Majaliwa azipiga ‘pini’ kampuni za upimaji ardhi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Muktasari:
- Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Oktoba 6, 2023; na ofisi ya Waziri Mkuu na kusambazwa kwa vyombo vya habari imeonyesha kuwa hatua hizo zinatachukuliwa kwa kampuni zote ambazo zina mikataba na zile zisizo na mikataba.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kampuni za upimaji viwanja zilizoshindwa kukamilisha kazi hiyo jijini Dodoma mikataba zichukuliwe hatua kali za kisheria.
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Oktoba 6, 2023; na ofisi ya Waziri Mkuu na kusambazwa kwa vyombo vya habari imeonyesha kuwa hatua hizo zinatachukuliwa kwa kampuni zote ambazo zina mikataba na zile zisizo na mikataba.
“Moja kati ya hatua hizo, ni ‘kuzi-blacklist’ kwa sababu makampuni hayo yapo, tutumie makampuni ambayo yana uaminifu badala ya kutumia makampuni ambayo yanatuzalishia migogoro,” sehemu ya taarifa hiyo imemnukuu Waziri Mkuu.
Imeelezwa kuwa Majaliwa ametoa maagizo hayo kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, kikihusisha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma, lengo likiwa kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo na kutafuta suluhisho.
“Tunatambua makampuni mengi hapa Dodoma ni ya watumishi wenyewe kama ambavyo imeelezwa kwenye ripoti. Mkurugenzi alikuwa na kampuni mbili, Mhasibu wake ana kampuni yake na wanazitumia kupima maeneo, kwa hiyo ni miradi yao.” Sehemu ya taarifa hiyo imesema.
Kwa mantiki hiyo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha makamishna wasaidizi wa mikoa, maafisa mipango miji na majiji, halmashauri na Manispaa, kutochukua watumishi wa muda kufanya kazi ya upimaji bali wafanye wao ili kuepusha mianya ya rushwa.
Pia ameagiza vibarua wanatembea na nyaraka za Serikali na kuuza viwanja kwa niaba ya maofisa wa jiji, watafutwe na kukamatwa.
Taarifa hiyo imewataja vibarua hao kuwa ni Justin Albert, Freddy Mathias, Elias na Magige ambapo imeagizwa kuwa: “watafutwe, wachunguzwe na vyombo vya dola kuhusu nyaraka za Serikali walizonazo, na wazirejeshe nyaraka za Serikali wanazozitumia vibaya kwa kuendelea kuuza viwanja maeneo ya Jiji ya Ukanda wa Kijani, Mkonze, Ndachi, Chinyika, Ng’ong’ona na Mkalama.”
“Hawa ni vibarua, lakini wana ramani na wanavijua viwanja vyote. Wao wanachofanya ni kufanya mauzo halafu wanapeleka kwa watu wao pale jiji na hati zinatoka. Kwa hiyo, watafutwe na wanyang’anywe zile nyaraka ili wasiendelee kuuza viwanja,” ameagiza.