza kumpa mtu akawa anakuleta hesabu kwa siku kama Sh7, 000 lakini mimi napendelea mkataba ambao nampa mtu ananiletea Sh10, 000 baada ya muda wa mkataba kuisha inakuwa ya kwake.


Inachangia uchumi, kipato

Profesa Aurelia Kamuzora ambaye ni mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe amesema bodaboda ni shughuli ya kiuchumi ambayo inawapa watu kipato cha kila siku, lakini pia huchangia uchumi wa nchi kwa namna mbalimbali.

“Tumeona vijana wakitumia mapato yatokanayo na pikipiki kujenga nyumba, kusomesha watoto na kuendesha maisha yao, wanalipa kodi ya Serikali kupitia leseni, lakini pia usafiri wa bodaboda unasaidia usafirishaji wa bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa haraka,” alisema.

Alisema kwa ukubwa wa shughuli za bodaboda nchi ilitakiwa kuwa kiwanda cha kuunda vipuri au pikipiki zenyewe, kwani kuagiza nje ya nchi kunatumia fedha nyingi za kigeni.

“Kwa upande wa usalama Serikali inahitaji kuzitambua bodaboda na kuziundia sera za usalama zaidi, nchi nyingine hutengeneza barabara za pembeni kwa ajili ya pikipiki na baiskeli, japo sina idadi kamili ila kwa sasa wanapata ajali nyingi, tunahitaji kuangalia sera zipi za kiuchumi na ujenzi wa barabara ili kuwapa usalama zaidi,” alisema.

Naye Dk Mwinuka Lutengano, mtaalamu wa Uchumi na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) anasema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine zinazoendelea kuna kundi kubwa la watu ambao wanajishughulisha kwenye sekta isiyo rasmi na hasa vijana.

“Shughuli ya kuendesha bodaboda hapa nchini ina maana kubwa, vijana wanapata kipato na wamekuwa msaada mkubwa kwao wenyewe na kundi kubwa la wanaowategemea. Lakini pia, msaada ni mkubwa kwa wale wanaopata huduma ya usafiri huo kwa haraka na unafuu kwenye baadhi ya maeneo,” alisema.

Mtaalamu huyo wa uchumi anaendelea kuwa kutokana na mazingira ya jiografia ya nchi, bado kuna maeneo na njia zina changamoto ya usafiri na hizo pikipiki ni msaada pia hata katika maeneo hayo.