Majambazi wapora milioni 15 Mpanda

Majambazi wapora milioni 15 Mpanda

Muktasari:

Walivamia viwanda vya kukoboa mpunga na kuwakata mapanga walinzi

Katavi. Walinzi wawili katika viwanda vya kukoboa mpunga vya  Mpanda Hoteli Manispaa ya Mpanda,  wamekatwakatwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao baada ya kuvamiwa na majambazi waliofanikiwa kupora Sh15 milioni mali ya mmiliki mmoja wa kiwanda Mashauri Noni.

Wakizungumza na Mwananchi Digital mmoja wa waathirika, Mashauri Noni amesema majambazi hao walivamia kiwandani hapo Desemba 13,2020 saa 5:00 usiku kisha kumkatakata kwa mapanga mlinzi wake Abeli Samweli mkazi wa Mpanda Hoteli hali iliyosababisha kulazwa hospitali ya rufaa mkoa wa Katavi.

Mmoja wa mashuhuda mlinzi wa mashine jirani Yesu Zakayo (53) mkazi wa Katumba alisema wakati mvua inanyesha saa 7:00 usiku aliona mtu anakuja lindoni kwake alipofika alikaa chini pasipo kumtambua baadaye alimweleza amekatwa mapanga alipomwangalia alimtambua kuwa ni Abeli Samweli mlinzi jirani alimuomba amuitie mke wake.

Mganga Mfawidhi hospitali ya rufaa mkoa wa Katavi Yustina Tizeba amekiri kuwapokea majeruhi hao watatu akidai kuwa mmoja alitibiwa na kuondoka na wawili wamelazwa hospitalini hapo lakini Abeli Samweli hali yake ni mbaya wanaandaa utaratibu wa kumpatia rufaa kwenda kutibiwa mkoani Mbeya.

Jeshi la Polisi mkoani Katavi limethibitisha kutokea tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini watuhumiwa waliohusika na tukio hilo.