Majaliwa awasimamisha kazi vigogo sita Arusha

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi sita wa Halmashuri ya Jiji la Arusha, akiwapo Mkurugenzi wa Jiji hilo, Dk John Pima ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma zinazowakabili.

Arusha. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi sita wa Halmashuri ya Jiji la Arusha, akiwapo Mkurugenzi wa Jiji hilo, Dk John Pima ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma zinazowakabili.

Waziri Mkuu amewasimamisha vigogo hao leo Jumanne Mei 24, 2022 baada ya kubaini ubadhirifu unaofanyika katika Halmashauri ya Jiji la Arusha ikiwamo kupangisha shule ya msingi binfsi ya mchepuo wa kiingereza ya Sojemu iliyopo Kata ya Muriet.

Wengini waliosimamishwa kazi ni Mariamu Mshana ambaye ni mweka hazina wa Jiji hilo, Alex Daniel , Innocent  Maduhu na Nuru Kinana kutoka ofisi ya mchumi pamoja na Joel ambao yupo katika Halmashauri ya Longido kwa sasa.

Majaliwa ameagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuanza kazi ya ukaguzi tuhuma hizo kwani ni kinyume na sheria na itakapobainika hatua za kisheria zichuliwe haraka ili kukomesha tabia hiyo.

"Kwa hiyo basi kwa mujibu wa sheria John Pima, mweka hazina Mariamu Shabani, Inocent maduhu, Alex Daniel wote ni wachumi wakae pembeni kupisha uchunguzi," amesema

Majaliwa amesema kuwa kuna baadhi ya vifaa vya ujenzi wa miradi ya Serikali ilijenga miradi yake ikiwamo mabanda ya ng’ombe na nyumba ya mkurugenzi wa Jiji hilo.

Majaliwa amesema halmashauri hiyo kupitia mkurugenzi huyo imekuwa ikighushi nyaraka pamoja na tabia ya kuhamisha wafanyakazi mara kwa mara ikiwa kama njia ya kufanya maovu.

"Ikiwa madudu hayo ikiwemo mtumishi wa Jiji la Arusha ambaye ni mchumi kuingiziwa Sh65 milioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mitaa na kata kitendo ambacho si kweli ikiwa kila kata huwa na akaunti," amesema Majaliwa