Majaliwa atoa neno kwa mashirika ya umma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

  • Akifungua mkutano wa viongozi wa umma, Ikulu jijini Dar es Salaam, Majaliwa amesema mashirika ya umma yana nafasi kubwa ya kusukuma maendeleo ya taifa katika nyanja mbalimbali kama  ilivyofanya nchi ya Korea Kusini, miaka 50 iliyopita.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameyataka mashirika ya umma kujijengea uwezo yenyewe na kuisaidia Serikali kutekeleza mpango wa pili wa maendeleo wa mwaka 2016/17 - 2020/21.

Akifungua mkutano wa viongozi wa umma, Ikulu jijini Dar es Salaam, Majaliwa amesema mashirika ya umma yana nafasi kubwa ya kusukuma maendeleo ya taifa katika nyanja mbalimbali kama  ilivyofanya nchi ya Korea Kusini, miaka 50 iliyopita.

Amewataka watendaji wa mashirika hayo kuwa wabunifu na kuyafanya mashirika yao kujiendesha kwa faida kiasi cha kufanya shughuli zao mpaka nje ya nchi au kuanzisha kampuni.

"Baadhi ya watendaji wa mashirika haya, wanachofanya ni kuhakikisha mashirika hayafi, kwa maana yaendelee kuwepo tu. Ni kama kuweka boya kwenye chombo baharini ili kusizame, lakini pia kisitembee. Hatuwezi kufika kwa mtindo huo," amesema kiongozi huyo.