Majaliwa ataka bei kikomo ya saruji nchini

Majaliwa ataka bei kikomo ya saruji nchini

Muktasari:

Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kukamilisha utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji ili kuuwezesha kila mkoa kujua bidhaa hiyo inapaswa kuuzwa kwa bei gani.

Dar es Salaam. Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kukamilisha utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji ili kuuwezesha kila mkoa kujua bidhaa hiyo inapaswa kuuzwa kwa bei gani.

Lengo la kufanya hivyo ni kudhibiti upandishwaji holela unaofanywa na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.

Ametoa maagizo hayo leo Jumatatu Desemba 7, 2020 alipozungumza na wakuu wa Mikoa, katibu mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, kaimu katibu mkuu Wizara ya Uchukuzi, maofisa biashara wa Mikoa, mawakala wa saruji walioko mikoani na wakurugenzi wa viwanda vya saruji kupitia kikao kilichofanyika kwa njia ya mtandao.

Akizungumza katika kikao hicho, Majaliwa amesema ni lazima utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji ukamilike ili kujua kila mkoa bidhaa hiyo inapatikana kwa kiasi gani.

“Mfano saruji inazalishwa Tanga au Dar es Salaam halafu Morogoro inauzwa Sh 28,000 sasa Kigoma itauzwaje lazima kuwe na bei kikomo.”

“Suala hili halihitaji kuundiwa bodi kwa sasa kwani vyombo vya kusimamia biashara vipo, wizara husika ipo, hivyo wahusika wote mhakikishe mnasimamia suala hili kikamilifu ili kuwawezesha wananchi kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu,” amesema Majaliwa.

Waziri mkuu alitumia nafasi hiyo pia kuwaonya mawakala wa saruji kutoficha bidhaa hiyo kwa lengo la kupandisha bei kwa sababu kitendo hicho ni sawa na uhujumu uchumi, huku akisema watakaobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

“Tume ya Ushindani (FCC) fanyeni ukaguzi ili kubaini kama bei za bidhaa hiyo ni shindani na ina tija kwa wananchi kwa sababu katika maeneo mengine hazina uhalisia na zinasababisha usumbufu nchini,” amesema Majaliwa