Majengo 21 UDSM kujengwa kuongeza wanafunzi 

Muktasari:

  • UDSM imeingia mkataba wa ujenzi na upanuzi wa kampasi zake jumla ya majengo 21 kujengwa na kukarabatiwa kutoa wigo wa wanafunzi wengi kujiunga. 

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeanza safari ya ujenzi wa kampasi mpya katika mikoa mbalimbali nchini ikiwa ni hatua ya kuendeleza upatikanaji wa elimu ya juu nchini.

Hatua hii inafuatia kusainiwa kwa mkataba wa usimamizi wa ujenzi na kampuni mbili, M/s Arqes Africa Architects & Interior Designers Limited na M/s Geometry Consultants Limited, kusimamia ujenzi wa majengo 21.

Ujenzi huu unaendana na agizo la Serikali la kuanzisha kampasi kuu za vyuo vikuu katika maeneo ambayo vyuo vya elimu ya juu vilikuwa vichache hivyo kupanua fursa za elimu nchi nzima.

UDSM ni mnufaika wa mradi wa Benki ya Dunia wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET), ukiwa na lengo la  kuimarishaji wa mazingira ya kujifunzia na upatanishi wa programu za kipaumbele na mahitaji ya soko la ajira katika taasisi za elimu ya juu zinazofaidika.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika leo Novemba 2 chuoni hapo, Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa William Anangisye amesema utekelezaji wa mradi wa HEET unafanyika sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, na Ilani ya Uchaguzi ya CCM yam waka 2020-2025.

Amesema kwa pamoja vinalenga katika kuimarisha uchumi wa viwanda ili kuendana na uchumi wa kati, na kuongeza fursa za ajira kwa makundi mbalimbali hususan vijana.

“Sisi tunajiona kuwa na bahati kubwa sana kufikiwa na mradi huu kwani unarandana na Dira yetu ya UDSM Vision 2061 na mpango mkakati wa Chuo 2020/21-2024/25 zinazolenga kufanya mageuzi ya kitaasisi yanayoendana na vipaumbele na mahitaji ya taifa ya sasa na baadaye.

“Hivyo Utekelezaji wa Mradi wa HEET umejikita kwenye kuimarisha na kuboresha miundombinu, ikiwemo ukarabati mkubwa na ujenzi wa majengo mapya pamoja na kufunga vifaa vipya kwenye majengo haya. Ni katika muktadha huo, chuo kinajipanua na kuwafikia Watanzania zaidi,”

Profesa Anangisye amebainisha kuwanutekelezaji wa kazi hizo za kimkakati umezingatia masuala mtambuka ikiwemo masuala ya jinsia, fursa sawa kwa wote, utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi. 

“Chuo kinahakikisha, kupitia ofisi ya usimamizi wa mradi, wadau wote wanashirikishwa katika hatua zote za utekelezaji wa mradi.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Balozi Mwanaidi Majar amesema utakuwepo ufuatiliaji wa karibu utekelezaji wa mradi huo unaopaswa kuleta tija kubwa katika nyanja mbalimbali za taaluma, utafiti na huduma kwa umma hapa chuoni.

Mwanaidi amesema kwa kutumia vyombo vyake mbalimbali, baraza litahakikisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unafanyika wa weledi na uadilifu ili kuhakikisha kuwa utekelezaji huo unakamilika kwa wakati, kulingana na muda uliowekwa. 

“Tunasisitiza kuwa kila mmoja anayehusika kwa namna moja au nyingine katika utekelezaji wa mradi huu atimize wajibu wake kwa ufanisi inavyopaswa na kwa wakati unaotakiwa.

“Baraza la chuo lina imani kubwa kuwa kampuni zikizosaini mikataba nayo yamepatikana kwa hatua na vigezo vyote vinavyotakiwa, kama ambavyo imekuwa jadi na utamaduni wa chuo chetu,” amesema Mwanaidi Maajar.

Makamu Mkuu wa chuo hicho- Mipango, Fedha, na Utawala, Profesa Bernadeta Killian amesema kukamilika kwa michoro ya majengo na kushirikisha washauri elekezi kusimamia ujenzi wa Dar es Salaam, Lindi na Zanzibar. 

"Chuo kikuu kinatekeleza Mradi kupitia nyanja za kipaumbele za kitaifa ambazo ni pamoja na: Uhandisi na Teknolojia, ICT, Mipango Miji, Uhandisi wa Mazingira na Teknolojia, Kilimo na Biashara ya Kilimo, na Utalii na Ukarimu.

"Mafunzo kwa wanataaluma juu ya matumizi ya teknolojia ya habari ya kufundishia yametolewa kwa wanataaluma 79, na mafunzo haya yanaendelea kwa kuzingatia zoezi la uhakiki wa mitaala," amesema Profesa Bernadeta