Majeruhi wa ajali ya ‘ambulance’ Same ahamishiwa KCMC
Muktasari:
- Mmoja wa majeruhi wa ajali iliyouwa muuguzi na dereva wa zahanati ya Kisiwani wilayani Same,Parasetwi Peutu(50) amehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini(KCMC) baada ya kuumia vibaya kwenye pingili za uti wa mgongo.
Moshi.Mmoja wa majeruhi wa ajali iliyouwa muuguzi na dereva wa zahanati ya Kisiwani wilayani Same, Parasetwi Peutu (50) amehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) baada ya kuumia vibaya kwenye pingili za uti wa mgongo.
Ajali hiyo iliyopoteza maisha ya watu wawili na majeruhi watatu ilitokea Agosti 7 mwaka huu katika eneo la Majevu, kata ya Kisima, barabara ya Same- Kisiwani wilayani humo baada ya tairi la nyuma la gari hilo kupasuka na kupoteza mwelekeo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Agosti 9, 2021 Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema majeruhi ambaye ndiye aliyekuwa mgonjwa na aliyekuwa akipelekwa hospitali ya wilaya Same, Ester Laizer (35) anaendelea vizuri.
Aidha amesema majeruhi mwingine Magdalena Lucas ambaye ni mama wa Ester pamoja na mwanaye wanaendelea vizuri na huenda wakaruhusiwa kutoka hospitalini leo au kesho.
"Ester ambaye ndiye aliyekuwa mgonjwa anaendelea vizuri na kati ya leo au kesho ataruhusiwa kutoka hospitalini baada ya afya yake kutengamaa,"amesema Kamanda Maigwa
Awali Kamanda Maigwa amesema ndugu hao walikuwa wakimsindikiza mgonjwa huyo katika hospitali ya wilaya ya Same baada ya kuishiwa damu kutokana na kuvuja damu nyingi puani.
Jana Kamanda Maigwa aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Joshua Methew(29) ambaye ni Muuguzi wa zahanati ya Kisiwani na Jumanne Makumbe(48) ambaye ni dereva baada ya gari lao kupasuka gurudumu la nyuma na kuanguka.